Mabadiliko tabia nchi tishio, tutunze mazingira

07Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mabadiliko tabia nchi tishio, tutunze mazingira

KILA Juni 5, ni maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo inalenga kuwakumbusha wanadamu umuhimu wa kutunza mazingira, kwa ajili ya kuondokana na uharibifu hatari kwao na viumbe wengine ambao wanategemea ikolojia kuishi.

Kwa sasa kasi ya uharibifu wa mazingira ni kubwa duniani na inachangiwa na shughuli za kibinadamu kama za viwanda, huku nchi zinazoongoza kwa uharibifu ni Marekani, China na Ulaya huku Afrika kwa ujumla wake ikichangia asilimia nne ya hewa ukaa.

Mkutano wa COP26 (Conference of Parties), ulijiwekea malengo ya kupunguza hewa ukaa kwa zaidi ya nusu ili kushusha joto kwa nyuzi joto 1.5, huku kila nchi ikitakiwa kuwasilisha mpango mkakati wake wa hadi 2030, na hadi sasa nchi 151 zimewasilisha, lakini nchi kubwa zinazochangia hewa ukaa kwa wingi hazijawasilisha.

Mathalani, Tanzania imejiwekea malengo ya kupunguza hewa ukaa kwa asilimia 30 hadi 35 ifikapo 2030, kwa kuwa na mipango kwenye sekta zote muhimu, hasa katika kulifikia lengo la kuondoa kabisa hewa ukaa ifikapo 2050.

Umoja wa Mataifa (UN), katika hesabu zao za makadirio ya mipango iliyopo na hatua zinazochukuliwa na nchi husika, inaona dunia itaweza kupunguza joto kwa nyuzi joto 2.5 ifikapo 2100.

Moja ya mikakati iliyopo duniani katika kupunguza uharibifu wa mazingira ni kuondoa matumizi ya nishati za gesi, mafuta na makaa ya mawe, kwa kuwekeza nguvu kwenye nishati jadidifu ambazo ni upepo, jua, upepo na mawimbi ya bahari na tungamotaka.

Tanzania ni moja ya nchi yenye rasilimali nyingi ya madini ya kimkakati ambayo zipo aina 17, ambazo zinahitajika sana duniani hasa katika kuzalisha nishati jadidifu, huku nchi zilizoendelea zikiwekea mkakati wa kuwa na mwongozo wa madini hayo.

Kwa ngazi ya nchi tunaweza kuweka mikakati mzuri ya kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi, lakini mabadiliko ya tabia nchi hayabagui kwa kuwa uharibifu unaweza kufanyika Marekani na madhara ya kasambaa kote, licha ya kwamba Afrika inachangia kwa kiasi kidogo sana hewa ukaa, lakini ndiyo inayoathirika.

Kwa sasa tunaona mvua hazinyeshi kwa wakati, ukame wa muda mrefu na hivi karibuni tuliona mamia ya mifugo ilikufa wilaya za Loliondo, Manyara na Simanjiro, lakini maji yalipungua kwa kiasi kikubwa kiasi cha kuwa na mgawo wa maji na umeme, yote ni athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Hali ya upatikanaji wa chakula nao umeathiriwa kwa kiasi kikubwa, hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilishauri wakulima wengi kulima mazao yanayohimili ukame na kuacha mazoea ya kulima mahindi, kwa kuwa hali ya ukame imezidi kuongezeka.

Kwa sasa kina cha maji Ziwa Tanganyika, Bahari ya Hindi na kwingine kinaongezeka kwa kasi, huku wananchi wa Pangani, Mafia na Micheweni Pemba wanaanza kumegwa na maji kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa sasa shughuli za kilimo zimeathiriwa, mathalani kule Micheweni Pemba maji ya chumvi yamesababisha wakulima hawawezi kulima tena, huku wavuvi wakishindwa kuvua na maeneo ya mialo na huduma za kijamii yakimezwa na maji.

Suala la mabadiliko ya tabia nchi siyo jambo dogo linahitaji ushiriki wa dunia kulikabili, kama nchi tunaweza kuchukua hatua kwa uwezo wetu, lakini kuna nyingine ziko nje ya uwezo wetu.

Tuendelee kuhamasisha upandaji miti kwenye maeneo mengi, kuhamasisha wanakijiji kutunza misitu ili kuzalisha kaboni ambayo inauzwa duniani, lakini kutumia vyema fedha za mazingira zinazotolewa duniani zilionyesha mabadiliko kwenye maisha ya watu ili watunze mazingira.

Ni muhimu kuelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira, kushiriki moja kwa moja kuweka mazingira safi, mamlaka za serikali kusimamia sheria ipasavyo kudhibiti viwanda na kampuni zinazotiririsha kemikali ambazo ni hatari kwa wananchi.

Mathalani, ukienda maeneo ya mabondeni jijini Dar es Salaam, kuna kilimo cha mboga kinafanyika, lakini maji yanayotumika ni machafu hali ambayo ni hatari kwa afya za walaji, ni lazima kuwalinda wananchi dhidi ya maradhi mengine ambayo ni mzigo kwa taifa.

Pia ni muhimu nchi ikajipanga na kutekeleza vyema yale iliyoahidi kwenye COP26 ili tutakapoonda kwenda COP27 tuwe tumejipanga vyema kutekeleza majukumu yote kimkakati kwa manufaa ya nchi, hasa kwa kupata fedha za ufadhili za mazingira zisaidie maendeleo ya nchi yetu.