Tanzania katika michezo hiyo itawakilishwa na timu za michezo ya riadha, ndondi, judo na kuogelea na kwa mara ya kwanza kutakuwa na mchezo wa kunyanyua vitu vizito kwa wenye ulemavu.
Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika michezo hiyo, lakini miaka inavyozidi kwenda mbele, matokeo yetu yamekuwa sio mazuri na katika michezo mitatu iliyopita ya Madola, wachezaji wetu wamerudi mikono mitupu.
Hadi sasa Tanzania ina jumla ya medali 21 za aina mbalimbali kutoka katika Michezo ya Jumuiya ya Madola, ambapo medali za dhahabu ni sita, fedha sita na shaba zikiwa tisa.
Ukiangalia historia, nyingi ya medali hizo Tanzania ilizotwaa zimetokana na mchezo wa riadha pamoja na ngumi. Tanzania ilianza kushiriki michezo hiyo mwaka 1966 Kingstone, Jamaica kabla ya kushiriki mwaka 1970 huko Edinburgh, ambako tulitwaa medali moja ya shaba.
Katika historia ya Tanzania kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola, kipindi kizuri zaidi kilikuwa mwaka 1974 michezo hiyo ilipofanyikia Christchurch, New Zealand ambako Filbert Bayi alivunja rekodi ya dunia na ile ya Jumuiya ya Madola.
Bayi alivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 baada ya kutumia dakika 3:32.16 na ile ya Jumuiya ya Madola ambayo hadi sasa anaishikilia ikiwa ni miaka 48 imepita tangu aitwae medali hiyo.
Mbali na Bayi, baadhi ya wanariadha wengine waliotwaa medali katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ni pamoja na Samson Ramadhani, Francis Naali, Simon Mrashani na wengine.
Timu ya Tanzania mwaka huu inakwenda Birmingham, kushiriki michezo hiyo, huku kukiwa na matumaini makubwa ya kurudi na medali baada ya miaka 12 ya kutoka kapa.
Baada ya riadha kwa muda mrefu kupeleka wakimbiaji wa mbio ndefu, mwaka huu timu ya Tanzania ina wachezaji wa mbio fupi kama mita 100, 200 na zile za kati za mita 800 na 1,500 pamoja na ndefu za uwanjani za mita 5,000 na 10,000.
Kwa upande wa mbio fupi, matumaini ni madogo ya kurudi na medali kwani wanariadha wetu hawajapata uzoefu wa kutosha katika kada hiyo, tofauti na wale wa marathoni, ambao angalau wameshiriki mbio nyingi na kufanya vizuri, mfano Simbu.
Mfano hai ni baadhi ya wanariadha wetu wa mbio fupi, walishiriki mashindano nchini Kenya, lakini walishindwa kung’ara, hivyo hata nafasi ya kufanya vizuri katika Michezo ya Jumuiya ya Madola inawezekana isiwepo.
Hivyo, sisi tunasema kwamba, maandalizi yaliyofanyika kuelekea michezo hiyo ndio yatakayotoaa taswira ya namna gani wanamichezo wetu wanaweza kurudi na medali.
Pamoja na yote tunaamini kwamba, maandalizi waliyofanya yanaweza pia kuwafanya wakarudi na medali, ingawa kazi sio ndogo na sisi kama wadau wa michezo tunawatakia kila la heri.









