Kanuni ya 33(1) ya Ligi Kuu Tanzania Bara inasema: “Mwalimu Mkuu wa timu atawajibika kutambua wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa. Katibu Mkuu atafanya masuala ya utawala, atakamilisha shughuli ya usajili wa wachezaji na kuwasilisha mikataba na fomu ya majina TFF kwa wakati.”
Nini sababu au madhumuni ya kanuni hiyo? Kwa kifupi kanuni hiyo inaainisha majukumu ya kocha (mwalimu) kama mtaalamu wa mpira wa miguu katika timu na Katibu (mtawala) kama mtaalamu wa uongozi katika klabu.
Kwa mujibu wa kanuni ya 33(3), walimu (makocha) wa klabu wanawajibika kutangaza majina ya wachezaji wanaoachwa, wanaositisha mikataba, uhamisho na usajili wa wachezaji katika kipindi kitakachotangazwa na TFF.
Usajili unafanywa ili kuziba nafasi ambayo iko wazi au kuimarisha timu kwa lengo la kufanya vizuri. Unapotaka kuimarisha timu ni lazima uwe na nafasi ambayo inaweza kutengenezwa kwa kuuza mchezaji, kuvunja mkataba wake au kutakiwa mahali kwa mkopo.
Kimsingi usajili una sura mbili tu. Kocha na mchezaji. Ni kocha kama mtaalamu wa mpira wa miguu kwa niaba ya klabu anayepanga au kuamua ni mchezaji wa aina gani anatakiwa kusajiliwa na kwa lengo lipi.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingi za Afrika zina wachezaji wenye uwezo na vipaji. Lakini kuwa na kipaji kwa mchezaji ni kitu kingine kama ilivyo kwa mchezaji mwenye uwezo.
Hili ni eneo ambalo lina matatizo makubwa kwa wachezaji wa Tanzania. Kwa lugha yenye kueleweka ni kuwa kuna wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kucheza mpira wa miguu lakini bado hawajatambua nafasi zao.
Kutojitambua ni pamoja na mchezaji kutojua ni kwa nini anakwenda klabu X badala ya klabu Y. Nini mustakabali wake katika mpira wa miguu ambayo ni ajira isiyo na kiinua mgongo, lakini ni mchezo ambao umri ni moja ya vigezo vya msingi.
Katika uga wa mpira wa miguu Tanzania ni jambo la kawaida kwa mchezaji anayeng’ara kwenye klabu Y kuamua kwenda klabu X kwa vile tu ameonyeshwa fedha.
Ni kweli kila mtu anahitaji fedha katika maisha yake ikiwamo kutatua matatizo mbalimbali yanayomzunguka. Fedha katika hali ya kawaida ni kila kitu, kwani inaweza kuhamisha hata mlima. Lakini fedha hiyo unaichukua kwa utaratibu gani?
Ni kawaida mchezaji anayecheza katika kikosi cha kwanza katika klabu X kwenda klabu Y huku akijua dhahiri hawezi kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.
Kwa mchezaji mwenye uwezo wa kucheza mpira wa miguu uamuzi wa aina hiyo ni wa kujimaliza.
Inaweza kuwa ni matatizo ya fedha yanamsukuma mchezaji kufanya uamuzi wa aina hiyo. Lakini kama kweli ni matatizo kwa nini aingie mkataba wa muda mrefu? Pata fedha, lakini uvumilie kukaa kwenye benchi kwa msimu mmoja tu.
Wapo wachezaji wenye uwezo wa kucheza mpira wa miguu, lakini hawaonekani kwa vile tu wameamua kukaa kwenye klabu Y wakati hawana nafasi katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo.
Unaweza kukaa misimu minne ukiwa benchi kwenye timu moja wakati una uwezo wa kucheza mpira wa miguu katika klabu za Ligi Kuu zilizobaki.
Hiki ni kipindi cha usajili. Lakini ni kipindi ambacho wachezaji wenye uwezo na vipaji wanatakiwa kufanya uamuzi mgumu kwa lengo la kulinda uwezo na vipaji vyao, vinginevyo watasahaulika katika medani hii ya mpira wa miguu.
Fursa ya kuchezea Timu ya Taifa (Taifa Stars) iko wazi kwa mchezaji yeyote mwenye uwezo, na anayecheza katika kikosi cha kwanza katika klabu yake. Hakuna kocha anayeingiza mchezaji kwenye Timu ya Taifa wakati hana nafasi hata katika klabu yake.









