Simba, Yanga imarisheni timu B kuokoa mamilioni

16Jul 2022
Mhariri
Nipashe
Simba, Yanga imarisheni timu B kuokoa mamilioni

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara inayoshirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini unatarajiwa kufunguliwa rasmi ifikapo Agosti 17, mwaka huu.

Lakini ligi hiyo itafunguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa Agosti 13, mwaka huu kwa kuwakutanisha mabingwa wapya Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga dhidi ya mshindi wa pili, Simba.

Watani hao wa jadi kutoka Kariakoo jijini Dar es Salaam wanakutana kwa sababu Yanga ndio bingwa pia wa mashindano ya Kombe la FA, kama ilivyokuwa kwa msimu uliopita ambapo Wekundu wa Msimbazi alibeba makombe yote.

Lakini kuelekea msimu mpya, Simba, Yanga na timu nyingine zote zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ziko katika mchakato wa kusajili wachezaji wapya ili kuimarisha na kuboresha vikosi vyao kwa ajili ya msimu huo wa 2022/2023.

Timu zote zinasema zinafanya usajili kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti maalumu zilizowasilishwa na makocha wao baada ya kubaini mapungufu mbalimbali katika msimu uliomalizika.

Mchakato wa usajili huwa unafanywa na timu zote, kuanzia bingwa hadi timu mpya zilizopanda daraja, timu zilizoshuka daraja pia hujiimarisha kwa ajili ya kwenda kupambana katika changamoto mpya waliyoangukia.

Lakini pia timu zilizomaliza nje ya malengo yake pia hufanya jitihada mbalimbali za kujenga vikosi vyao kwa ajili ya kuanza msimu mpya wakiwa imara.

Unaweza kusema jambo hili ni la kawaida, lakini kwa upande wa Ligi Kuu Tanzania Bara hali imebadilika kutokana na motisha inayotolewa na wadhamini wenza wa ligi hiyo ambao wana haki ya kuonyesha michezo yote kwenye televisheni ambao ni Kampuni ya Azam Media.

Wadhamini hawa hutoa motisha kuanzia kwa bingwa mpaka timu iliyoshuka daraja lakini kwa viwango vya fedha tofauti. Kwa maana hiyo, msimu uliopita kila timu ilijiwekea malengo ili kupata motisha kubwa ambao inaamini itawasaidia kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

Ili kupata vikosi imara, kila timu imekuwa ikihangaika ndani na nje ya Tanzania kusajili wachezaji watakaowasaidia, lakini wakati ikifanya hivi kuimarisha vikosi vyao vya kwanza, timu zimekuwa nyuma kusajili wachezaji wenye vipaji kwa ajili ya timu zao za vijana za umri chini ya miaka 17 na 20, ambazo kwa hakika ndio msingi wa kupata timu A.

Mbali na kufanya mchujo (scouting) ya kupata nyota wanaosajiliwa kwa ajili ya timu hizo, kumekuwa na tatizo la kushindwa kuwatunza yosso hao kama inavyotakiwa na matokeo yake wanaposhiriki katika mashindano ya U-17 na u-20, hutolewa mapema au baadhi ya timu hushindwa kupeleka yosso hao kuchuana.

Umefika wakati, Simba, Yanga, Azam FC kuwekeza kikamilifu katika timu za vijana kwa sababu kwa kufanya hivyo, sio tu kutawapa nafasi yosso wao kuonekana, lakini itawapunguzia gharama ya kutumia kiasi kikubwa cha fedha kusajili wachezaji wa kigeni au kutoka katika timu nyingine.

Klabu inapokuwa na timu imara za vijana, basi hupata nafasi ya kupandisha baadhi ya nyota wake walioiva na hivyo, hupunguza bajeti ya kusajili wachezaji wapya kutoka sehemu nyingine.

Ukiondoa vigogo hawa wa soka wenye wadhamini mbalimbali pamoja na Azam FC inayomilikiwa na mfanyabiashara mkubwa wa hapa nchini, timu nyingine zinatakiwa kujikita kutunza timu za vijana ili ziwasaidie katika kuboresha vikosi vyao bila ya kutumia fedha kiasi kikubwa kama ilivyo sasa.

Kwa kufanya hivi, si tu kutaokoa mamilioni ya fedha kusajili wachezaji wageni au kutoka nje ya klabu husika, lakini pia kutasaidia kuzijenga timu za taifa ambazo zinategemea kupata wachezaji kutoka kwa klabu za hapa nchini.

Ushauri huu pia unawahusu wote wanaomiliki timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake Tanzania ingawa inafahamika inahitaji kuwa na bajeti ya kutosha kuhudumia timu B.

Kama ambavyo Simba, Yanga, Azam na timu nyingine zina ndoto ya kufikia mafanikio ambayo Al Ahly, Zamalek kutoka Misri, Mamelodi Sundowns ( Afrika Kusini) au RS Berkane ya Morocco, basi wakati umefika wakafuata nyao zao kwa kuwa na akademi au timu za vijana imara na si kukusanya na kuwaweka yosso pamoja kutimiza matakwa yaliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kushiriki Ligi Kuu.