Lala salama Ligi Kuu, TFF ikisinzia tutavurunda CAF

04Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Lala salama Ligi Kuu, TFF ikisinzia tutavurunda CAF

LIGI Kuu Bara imeingia raundi ya 19, ambapo mzunguko huu utakapokamilika kila timu itakuwa imebakiza mechi 11 kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa 2012/22 ambao unashirikisha timu 16, mbili za mkiani zikishuka daraja moja kwa moja kwenda kucheza Ligi ya Championship msimu ujao.

Lakini, timu mbili zitakazoshika nafasi ya 13 na 14, zitacheza mechi ya mchujo dhidi ya timu mbili zitakazoshika nafasi ya tatu na ya nne kwenye Ligi ya Championship kuwania nafasi mbili za kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Hadi ligi hiyo inarejea juzi baada ya kumalizika kwa Kalenda ya Fifa, Yanga bado ndiyo ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 48, huku ikifuatiwa na Simba yenye pointi 37 katika nafasi ya pili na hali ikiwa mbaya zaidi kwa Tanzania Prisons inayoburuza mkia ikiwa na pointi 13, moja nyuma ya Mbeya Kwanza iliyopo nafasi ya 15.

Kwa ujumla msimu huu umekuwa na ushindani mkubwa zaidi ndani ya muongo mmoja sasa, hivyo katika raundi kama hii Shirikisho la Soka nchini (TFF), likishirikiana na Bodi ya Ligi (TPLB), kwa kuvishirikisha vyombo vya usalama na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), hawana budi kuzidi kuimulika ligi hiyo kwa umakini zaidi ili kuepuka kupata bingwa asiyestahili.

Tunatambua mbali ya timu zilizopo katika mbio ya ubingwa, lakini pia zipo zinazohaha kujinasua katika mstari wa kushuka daraja, kucheza mechi za mchujo na zinazotaka kumaliza nafasi nne za juu ili kunufaika na bonasi kubwa kutoka kwa wadhamini, hivyo ni kipindi ambacho umakini zaidi unahitajika kwa kuanza kuwamulika viongozi wa klabu, wachezaji hadi waamuzi.

Ikumbukwe kwa mujibu wa mkataba ambao TFF iliingia na Kampuni ya Azam Media Limited Mei mwaka jana kwa upande wa haki za matangazo ya televisheni ambao una thamani ya Sh. bilioni 225.6 kwa kipindi cha miaka 10, kuna bonasi kubwa mwishoni mwa msimu kutegemea na nafasi timu itakayomaliza kuanzia bingwa hadi itakayoburuza mkia.

Kwa bingwa, mbali na kombe na zawadi kutoka kwa Mdhamini Mkuu, Benki ya NBC, Azam Media Limited itatoa bonasi ya Sh. milioni 500, mshindi wa pili milioni 250, watatu milioni 225, wa nne milioni 200 na zitakwenda zikipungua hadi mwisho na zitakazocheza mechi ya mtoano zikilamba milioni 20 kila moja.

Hivyo, raundi hii kunahitajika umakini mkubwa kwani timu zote zinauhitaji mkubwa wa kumaliza nafasi za juu ili kupata bonasi kubwa, lakini fedha zinazopata zinaweza kutumika vibaya katika kutafuta matokeo nje ya uwanja kwa kutembeza rushwa ili kupanga matokeo.

Kwa kuwa bingwa huiwakilisha nchini kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tunachotaka kukiona sisi ni ligi hiyo ikimalizika kwa kupatikana bingwa aliyestahili ili mwakani aweze kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika michuano hiyo ya kimataifa ya kwanza kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Lakini kama Simba ambayo jana usiku ilikuwa ikicheza dhidi ya US Gendarmerie ya Niger kwenye mechi ya hatua mwisho ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikihitaji kushinda ili kutinga robo fainali, endapo imefanikiwa kusonga mbele kuna uwezekano mkubwa wa kuingiza timu nne kwenye michuano ijayo ya kimataifa; mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho.

Kwa mantiki hiyo, ni wazi timu tatu zitakazomaliza nafasi ya juu, zinaweza kupata tiketi ya kuiwakilisha nchini kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, jambo ambalo tunataka kuona umakini mkubwa unafanyika katika ligi hiyo ili kutoa wawakilishi waliostahili na si wakiujanjaujanja.

Lengo letu ni kuona kama Tanzania itafanikiwa kuingiza timu nne kwenye michuano hiyo ya CAF msimu ujao, basi zote zifike hatua ya makundi robo fainali na kuendelea, na si kuishia raundi ya awali kama ambavyo imetokea msimu huu kwenye michuano hiyo inayoendelea Afrika.

Aidha, tunataka kuona Tanzania ikiwa nchi ambayo kila msimu inaingiza timu nne kwenye michuano hiyo ya CAF, lakini hilo litawezekana tu kama wawakilishi watakaopatikana angalau watakuwa wanajitutumua hatua ya makundi, robo fainali na kuendelea, kwa kuwa katika hatua hizo ndiyo nchi husika hupata pointi nyingi, hivyo bila TFFna TPBL kumulika kwa umakini mechi hizi 11 zilizosalia itakuwa ndoto hilo kutokea.