Mchakato marekebisho Sheria Makosa Jinai ufanyike haraka

22Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mchakato marekebisho Sheria Makosa Jinai ufanyike haraka

TAARIFA kuwa makosa ya ubakaji na ulawiti yapo mbioni kuondolewa, dhamana zinatia moyo kutokana na vitendo hivyo kushamiri katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Taarifa zinasema serikali inatarajia kuanza mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Suala la watu wanaotuhumiwa kufanya ukatili wa kijinsia ukiwamo ubakaji, udhalilishaji wa watoto, kuachiwa kwa dhamana wanapofikishwa mahakamani, limekuwa likilalamikiwa na watu wengi.

Malalamiko hayo yanatokana na baadhi ya washtakiwa hao au watuhumiwa wanapoachiwa hurudi mitaani na kuendeleza vitendo hivyo.

Utafiti mdogo uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka umegundua kuwa baadhi ya watuhumiwa wa makosa hayo wakiwa nje kwa dhamana wanakimbia na wengine kuharibu ushahidi au kumalizana na wazazi ama ndugu wa mwathirika wa vitendo hivyo.

Wanaharakati wa haki za binadamu na wadau wanaotetea haki hizo, kila mara wamekuwa wakiomba marekebisho ya sheria ili zile zenye upungufu ziweze kurekebishwa na kutenda haki.

Katika mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, serikali inakusudia kukutana na wataalamu kupata maoni yatakayosaidia kujenga hoja ya kufanya makosa hayo kutokuwa na dhamana ili kupunguza matukio hayo kwenye jamii.

Hatua hiyo ni ya kupongezwa kwa sababu kila siku kumekuwa na matukio ya udhalilishaji na ukiukwaji wa haki za binadamu kutokana na vitendo vya ukatili.

Serikali imesema katika marekebisho hayo wanalenga kulinda kundi la watoto na wanawake ambao ni waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili.

Pia imeelezwa kuwapo nia ya kupitia sheria nyingine ambazo zinamgusa mtoto ili ziweze kuendana na hali halisi iliyoko katika jamii kuwasaidia watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili katika jamii.

Wameangalia pia katika sheria mbalimbali zikiwamo sheria za Zanzibar ambazo zimeweka kosa la ulawiti kutokuwa na dhamana ili kusaidia kuwalinda watoto na wanawake dhidi ya vitendo hivyo.

Katika kuangalia suala hilo, baadhi ya makosa hasa ya ulawiti inaonyesha yakizungumzwa kwa jamii, itakwambia ni sahihi kukosa dhamana hasa katika kulinda mila na desturi za Tanzania.

Ni matumaini yetu kuwa wataalamu waliokutana kujadiliana namna bora ya kuhakikisha jamii inapata elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili, watahakikisha mchakato huu unakwenda haraka ili watoto na wanawake wanaofanyiwa vitendo hivyo waweze kulindwa.

Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2021, matukio ya ukatili kwa watoto yaliyoripotiwa ni 11,499, huku makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ni ubakaji (5,899), mimba kwa wanafunzi (1,677) na ulawiti (1,114).

Mikoa iliyoongoza kwa matukio ya ukatili ni Arusha (808), Tanga (691), Shinyanga (505), Mwanza (500) na Mkoa wa Kipolisi Ilala (489).

Vitendo hivyo vya ukatili sasa hivi vimekuwa vikishuhudiwa kufanyiwa watoto wa kiume, tofauti na ilivyokuwa imezoeleka kuwa wanaofanyiwa ukatili huo ni wa kike.

Wazazi, walezi na jamii ni jukumu letu pia kutoa ushirikiano ili tatizo hili liweze kukomeshwa kabisa.