TFF anzisheni Ligi ya soka vyuo vikuu

11Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TFF anzisheni Ligi ya soka vyuo vikuu

TIMU ya Taifa, Taifa Stars, haifanyi vizuri sana kwenye mashindano ya kimataifa na sababu zinaweza kutajwa nyingi sana, lakini ukweli ni kwamba, nchi haina wachezaji bora wanaoweza kuipa mafanikio timu hiyo.

Kwa miaka mingi Stars imekuwa haifanyi vizuri katika mashindano ya timu ya Taifa. Hii inatokana na kukosa Wachezaji wenye uwezo wa kupambana na kuleta matokeo chanya.

Pamoja na klabu kuwekeza kwa wachezaji wao na pia kuanzisha timu za vijana chini ya umri wa miaka 17, lakini mwishowe wengi wao hupotelea sehemu nyingine hasa mashuleni ambako ndio wanakoona wanaweza kupata maisha mazuri baada ya masomo yao.

Sisi tukiwa kama wadau wakuu wa mpira wa miguu Tanzania, tunaona kwamba, huu ni wakati sasa kwa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) kuanzisha Ligi ya Wanavyuo.

Ligi hiyo inakuwa ikihusisha vyuo mbalimbali vilivyopo nchini ili kuweza kuibua vipaji vitakavyosaidia timu ya taifa.

Kunaweza kusiwe na matokeo ya haraka katika kupata vipaji, lakini tunaamini mbeleni kunaweza kuleta matokeo chanya.

Huu ni ushauri tukiwa kama wadau wa soka, kwani kwa uwepo wa Ligi ya vyuo vikuu tunaamini kabisa tutaweza kutoa wachezaji bora na wa kiwango cha juu kabisa.

Hiyo inatakiwa kufanyika kuanzia vyuo vikuu, vyuo vya kati na vyuo vingine ili wanafunzi waweze kuonesha uwezo wao na baadae kuisaidia timu ya Taifa. Hii pia itawasaidia wanafunzi kujipatia vipato vyao kupitia mishahara na kujikimu kwa namna mbalimbali.

Chuo ambacho kitawezesha timu yake kushinda ligi hiyo, basi TFF waweke utaratibu kwa kushirikiana na bodi ya Ligi kuhakikisha kuwa timu itakayoongoza Ligi iweze kuingia moja kwa moja kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kama ilivyo kwa Ligi Daraja la Pili na la kwanza, uwepo wa Ligi ya vyuo Tanzaia kunaweza kuwa msaada mkubwa kwa soka letu hapa nchini.

Kwa muda mrefu sasa, michezo vyuoni imekuwa ikisahaulika na Wanafunzi wamekuwa wakicheza kama sehemu ya kujifurahisha tu bila kuwa na malengo maalumu au mipango madhubuti ya michezo wanayoshiriki. Na hii tunaona kwamba, inachangiwa sana na kukosa sapoti kutoka kwa mamlaka zinazosimamia michezo nchini.

Ni ukweli usiopingika kuwa vyuo vinabeba vijana wengi wenye vipaji vikubwa katika michezo, hasa mpira wa miguu. Kama TFF itaweza kutumia kundi kubwa kama hili la vijana katika kupata na kuibua vipaji, tunaamini wanaweza kuwa msaada mkubwa zaidi nchini.

Tunaona kwamba, TFF isaidie kusimamia Ligi hiyo ili kutafuta wadhamini na wawekezaji katika timu hizi ili ziweze kujiendesha.

Ni wakati sasa wa TFF kuangalia hili kundi muhimu nchini na kuwasadia hawa vijana ili waweze kuonesha uwezo wao wanapokuwa vyuoni na mara baada ya kumaliza chuo waweze kujiunga na timu mbalimbali nje na ndani ya nchi.

Kwani hii pia itakuwa sehemu ya kupunguza tatizo la ajira nchini, kwani wachezaji wa vyuo ambao watakuwa na mafanikio makubwa zaidi wanaweza kupata ajira kupitia michezo na kujitengenezea fedha nyingi.

Ni matumaini yetu kuwa TFF, Bodi ya Ligi, Wizara inayohusika na vyuo hapa nchini vitakaa chini na kukubaliana kuanza kwa mchakato huo.

Tunaamini baada ya miaka mitatu na kuendelea, tunaweza tukajikuta tuna wachezaji wengi sana wenye vipaji vya hali ya juu hapa nchini ambao watakuwa msaada mkubwa kwa nchi.

Wakati ndio huu, tunaweza kuamua sasa.