Adhabu dhidi ya Manara iwe fundisho kwa wadau 

23Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Adhabu dhidi ya Manara iwe fundisho kwa wadau 

SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF), juzi lilitangaza kumfungia Msemaji wa Yanga, Haji Manara, kutojihusisha na masuala ya mpira kwa muda wa miaka miwili.

Sambamba na adhabu hiyo, msemaji huyo ametozwa pia faini ya Sh. milioni 20. 

Adhabu hiyo iliyotolewa na Kamati ya Maadili ya TFF, inatokana na Manara kubainika kufanya vitendo visivyo vya kiungwana na ukiukwaji wa maadili jambo ambalo halitakiwi katika mchezo wa soka.

Manara alitiwa hatiani kwa kumdhalilisha Rais wa Shirikisho hilo, Wallace Karia, baada ya kumtamkia maneno makali yenye mwelekeo wa utovu wa nidhamu wakati wa mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka la Azam kati ya Yanga na Coastal Union, iliyofanyika Julai 2, mwaka huu, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Kutokana na kauli hiyo, sekretarieti ya TFF iliwasilisha malalamiko mbele ya kamati ya maadili ambayo kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wakati wa hukumu, Manara alikiri kutamka, kuomba radhi.

Katibu wa Kamati hiyo, Walter Lungu, akisoma uamuzi, alisema Manara alipewa adhabu hiyo na faini, kulingana na Kanuni ya katiba ya TFF, kifungu cha 73(5) na (6) licha ya  kwamba aliomba msamaha kutokana na kitendo alichofanya.

Hii si mara ya kwanza kwa Manara kukumbwa na adhabu ndani ya TFF kwani amekuwa akifanya mambo kama hayo mara kwa mara na kupewa adhabu kwa mujibu wa kanuni zinazoongoza soka nchini.

Kwa adhabu hiyo, Yanga itakosa huduma za msemaji wao huyo kuanzia sasa hasa katika matukio makubwa yanayokuja, likiwamo la Wiki ya Wananchi, ambayo huandamana na masuala mbalimbali ya kijamii pamoja na kutambulisha kikosi kipya kwa msimu mpya wa ligi.

Sambamba na klabu kukosa huduma zake, umma wa wapenda soka watakosa uwapo wake hasa kutokana na hamasa ambazo amekuwa akifanya na kuwavuta mashabiki wa soka kupenda mpira. Bila kuwapo kwa unazi wa namna yoyote, ni ukweli ulio wazi kwamba Manara amekuwa kivutio kikubwa katika kuhamasisha mambo ya soka hususani linapokaribia pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga.

Awali, Manara alipokuwa Simba, alikuwa anawafanya mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kutega masikio atatoa kauli gani na hata alipohamia upande wa pili, alikuwa kivutio kwa kuipamba timu yake na watu kumiminika uwanjani kushuhudia mchezo.

Baada ya kutangazwa kwa adhabu hizo, kumekuwa na maoni kinzani kutoka kwa wadau huku baadhi wakisema adhabu hiyo ni kubwa na imetolewa kwa uonevu huku wengine wakisema kutokana na kujirudia mara kwa mara kwa matendo kama hayo anayoyafanya, anastahili na huenda ni ndogo kuliko iliyotarajiwa.

Pamoja na hayo yote, vitendo kama hivyo, tena vya udhalilishaji dhidi ya viongozi wa juu waliopewa dhamana ya kusimamia maendeleo ya soka nchini, adhabu aliyopewa ni sahihi kwa minajili ya kulinda heshima kwa mamlaka zilizokasimiwa jukumu la kuendeleza mchezo huo ambao unapendwa na mabilioni ya watu duniani.

Inawezekana kulikuwa na sababu ya yeye kufanya hivyo lakini kulingana na mazingira na kitendo kilichofanyika, ni dhahiri kwamba adhabu hiyo ni sahihi na kwa sasa inapaswa kuheshimiwa. Kutokana na ukweli kwamba soka ni ‘fair play’, Manara alistahili kuwa mvumilivu hata kama alichokozwa kwa namna yoyote.

Wanaopinga kwamba Manara ameonewa, wakiwamo wanachama wa Yanga na wadau mbalimbali kama vile wachambuzi wa michezo katika vyombo vya habari, wanapaswa kukubaliana na uamuzi huo ambao umetolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa, hivyo ni vyema wakasubiri kama matokeo mengine iwapo mhusika atakata rufani.

Kuna msemo kwamba “atajifunzaje asipochafuka?” Kwa mantiki hiyo kuna uwezekano mkubwa adhabu hiyo ikaleta sura mpya katika utendaji kwenye medani ya soka kwani ni imani kwamba kupitia adhabu hiyo watu watajifunza kuheshimu mamlaka zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za taasisi pamoja na nchi kwa ujumla.