AMECEA iliyokutana kujadili ajenda kuu ya ulinzi na utunzaji wa mazingira, tunawapongeza wanachama wake kujitokeza na kueleza waziwazi kuwa kama taifa na dunia hatutalinda na kuhifadhi mazingira kuna hatari ya kuangamia nasi tukiwa wahanga.
Wanachama wa mabaraza hayo kutoka Ethiopia, Eritrea, Kenya, Malawi, Tanzania, Uganda, Sudani na Sudani ya Kusini, Zambia na waalikwa kutoka Djibouti na Somalia wametafakari mzigo mkubwa unaozielemea nchi zao kutokana na uharibifu wa mazingira na kukemea tabia ya mwanadamu ya kuharibu maumbile.
Baadhi ya changamoto za uharibifu wa mazingira zinazotajwa na Maaskofu ni mengi kama ukame na njaa za mara kwa mara, upepo na vimbunga, mvua zisizotabirika, mafuriko, wadudu kama nzige ambao hata mwaka huu walionekana kwenye ukanda wa AMECEA.
Wakati mkutano huo, umemalizika Dar es Salaam juzi, upatikanaji wa mahindi katika mikoa mingi mwaka huu ni changamoto, mazao mengine kama mpunga pia yamekwamishwa na ukame.
Tukiangalia huduma muhimu za kijamii kama maji zinaendelea kuwa tatizo kutokana na vyanzo vingi kuharibika. Siyo siri, mito mingi inakauka, mabwawa na hata maziwa kama Rukwa nayo yamepungua kina, aina kadhaa za samaki zimetoweka.
Aidha, maziwa mengine makubwa kama Victoria na Tanganyika kina kinaongezeka kutokana na sababu kadhaa lakini mojawapo ni kujaa tope (silt) na taka.
Kadhalika, misitu ya asili iliyokuwa vyanzo vya maji na mito mikubwa vimekuwa makao ya taka za plastiki na hata za kilimo na za sumu mathalani, Ziwa Victoria.
Hii ni rasilimali inayotumiwa na nchi wanachama wa AMECEA, kuanzia Tanzania, Uganda na Kenya lakini ni chanzo cha Mto Nile unapita Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini, hadi Bahari ya Mediteranian.
Maji yake ni muhimu kwa maendeleo ya nchi nyingi za Afrika, kadhalika Ziwa Victoria nalo lina umuhimu wa kipekee kwa kuwa ni mama wa Mto Nile, hivyo linahitaji kulindwa na kutunzwa vingine kama AMECEA wanavyosema kuna kitisho cha dunia kutoweka kutokana na uharibifu wa mazingira unaotishia hatima ya watu na viumbe kama wanyama, mimea, wadudu na hewa angani.
Tunaona kuwa wanachosema maaskofu hawa ni ukweli, wanaeleza kuwa kunahitajika mikakati mipya ya kichungaji, kitaifa, kikanda na kimataifa ili kulinda ikolojia ambao ni uhusiano wa binadamu na mazingira na kuzuia mabadiliko zaidi ya tabia nchi ambayo yasipodhibitiwa yataathiri kila mtu.
Mikakati na matendo ili tuweze kusafiri kwa pamoja katika nia ya kubadilika katika Kanda ya Afrika Mashariki na kote Afrika inahitajika, mojawapo ni kuzuia mizozo na vita vinavyoathiri mazingira na kuongeza umaskini kutokana na kukosekana chakula, malisho ya wanyama, ardhi ya kilimo, maji na hata kuibuka maradhi.
Tunaungana na serikali na maaskofu kusisitiza kulinda na kutunza mazingira kwa kuwahamasisha watu kubadilika na kufahamu kuwa mabadiliko ya tabianchi siyo hadithi wala ndoto ni ukweli unaoonekana kwenye ukame, mafuriko na vimbunga vinavyowatesa hata sasa.
Tunaisihi jamii kuacha kukata misitu kwani kasi ya misitu ya asili kutoweka inatisha. Ili kukabiliana uhaba wa nishati ya kupikia serikali isaidie kwa kutoa ruzuku ya gesi, umeme na vifaa vya kupikia ili kupunguza na mwisho kuacha matumizi ya kuni na kuchoma mkaa.
Aidha, kuanzia sasa kuwe na kampeni kabambe za kupanda miti ya asili inayolinda maji, ardhi, pia kuhifadhi, misitu, maji, viumbe na kufundisha elimu ya mazingira kwa kina ili kuiokoa Tanzania na mabadiliko ya tabia nchi.









