Hili la utapeli ‘kamari mtandao’ liandaliwe vita vipya kulimaliza

10Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hili la utapeli ‘kamari mtandao’ liandaliwe vita vipya kulimaliza

KUNA jambo linalotoa maswali mengi ya kijamii sasa. Mambo yote yana majibu kwa umma, iwe kisheria au hata kutumia kanuni kadhaa za kiserikali, lakini kasoro zake hazikomi.

Swali la utapeli kwa michezo ya kubahatisha kupitia mifumo ya mitandao na hasa simu za mkononi linaendelea kuumiza watu. Siku chache zilizopita, kundi kubwa la kijamii limeumizwa kupitia michezo ya kubahatisha yenye kanuni zake, ikielezwa mtu anawekeza kiasi fulani cha fedha kutarajia faida na ndipo anaangukia kidevu.

Tahadhari nyingi zimeshatolewa na serikali kuwataka watu wawe makini na haya, lakini kama vile kumpigia mbuzi gitaa.
Maana aina hiyo mpya ya utapeli mara tu baada ya kujitokeza kwenye mtandao, huku mmiliki wake halisi haeleweki sawa, wakakurupukia kuamini wanawekeza fedha kwenye kamari hiyo wavune, lakini wanaangukia kuvunwa na matapeli.

Ingawa kundi kubwa linaficha kiasi cha dhuluma, imebainika kiwango cha dhuluma kwa wengi ni kati ya Sh. 20,000 na Sh. milioni mbili. Ni aina ya dhuluma inayofanana sana na kilichotokea huko nyuma katika mchezo wa kubahatisha usio rasmi, kwa kivuli cha kampuni ya DECI. Wengi walitaharuki na kukimbilia kujiunga kucheza kamali hiyo yenye matarajio wangevuna pesa, ila wakaishia kuvunwa kiasi kikubwa cha pesa.

Nakumbuka baada ya mkasa wa watu kutapeliwa kupitia kamali ya DECI ambayo taharuki yake ilituma salamu kwa wengi, serikali nayo ikichukua hatua za kuimarisha kanuni na sheria husika, bado inaonekana kuna shida ambayo inaacha maswali, shida iko wapi, uelewa au kiburi cha wanaojitosa kucheza katika mazingira hayo kama ya sasa.

Msingi wa michezo ya kubahatisha nchini ina sheria yake mamlaka maalum, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha inayosajili na kusimamia michezo, pia kusimama vigezo na haki zote za kisheria kwa wachezaji na wachezeshaji, hata serikali katika nafasi yake ikiwamo kodi. Hapo ndipo inazaa swali, shida imekaa wapi?

Baada ya mkasa ambao hadi mwanzoni mwa wiki hii, kumeshuhudiwa vilio vya kutapeliwa, Nipashe ilipochukua hatua ya kiudadisi undani, si Benki Kuu (BoT) au wizara husika, zote zimekana kuutambua mchezo huo na kuuacha kando kuwa utapeli. Hapo napo kunahalalisha kwamba wanaocheza kudhulumiwa tena na ‘mtu asiyejulikana.’

Hatua hiyo ilijidhihirisha zaidi, pale wachezaji hasa waliojihusisha na mtandao huo wakiwekeza fedha zao zisizorudi, wakaanza kukatishwa tamaa mtandaoni, wakipewa kauli zenye ishara za kutapeliwa kwao.

Ni aina ya ujumbe wa kimtandao ambao wachezaji wake awali wanasema ilikuwa tofauti, kwani walipewa kauli za hamasa kibiashara. Ghafla zikatoweka, baada tu ya kubainika na kuwapo kauli ya umma kwamba kunafanyika utapeli katika mtandao huo, ikisambaa hadi katika vyombo vya habari.

Kwa majumuisho ya yote inaonekana kuna shida bado katika haki kupitia ndani ya mifumo ya mitandao ya jamii. Kuna suala la uelewa kuhusu mitandao, sheria zake na mantiki ya kielimu kwa jumla, huku kukiwapo wanaotaka kupata kipato kwa njia za mkato.

Tunajua serikali imefanya juhudi za makusudi katika kukabili madhila ya yanayojificha katika mifumo ya mitandao ya jamii, pia michezo ya kubahatisha kwa sheria, miongozo na vyombo maalum vinavyosimamia.

Ila kwa hili tunaloshuhudia tena, bado kuna mambo makuu mawili yanayostahili serikali kuchukuwa hatua zaidi. Kwanza, elimu zaidi kwa umma inatakiwa maana kuna kiashiria cha upungufu katika uelewa, pia wahusika wa utapeli wasakwe kwa nguvu zote kwa kutumia mamlaka za usalama wa dola, maana kinachojengwa si sahihi na tusishangae, DECI nyingine ikajirudia kama hapatakuwapo udhibiti sahihi.