Ajali ya kwanza wamefariki dunia watu wanane akiwamo mama na watoto wake wanne waliokuwa wanasafiri kwenda Ngara. Chanzo cha ajali hiyo kimeelezwa kuwa ni uzembe wa dereva wa lori lililokuwa linatokea Rwanda na katika ajali ya pili chanzo ni mwendo kasi wa dereva wa gari mojawapo.
Matukio ya ajali kwa sasa yameongezeka na kumekuwa na taarifa juu ya matukio hayo siku hadi siku. Mfano, Juni 5, mwaka huu, watu watano walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa katika ajali iliyotokea eneo la Inyala, mkoani Mbeya, chanzo kikiwa lori lililobeba shehena ya mahindi kufeli breki na kugongana na basi dogo.
Ajali nyingine ni ya treni iliyotokea Kata ya Malolo mkoani Tabora na kusababisha vifo vya watu wanne na 132 kujeruhiwa.
Kama vile haitoshi, Juni 25, mwaka huu, watu sita wakiwamo wanne wa familia moja katika eneo la Inala, mkoani Tabora, wakati wakienda kwenye mazishi ya mama yao, walifariki dunia chanzo kikidaiwa ni gari hilo kuhama upande wake na kwenda kwenye uvungu wa lori.
Julai 9, mwaka huu, askari wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wa kikosi cha 825 KJ kambi ya Mtabila wilayani Kasulu, Kigoma, walifariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.
Wimbi la ajali limeendelea kurindima baada ya jana wanafamilia watatu kufariki dunia katika ajali wakati wakitoka hospitalini kumpeleka mtoto wa mwaka mmoja na nusu kupata sindano za saa. Pikipiki yao iligongwa kwa nyuma na kisha kukanyangwa na gari na miili yao kuharibika.
Kutokana na ajali hizo, watu 87 wamefariki dunia kuanzia Juni 5, mwaka huu. Hizo ni ajali chache kati ya nyingi zilizoripotiwa huku kukiwa na za watu kugongwa na magari, bodaboda na bajaji.
Kwa hali ilivyo, ni lazima sasa taifa sasa kuona hili ni tatizo kubwa linalomeza watu wetu, kusababisha ongezeko la umaskini, mzigo kwa familia kutunza na kuuguza majeruhi, kuongeza wenye ulemavu ambao ni tegemezi wanaoshindwa kuhudumia familia zao ambazo nazo zinakuwa tegemezi. Ajali hizo pia zinasababisha hospitali kuelemewa na majeruhi pamoja na familia kubeba mzigo mkubwa wa gharama.
Kasi ya madereva kutoheshimu kwa hiari sheria za usalama barabarani inaongezeka na ndiyo maana siku hizi ajali ni tukio linaloongoza kuteketeza maisha ya wananchi.
Kwa ujumla, kampeni za kukabiliana na ajali hizi zinapaswa kufanyika huku viongozi wa kila ngazi wakiwakumbusha madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani. Kinyume cha hapo, tatizo hilo litaendelea huku taifa likizidi kupoteza mamilioni ya kodi.
Pia nguvu kazi na umaskini vitaingia kwenye baadhi ya familia hasa ambazo baba au mama aliyekuwa anategemewa kwa kila kitu anapofariki dunia au kujeruhiwa na kuuguzwa kwa muda mrefu na hatimaye kupata ulemavu wa kudumu ambao utasababisha ashindwe kufanya shughuli za kuingiza kipato katika familia.









