Shime tujiandae kuhesabiwa kwa maendeleo

20Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Shime tujiandae kuhesabiwa kwa maendeleo

WAKATI elimu na uhamasishaji wa wananchi kushiriki Sensa ya Watu na Makazi, inayotarajiwa kuanza Agosti 23, mwaka huu, ikiendelea jamii imetakiwa kujijengea uelewa wa umuhimu wa siku hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mtakwimu ya Taifa (NBS), kwenye tovuti yake, utekelezaji wa sensa utafanyika kwa awamu tatu ambazo ni kabla ya kuhesabu, wakati wa kuhesabu na baada ya kuhesabu watu. 

Kipindi cha kabla ya kuhesabu watu kinajumuisha mambo mbalimbali, ikiwamo uandaaji wa kitabu cha mkakati wa usimamizi na utekelezaji wa sensa na nyaraka nyingine. 

Pia, utengaji wa maeneo ya kuhesabia na uzalishaji wa ramani na uandaaji wa madodoso na miongozo mbalimbali na uhamasishaji.

Kipindi baada ya kuhesabu watu kinajumuisha uchakataji wa taarifa za Sensa, uchambuzi, utoaji wa matokeo ya awali, usambazaji wa matokeo ya mwisho, uhamasishaji wa matumizi ya takwimu kwa watumishi wa wizara, Idara na taasisi za serikali. 

Elimu ya sensa inatolewa ili jamii ifahamu umuhimu wa kutoa ushirikiano kwa makarani watakao kuwa wamepewa kazi ya kuchukua taarifa muhimu. 

Uhamamishaji huo unazingatia kuitaka jamii kutoa taarifa zitakazowezesha serikali kupanga mipango yake ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wake. 

Bila kuwa na takwimu sahihi ya idadi ya watu ni vigumu serikali kupanga bajeti itakayotosheleza mahitaji ya wananchi wake kuanzia kwenye sekta ya afya, elimu na huduma muhimu za maji na umeme. 

Idadi ya watu ndiyo mwongozo utakaowezesha serikali kutambua katika kuleta maendeleo inajipanga vipi kutokana na idadi hiyo. 

Ni lazima makundi yote ya watu yajulikane kuanzia wazee, vijana, watoto, wanawake na wanaume ili kutoa picha nzuri itakayoongoza katika mipango hiyo. 

Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakificha kundi fulani likiwamo la wenye ulemavu na kulikosha haki ya kunufaika na mipango ya serikali. 

Watoto wenye ulemavu wamekuwa wakikosa haki yao ya kupata elimu kutokana na baadhi ya wazazi kuwaficha ndani ili wasitambulike kwenye jamii. 

Hali hii imesababisha watoto hao kusoma misaada mbalimbali ikiwamo ya vifaa vya kuwawezesha kurahisisha maisha yao. 

Katika kuhakikisha uchukuaji taarifa za sensa unakwenda vizuri, makarani watakaoteuliwa kufanyakazi hiyo ni lazima wajue jinsi ya kutumia lugha nzuri wanapokwenda kwa wananchi. 

Wengine hugoma kutoa taarifa zao kwa sababu tu hakuongozwa vizuri kwa lugha itakayomfanya mtu atoe ushirikiano bila kikwazo. 

Wasimamizi wa sensa pia wanatakiwa kuwa waadilifu kwa kutunza siri zitakazotolewa na wananchi kwani hiyo pia ni changamoto inayofanya watu washindwe kutoa taarifa zao kwa kuogopa taarifa zao kusambazwa kusikostahili. 

Serikali imetumia gharama kubwa kuhakikisha zoezi hilo linakwenda vizuri, kuanzia kwenye vifaa vitakavyotumika hadi kwa watu watakaochukuliwa kufanya kazi hiyo. 

Ni vizuri basi lengo hilo ambalo serikali imejiwekea kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wananchi wake, lisiharibiwe na watu wachache.

Kwa ushirikiano hakuna jambo litakaloshindikana na maendeleo yatapatikana kwa wote.