Utaratibu kusikiliza kero za wastaafu umekaa vyema

21Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Utaratibu kusikiliza kero za wastaafu umekaa vyema

SERIKALI imeanza utaratibu wa kusikiliza kero za wastaafu na kuzishughulikia.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako, amejipanga kupiga kambi kwenye mikoa mitatu nchini.

Ameanza na kambi hiyo mkoani Dodoma huku miongoni mwa kero zilizoibuka ni kupunjwa mafao.

Katika usikilizaji wa kero hizo kikao kilijumuisha Wakurugenzi na Watendaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PSSSF.

Hatua hiyo ya Prof. Ndalichako inatokana na kupokea kero mbalimbali za wastaafu, tangu ashike wadhifa katika wizara yake kwa kipindi cha miezi sita.

Hii ni hatua nzuri ambayo inaleta matumaini kwa wananchi kuiamini serikali yao na watendaji wake wanaosikiliza kero zao.

Mtu anapostaafu anategemea mafao yake ndiyo yamwezeshe kuendesha maisha yake mpaka kifo kitakapomfika.

Michango yake anayowekeza katika mifuko ya hifadhi ya jamii anajua ipo salama na hata anapofikia wakati wa kustaafu anajua kuwa fedha zake za mafao atazipata bila usumbufu.

Inapotokea kuwapo usumbufu wa aina yoyote ilhali mstaafu akiwa na taarifa zake zote za kumpatia mafao yake, haipendezi na inavunja moyo kwa wengine wanaowekeza katika mifuko hiyo.

Baadhi ya wastaafu wanalalamika kutopata mafao yao kwa muda wa miaka miwili wakati kimsingi yanatakiwa kulipwa ndani ya siku 60 tangu mtu astaafu.

Hata hivyo, kuna hoja ya vitu vinavyohitajika katika usimamizi wa mifuko ambayo imetakiwa kuwa na kauli moja wakati wanapohudumia wateja wao.

Mfano hoja ya mtumishi aliyekuwa anafanya sekta binafsi, lakini baadaye kuajiriwa serikalini akiwa na umri wa miaka 58, kiutaratibu kulipwa mafao ni mpaka afikishe miaka 60.

Mtu huyo anatakiwa kupata ushauri kwa wataalamu.

Mkanganyiko unapotokea, tunamshukuru Waziri Ndalichako kuagiza mafao ya aina hiyo yakokotolewe upya.

Waziri Ndalichako, anatarajia pia kuwasikiliza wastaafu kwenye mikoa mingine ya Dar es Salaam na Mwanza ambako kuna wastaafu wengi.

Ameahidi kuangalia changamoto za wastaafu bila kujali walistaafu lini na yeyote mwenye changamoto ya mfuko wa NSSF au PSSSF, serikali itahakikisha inawapatia ufumbuzi ndani ya muda mfupi.

Katika kero hizo Waziri Ndalichako amebaini baadhi ya watumishi walipandishwa vyeo, lakini mshahara haukubadilishwa hadi anastaafu.

Tunapongeza kwa ufafanuzi kuwa mtu wa aina hiyo kama alikuwa mtumishi wa umma na kama alibadilishwa atalipwa arrears (malimbikizo) tangu alipopandishwa cheo hadi anastaafu na atalipiwa pia tofauti iliyotakiwa kulipwa kwenye mifuko na ataongezewa kwenye mafao yake.

Ni matumaini yetu kuwa utaratibu huu utaondoa manung’uniko na vilivyo vya wastaafu kucheleweshea mafao yao na baadhi ya kupunjwa.

Ni vyema pia wastaafu wakahakikisha wanahakiki taarifa zao vizuri hata wanapofikia umri wa kupata mafao yao kusitokee tena ucheleweshaji na visingizio visivyokuwa na tija.