Kuanzisha nyanda za malisho tiba migogoro wakulima, wafugaji

13Jul 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kuanzisha nyanda za malisho tiba migogoro wakulima, wafugaji

MAPIGANO kati ya wakulima na wafugaji, kwenye baadhi ya maeneo ni miongoni mwa migogoro inayoibuka mara kwa mara  na licha ya kutafutiwa ufumbuzi bado inajitokeza.

Ipo mifano mingi ya migogoro hiyo ambayo imetokea miaka ya nyuma na kusababisha maafa kwa makundi hayo mawili, lakini mfano mwingine ni wa hivi karibuni katika tukio la Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wafugaji kutoka Arusha wakivamia eneo hilo.Diwani wa Masama Rundugai (CCM) wilayani humo, Aziz Simbano na wenzake wawili na mwanawe wa kiume, walinusurika kuuawa, baada ya kujeruhiwa na wafugaji waliotaka kulisha kwa nguvu mifugo mazao yake.Migogoro kama hiyo imekuwa kutokea mara kadhaa katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Pwani, Manyara, lakini baadaye ikawa imetulia baada ya serikali kuingilia kati kuitatua.Lakini kwa tukio hilo la wilayani Hai, ipo haja ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, ili kuzuia kuiona na kuibuka kama uyoga na kuhatarisha maisha ya makundi hayo mawili.Binafsi ninadhani njia mojawapo inayoweza kusaidia kupunguza migogoro hiyo, ni kutengwa kwa maeneo ya malisho (nyanda za malisho) na kuyatambua kisheria ili kuzuia uvamizi unaoweza kufanywa na watumiaji wengine wa ardhi.Iwapo watakuwa na maeneo yao yenye malisho na maji ya kutosha wakati wote, ambayo yanatambuliwa kisheria, ninadhani hawatahama ovyo na kujikuta wakigombana na wakulima kwa tuhuma za kuharibu mazao.Kwa miaka mingi, Watanzania wamekuwa wakiishi mchanganyiko kuanzia wakulima na jamii ya wafugaji, huku wafugaji wakitumia ufugaji wa asili na kuchangia katika ukuaji wa soko la nyama nchini.Lakini sasa mtindo wao wa kuhama kutafuta maji na malisho, umekuwa ukidaiwa kuchangia kuwapo kwa migogoro kati yao na wakulima ambayo wakati mwingine husababisha mapigano.Wakati mwingine mapigano hayo husababisha majeraha na hata vifo kwa makundi hayo na pia kwa mifugo. Hivyo ingekuwa vyema iwapo utashi wa kisiasa utachukua mkondo wake ili kuwa ufumbuzi wa kudumu.Ninadhani umefika wakati sasa kutumia utashi wa kisiasa kumaliza tofauti za makundi hayo, ili yaishi kwa amani kutokana na ukweli kwamba yote yanategemeana kwa namna moja au nyingine.Utashi wa kisiasa kwa maana ya viongozi wa kuchaguliwa wenye ushawishi kuingilia kati ili kumaliza tofauti zao, kwani bila utashi wa kisiasa, ninaamini kwamba migogoro na mapigano, vinaweza kuendelea kuibuka.Hatua hizo zinaweza kusaidia kuondoa uhasama kati ya makundi hayo na kuyafanya kuwa na ushirikiano wa kudumu na hata kuendelea na uzalishaji mali ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.Ikumbukwe kuwa, mfugaji anaweza kununua mazao kutoka kwa mkulima, na pia mkulima anaweza kununua kitoweo kutoka kwa mfugaji, hivyo suala la ushirikiano wa makundi hayo ni wa muhimu kuliko utengano.Kimsingi, wote ni Watanzania, wana haki ya kutumia ardhi kulingana na taratibu zilizowekwa, ndiyo maana ninashauri kutafutwa kwa njia ambayo inaweza kumaliza uhasama huo wa miaka nenda miaka rudi.Siamini katika kuendeleza migogoro, bali njia sahihi za kuimaliza, kwani imekuwa ikisababisha upotevu wa rasilimali kwa raia, jamii na serikali kwa ujumla, uharibifu wa mali, uhai wa raia na mifugo.Hivyo, ninaona kuna haja kushauri mamlaka husika kila iwezekavyo kuhamasisha suala la amani na ushirikiano kwenye jamii vinahamasishwa, ili kila kundi liendeshe shughuli zake bila chokochoko.