Kwa sasa unga wa ugali umepanda kutoka Sh. 1,000 kwa kilo hadi 2,000, huku dagaa wakipanda kutoka 6,000 hadi 8,500 kwa jiji la Dar es Salaam.
Kilo ya mchele mzuri uliokuwa ukiuzwa Sh. 1,500 sasa umpenda hadi Sh. 2,500 huku unga wa ngano ukipanda kutoka Sh. 1,200 hadi Sh. 2,000.
Kupanda kwa bei hizo pia kunachangiwa na mavuno kutokuwa mazuri kwenye msimu uliopita kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo yamesababisha mvua kuwa kidogo.
Kwa ujumla gharama za maisha zimezidi kuongezeka na bei zinaongezeka kila kukicha kwenye kila bidhaa, jambo ambalo linawafanya watu kuhaha namna ya kuendesha familia kwa kipato walichonacho.
Bidhaa kwenye masoko zimeendelea kupanda na sasa ni vigumu kupata kitu kinachouzwa Sh. 500, vingi vinaanzia Sh.1,000 kwenda juu zikiwamo nyanya, vitunguu, bamia, hoho, karoti na ndizi.
Wakulima wameamua kuuza mazao kabla ya kuyavuna kwa kuwa wanunuzi kutoka maeneo mbalimbali wanafika bei, kiasi kwamba chakula kinakwenda kwenye masoko mengine na ya ndani yakikosa.
Serikali imeeleza jitihada mbalimbali ikiwamo kuwa na hifadhi ya chakula, lakini bado kuna tatizo la kufuatilia bei kwa kuwa wanufaika wakubwa ni mawakala ambao huwaulizia wachuuzi wa chini wanaouza sokoni.
Hali ya maisha ya mkulima inazidi kuwa mbaya kila siku na kubaki kufanya kilimo cha mazoea ambacho hakimkwamui kiuchumi, huku mchuuzi wa mwisho akibaki kuwa muuzaji mdogo mdogo asiyepiga hatua kubwa kimaisha.
Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, alikaririwa akiahidi kutoa tamko la serikali Julai 15, mwaka huu.
Pia anakiri kuwapo upungufu wa uzalishaji msimu wa 2021/23 akiba ya msimu wa 2020/21 ikiisha, na kwamba mahitaji yameongezeka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kuwa mvua zilikata zikaathiri mazao kukomaa.
Ni muhimu serikali ikaendeleza mkakati wa kuelimisha wananchi umuhimu wa kuhifadhi chakula, hasa wakulima kutoshawishika na bei wanazopewa kwa kuwa wakihifadhi watapata zaidi.
Pia ni muhimu kuhamisha na kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji ambacho hakiathiriwi na ukosefu wa mvua.
Ni muhimu kufundisha kuhifadhi na kusindika vyakula hasa msimu ambao kinazalishwa kwa wingi ili kusaidia kuwa na uhakika wa chakula hasa nyakati ambazo kuna uhaba.
Kwa sasa hali ni ngumu kwa kuwa watu hawana utamaduni wa kuhifadhi, hawajui njia bora za uhifadhi wa chakula na umuhimu wake, ndiyo maana kuna haja ya kutoa elimu sahihi kwa wakati sahihi.
Tanzania imejaliwa mikoa ambayo ni wazalishaji wakubwa wa chakula, ni muhimu wakulima wakaelimisha mbinu za kilimo bora kinachohimili hali ya hewa iliyopo.
Kuwa na ufuatiliaji wa karibu wa shughuli za kilimo na kutoa ushauri wa mara kwa mara, pia kufuatilia kama ushauri unafanyiwa kazi ipasavyo.
Mwaka jana Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), walitoa tahadhari ya uwepo wa mvua chache na kushauri aina ya mazao ambayo hayahitaji mvua nyingi, lakini kwa kuwa hakukua na ufuatiliaji wakulima waliendelea kulima mazao yale yale na hawakupata mavuno.









