Kwa wanaokwenda Mwanza, Musoma, Shinyanga, Bukoba, Kahama na kwingine kwa mwelekeo huo wanapotoka Dar es Salaam, kituo cha kwanza kwa ajili ya huduma za kijamii ni mjini Morogoro.
Kama hilo haitoshi, wanaokwenda mikoa ya jirani kama Dodoma hasa kwa magari yasiyo ya alfajiri, wanasimama kupata chakula cha mchana au cha jioni kwenye moja ya hoteli za mkoa huo kutegemeana na makubaliano baina ya dereva na wamiliki wa hoteli.
Kwa ujumla, unaposafiri kwenda mikoa mingine hususan ya Kanda ya Kaskazini na Kusini huduma za vyakula ni za kuridhisha sana kuanzia usafi wa eneo husika na vyakula, lakini siyo kwa njia ya Morogoro.
Hoteli zote ambazo mabasi yanasimama ili abiria 'wachimbe dawa', wapate huduma ya chakula na mapumziko kwa ujumla siyo za kuridhisha kabisa, hali inayozua maswali mengi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwamba huwa haioni hayo yote?
Kuanzia huduma ya vyoo ni kuchafu na vibovu kiasi cha kuziweka hatarini afya za wasafiri kwa kuwa hakuna anayefuatilia, mwenye biashara huamua anavyotaka kwa kuwa hakuna ukaguzi.
Vyakula vinauzwa bei ya juu, vinywaji vinauzwa mara mbili hadi tatu ya bei na wakati mwingine abiria ananunua kwa kuwa anahitaji na ndilo eneo pekee alilofikishwa na dereva wa basi husika.
Ninatambua kwenye kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuna Ofisa Afya ambaye moja ya majukumu yake ni kufuatilia usafi wa maeneo yote ya biashara, hasa hoteli na migahawa inayotumiwa na watu wengi, kisha kuchukua hatua, ikiwamo kufunga biashara husika kwa anayebainika kutokidhi vigezo.
Migahawa na hoteli ninayoizungumzia mjini Morogoro iko kilomita chache kutoka iliko Manispaa ya Morogoro. Swali ninalojiuliza wanafanya ukaguzi hadi kwenye vyoo, wanaona vingine havina milango na ni chakavu kupita kiasi au wanaacha bora liende na kukusanya kodi pekee?
Ni muhimu sana Manispaa ya Morogoro ikajali afya za wananchi, kama ambavyo maeneo hayo yanawaingizia fedha kama chanzo cha mapato, wanao wajibu wa msingi kufuatilia huduma zinazotolewa humo kama zinaridhisha.
Ni lazima hatua zichukuliwe ili mazingira ya hoteli na migahawa iboreshwe au kujengwa upya. Kama mtu anataka kuwekeza kwenye huduma hizo, afanye uwekezaji wa kuridhisha na kukidhi vigezo vyote vya afya kuliko wananchi kuingizwa kwenye matatizo.
Kama maeneo haya wanatoza fedha zaidi ya bei halisi ya bidhaa husika, kwanini wanashindwa kuboresha maeneo yakawa mazuri na ya kuridhisha kuanzia huduma za vyoo, chakula na vinywaji?
Maana yake ni kwamba hakuna ufuatiliaji wa serikali, ndiyo maana kimebaki kuwa chanzo cha mapato pekee pasi na ufuatiliaji wa kama huduma zinazotolewa zinakidhi matakwa ya kiafya kwa mujibu wa sheria.
Wasafiri ni watoto, vijana, umri wa kati na wazee ambao ni mchanganyiko wa wanaume na wanawake, wote wanatumia vyoo visivyoridhisha na ambao wako hatarini zaidi kupata maradhi ya njia ya haja ndogo ni wanawake na watoto.
Lazima hatua zichukuliwe tuone mabadiliko kuliko hali kuachwa ilivyo, serikali isiishie kukusanya mapato pekee, bali kujiridhisha na kusimamia usafi wa maeneo husika. Kama inashindikana wachukue hatua kwa mujibu wa sheria.
Hoteli nyingi za Kanda ya Kaskazini mteja anaponunua chochote anapewa stakabadhi ya EFD, lakini kwa hizi za Manispaa ya Morogoro, kwa uzoefu wangu wa kusafiri njia hiyo sijawahi kupewa stakabidhi, maana yake hata Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapoteza mamilioni ya shilingi ambayo yangeingia kwenye kapu la Taifa na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kama hoteli za Kamda ya Kaskazini imewezekana kuweka mashine za EFD, basi hata Morogoro na mikoa mingine ambayo mamia ya wasafiri hutumia huduma, kuwe stakabadhi hizo muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mungu ibariki Tanzania



.jpg?itok=nfwjwDzv)








