Kalolanya anavyotuambia benchi si adui

27Jun 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kalolanya anavyotuambia benchi si adui

UKIMWONA kwa sasa akiwa golini na jinsi anavyofanya kazi yake kwa ustadi unaweza ukadhani kwamba Simba na ina golikipa mpya.

Kwa mechi kadhaa sasa ambazo Simba imeonekana kuukosa ubingwa wa Tanzania Bara kuna golikipa mwingine ambaye anakaa golini.

Anadaka michomo kwa ustadi na 'saves' za maana kiasi cha kuwakosha mashabiki wengi waliopo uwanjani na wale ambao wanamtazama kwenye televisheni.

Kuna watu wameshaanza kusema kuwa alikuwa wapi huyu, si bora angekaa hata mechi zingine za huko nyuma?

Huyu ni Beno Kakolanya. Kipa namba mbili wa Simba ambaye wanachama na mashabiki wengi wa timu hiyo walikuwa hawamwamini. Asipokuwapo Aishi Manula roho zao zikakaa juu kama mkungu wa ndizi.

Hii ilisababisha msimu huu kumsajili Jeremiah Kisubi, ambaye dirisha dogo akapelekwa Mtibwa Sugar kwa mkopo.

Wengi wanashangaa kiwango hiki anachoonyesha sasa Beno amekipata wapi wakati kila msimu yeye ni mtu wa benchi?

Kiwango chake cha sasa kimesababisha mashabiki wa Simba kudai kuwa hata kwenye mechi za Ligi Kuu au Ligi ya Mabingwa kama Manula akiumia hawana wasiwasi tena, wanajua wana mtu golini.

Kwa siku za karibuni tangu mechi ya fainali ya Kombe la FA, Kakolanya amefanya kazi kubwa ambayo si mashabiki wa Simba tu, bali hata wa soka kwa ujumla wamemkubali.

Na sidhani kwa misimu ya hivi karibuni inaweza kwenda sokoni kutafuta makipa, badala yake itakuwa inalea makipa vijana ambao watakuja kuwa namba tatu.

Mashabiki wengi wa soka wanadhani kuwa mchezaji kucheza mechi nyingi ndiyo dawa ya kulinda kipaji chake, na kama hapati muda mrefu wa kucheza, kipaji kinadumaa au kushuka.

Hiyo tumeoana mara nyingi wachezaji ambao wanakaa benchi hasa wa Kitanzania, viwango navyo vinakuwa hivyo hivyo kwa kibenchi.

Hapa Bongo utaona kabisa hata uwanjani tofauti na mchezaji wa kikosi cha kwanza na yule anayetokea benchi.

Inaonekana ni kama anayeingia anakwenda kutimiza idadi ya wachezaji 11 kwa sababu yule tegemeo amechoka, au hayuko vizuri siku hiyo.

Kakolanya hakupata nafasi sana ya kucheza ni kutokana na uwepo wa Manula, ambaye amekuwa mlinda mlango namba moja wa Simba hakuna asiyefahamu uwezo wa Manula.

Pamoja na kwamba amekaa kwa muda mrefu benchi, lakini nafasi chache alizopata za kucheza, anachokifanya ni kinyume na matarajio ya watu wengi, Wengi walitegemea kumuona Beno akifanya makosa ya mara kwa mara kwa sababu ya kutokaa golini kwa kipindi kirefu, si kwenye Ligi ya Mabingwa, Shirikisho, Ligi Kuu au FA Cup.

Beno anatoa somo kubwa sana anatuambia kwa vitendo kwamba unapopatiwa nafasi fanya watu wasiwaze kuhusu yule uliyechukua nafasi yake, badala yake wafikirie kuhusu wewe.

Mechi zote alizocheza amesimama golini vyema, tena kwa kujaribiwa na tumeona 'saves' zake za maana pamoja 'clean sheets. Kifupi watoto wa mjini wanasema, amefanya kweli.

Inaonyesha kabisa kuwa pamoja na kwamba Manula alikuwa anacheza mechi nyingi, lakini Kakolanya hakukata tamaa, au kuwa na kinyongo, au kulazimisha kuondoka ili akapate nafasi ya kucheza kwenye timu zingine, badala yake alikomaa na kupigania namba.

Japo bado ukweli ni kwamba Manula ataendea kuwa namba moja, lakini naye itaanza kumfikirisha na kujituma zaidi, kwani uzembe wowote ule au kutokuwa makini, kunaweza kumfanya kukaa benchi na Kakolanya kuchukua nafasi yake.

Bahati nzuri ni kwamba tayari mashabiki wameshamuona jinsi alivyopandisha kiwango chake, hivyo hakuna yoyote atakayepiga kelele.

Hili liwe somo sasa kwa wachezaji wengine kuwa kukaa benchi siyo kama hujui, au kukufanya ubweteke, usijitume mazoezini, la hasha.

Unatakiwe upambanie namba, siyo kujihisi mnyonge na kutaka kuondoka ili kupata sehemu rahisi ya kwenda kucheza. Namba siku zote haina mwenyewe, atakayecheza vema ndiye atakayecheza.

Mchezaji yoyote anayetokea benchini atakiwa kufanya sana mazoezi na kujua udhaifu yake unaosababisha kutokuwepo kikosi cha kwanza, akaufayia kazi.

Inatakiwa dakika chache zile zile hata kama ni tano utakazopewa, unatakiwa kuzifanyia kazi ili si kocha wala benchi la ufundi tu, bali hata mashabiki wajiulize ni kwa nini unakaa nje.

Haipendezi kwa mchezaji anayetokea benchini, hata mashabiki wakubali kuwa hautakiwi kuanza.

Wakati tunaishi kwenye mawazo ambayo benchi ni adui mkubwa wa viwango vya wachezaji, Beno ameamua kwenda kinyume na sisi na ametushinda. Hivi mmemwelewa Beno?

Atatuambia benchi si adui wa wachezaji kama watajitambua. Benchi litaendelea kuwa si salama na adui wa wachezaji wasiojitambua, kujituma, wakata tamaa na walioridhika kukaa kwenye mabo hiyo ndefu.