Ajira za walimu ziguse uwiano  wa shule za mijini, vijijini

12Jul 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ajira za walimu ziguse uwiano  wa shule za mijini, vijijini

SERIKALI imeajiri walimu 9,800, ambao sasa wanatakiwa kuripoti kwenye vituo vipya vya kazi ili waanze kutekeleza majukumu yao ya kufunza na kufundisha watoto katika shule za msingi na sekondari.

Ajira mpya huenda zikasaidia kupunguza changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakumba walimu, wanafunzi na hata wazazi na walezi, huku chanzo chake kikidaiwa kuwa ni uhaba wa walimu. 

Miongoni mwa changamoto hizo ni baadhi ya shule kuwa na walimu wachache ambao hulazimika kufundisha vipindi vingi, huku wanafunzi nao wakikosa baadhi ya masomo kutokana na uhaba huo. 

Uhaba huo pia umekuwa ukisababisha wazazi na walezi kubebeshwa mzigo kwa kutozwa fedha za masomo ya ziada 'twisheni', kwani wakiwa shuleni, hawasomi vipindi vyote kutokana na uhaba huo. 

Hivyo, hatua ya kuajiriwa kwa walimu wapya 9,800 kunaweza angalau kupunguza baadhi ya changamoto ambazo zinasababishwa na uhaba huo, hasa shule za vijijini ambazo zina walimu wachache zaidi. 

Serikali inawataka waajiriwa hao wapya kuripoti kwa wakurugenzi wa halmashauri walizopangiwa wakiwa na kitambulisho cha taifa au namba ya utambulisho ya NIDA, cheti halisi cha kuzaliwa, ni vyema wafanye hivyo. 

Ninaamini kuwa hatua ya serikali kuajiri walimu, inalenga kupunguza changamoto ambayo imekuwapo kwenye baadhi ya shule, ikiwamo ya kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi huku walimu wakiwa wachache. 

Pamoja na hayo, ninadhani suala la uhaba wa walimu lingefaa kufanyiwa kazi kwa njia ya hii pia, ya kuwa na uwiano kati ya walimu wa shule za mijini na vijijini, badala ya upande mmoja kuwa na mrundikano wa walimu. 

Pamoja na hayo, ninadhani suala la uhaba wa walimu lingefaa kufanyiwa kazi kwa njia ya hii pia, ya kuwa na uwiano kati ya walimu wa shule za mijini na vijijini, badala ya upande mmoja kuwa na mrundikano wa walimu. 

Mfano, Desemba 2016, takwimu za Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zilieleza kuwa kulikuwa na walimu 272,264 wa shule za msingi na sekondari kutoka 153,767 mwaka 2005. 

Lakini, ikabainika kuwa shule nyingi za vijijini zina uhaba mkubwa wa walimu, tofauti za mijini ambazo walimu wamerundikana, hivyo ingefaa suala la uwiano kati ya shule za mijini na vijijini likatiliwa mkazo. 

Nakumbuka mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu, alitangaza kuwa, walimu wanaotaka kuhama kutoka mijini kwenda vijijini ruksa, na akaweka masharti kwa wanaohamishwa vijijini kwenda mjini. 

Kwamba, walimu wanaotaka kuhama kutoka vijijini kwenda mjini, lazima Tume ya Utumishi wa Walimu nchini, ihakikishe kabla ya kuwahamishwa wawe na walimu mbadala wa kule wanakotoka. 

Lengo lake lilikuwa ni kukabili uhaba wa walimu katika shule za vijijini, hivyo kwa mtazamo wangu, ninadhani pamoja na kuajiri walimu wapya, bado ipo ya kudhibiti wingi wa walimu kwenye shule za mijini. 

Kama alivyowahi kusema Waziri Ummy,  kuwa ni uhamisho ni haki ya mtumishi, lakini ni vyema akawapo mwingine wa kuziba nafasi ya anayehama, vinginevyo shule za vijijini vitaendelea kuwa na uhaba wa walimu. 

Lakini,  ingekuwa vyema kama Tume ya Utumishi wa Walimu itafanya tathmini ya kina kwa kuangalia uwiano wa walimu kwenye shule za msingi na sekondari katika mamlaka za serikali za mitaa. 

Hatua hiyo iwe ni kwa ajili ya takwimu sahihi za mahitaji halisi ya walimu na uwiano uliosawa katika halmashauri badala ya upande mmoja kuwa na mrundikano huku shule nyingine zikiwa na uhaba mkubwa wa walimu. 

Pamoja na hayo, jambo lingine ambalo ninadhani linaweza likasaidia kupunguza walimu kuhama kutoka shule za vijijini, ni kuboresha mazingira ya huko ikiwamo nyumba kuwa mahata usafiri ili wafike kazini kwa wakati. 

Kumekuwapo na malalamiko kuwa mazingira duni ya shule za vijijini ni kikwazo kwa walimu, na inawezekana yanachangia hata baadhi yao kuandika sababu za uongo, ili mradi wahamishwe kutoka katika mazingira hayo. 

Lakini, mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, katika shule za vijijini, ni vyema yakawa rafiki kwa walimu na wanafunzi, hatua ambayo ninadhani inaweza kupunguza kasi ya walimu kukimbilia shule za mijini. 

Ikumbukwe kuwa bila kuboresha mazingira ya shule za vijijini, ufundishaji na ujifunzaji unaweza kuendelea kuwa mgumu na hivyo kuwafanya wanafunzi kushuka kitaaluma au kufaulu kwa alama ndogo.