Tusimwangushe Rais miradi ya maji

08Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tusimwangushe Rais miradi ya maji

JUZI Rais Samia Suluhu Hassan, alishuhudia utiaji saini mikataba ya miradi ya maji kwa ajili ya miji 28 ya Tanzania Bara itakayogharimu Shilingi trilioni 1.7.

Hii ni hatua muhimu kwa nchi yetu ambayo katika baadhi ya maeneo yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa majisafi na salama kwa wananchi wake.

Utiaji saini huo ulifanyika jijini Dodoma na Rais Samia alitoa angalizo kwa fedha hizo kutumika vizuri kwa kuwa ni mkopo utakaolipwa na Watanzania wote.

Juhudi za Rais Samia kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma muhimu zinaonekana na Watanzania wana kila sababu ya kumuunga mkono kwa kutomuangusha inapokuja kwenye suala la utekelezaji.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa kwa ushirikiano wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), mabilioni ya watu duniani wanaendelea kutaabika kutokana na kukosa huduma bora za maji na masuala ya usafi.

Hivyo, suala la upatikanaji majisafi na salama linahusu watu wote kuanzia mijini hadi vijijini na mkopo huo ilioupata Tanzania katika kutekeleza miradi mipya ya maji ni muhimu katika kuwaondoa Watanzania kwenye ukosefu wa huduma hiyo na hatimaye waweze kunufaika nayo.

Wakati wa utiaji saini Rais Samia, aliwatahadharisha makandarasi kutozidisha faida kwa lengo la kuiumiza serikali na kupata hasara.

Pia, ni vizuri kuzingatia kuwa fedha hizo ni mkopo na kila Mtanzania ataulipa, hivyo hasara itabebwa na wote wakiwamo hao wakandarasi watakaopewa kazi hiyo kwa utekelezaji.

Lengo la serikali ni kuona majisafi na salama yanapatikana kwa asilimia 85 vijijini na baadhi ya vyanzo vinavyotegemewa katika miradi hiyo ni Ziwa Victoria.

Waziri wa Maji, Juma Aweso, amemhakikishia Rais kusimamia miradi hiyo na kukamilika kama inavyotarajiwa, ili kuwanusuru wananchi hasa kinamama na athari zinazotokana na uhaba wa maji.

Baadhi ya miji itakayonufaika katika mradi huo imetajiwa kuwa ni Handeni, Korogwe, Pangani, Kilwa Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Chunya, Rujewa, Wanging’ombe, Makambako, Njombe, Kiomboi, Singida, Manyoni, Chemba na Chamwino.

Miji mingine ni Kasulu, Mpanga, Sikonge, Urambo, Kaliua, Kayanga, Geita, Chato, Mafinga, Newala, Tandahimba, Nanyamba, Rorya na Songea.

Inaelezwa kuwa ndani ya mwaka mmoja miradi ya maji katika Wizara ya Maji imetekelezwa kwa asilimia 90, huku bajeti ya maji kwa mwaka huu wa fedha ikiwa tayari imeshapitishwa.

Ripoti ya UN ya mpango wa ufuatiliaji wa “hatua kuhusu maji ya kunywa na masuala ya usafi :2000-2017, ikilenga kutokuwepo usawa, imebaini kwamba wakati kuna hatua kubwa zilizopigwa katika kufikia fursa ya msingi ya maji kwa wote, usafi na huduma za majisafi, bado kuna pengo kubwa katika ubora wa huduma zinazotolewa katika masuala hayo.

Umuhimu wa huduma ya maji kwa binadamu ni mkubwa na maji ni uhai, bila huduma hiyo hakuna kitakachoendelea.

Kama alivyotahadharisha Rais Samia kuhusu usimamizi wa miradi hiyo ya maji, ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha hakuna kitakachoharibika ni kwa faida ya wote bila kujali kabila, dini, rangi, mtoto, mzee, maskini au tajiri.

Pamoja tukijitoa kulinda na kusimamia miradi hiyo wananchi watakombolewa na adha ya ukosefu wa huduma hiyo muhimu na kufurahia maisha.