US Gendarmarie kutoka Niger.
Mechi hiyo ni ya mwisho katika hatua ya makundi, Simba ilipangwa katika Kundi D pamoja na timu za RS Berkane ya Morocco na Asec Mimosas kutoka Ivory Coast.
Bila kusubiri matokeo mengine, Simba iliyoanza hatua ya makundi kwa ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Asec Mimosas, kesho inahitaji ushindi na kuendeleza rekodi yake safi ya kuvuna pointi zote inapocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Benjamin.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanatakiwa kuingia katika mchezo huo kwa nidhamu na tahadhari ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Tunawakumbusha wachezaji wa Simba kuendelea kupambana kwa kucheza katika kiwango bora kama walivyofanya kwenye mechi michezo mingine iliyopita na hatimaye watapata kile ambacho wanakihitaji.
Inafahamika wazi kusonga mbele kwa Simba katika michuano hiyo, si tu kutainufaisha klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini, lakini itaendelea kuipa Tanzania nafasi ya kutoa timu nne kwenye mashindano ya CAF katika msimu ujao.
Simba haitakiwi kuingia uwanjani ikiwadharau US Gendarmerie, eti kwa sababu inaburuza mkia kwenye kundi hilo, lakini ielewe pia wapinzani wao wanahitaji kulinda heshima na vile vile kuweka rekodi ya kuwachapa Wekundu wa Msimbazi nyumbani kwao.
Tunawakumbusha nyota wa Simba kushuka uwanjani wakifahamu wanapeperusha bendera ya Tanzania, hivyo wanatakiwa kujituma kwa kiwango cha juu kwa sababu pia watakuwa wanajitengenezea maisha yao kwa kuwavutia mawakala na makocha wa klabu nyingine za mataifa ya Ulaya ili kuwasajili.
Huu ni wakati ambao mashabiki, wanachama na wadau wa soka nchini kuweka tofauti zao pembeni na kuiombea dua njema Simba ambayo kwenye hatua hiyo ya makundi, imepakia peke kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki.
Simba inatakiwa ifahamu si Watanzania tu wanawaangalia, mechi ya kesho itafuatiliwa na wadau wengine ambao kwa namna moja au nyingine wanaweza kuwavutia kuja kuwekeza kwenye soka la hapa nchini.
Katika kuhakikisha mambo mazuri yanapatikana, huu ni wakati wa mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwashangilia wachezaji kuanzia dakika ya kwanza hadi pale filimbi ya mwisho itakapolia.
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa kuanzia saa 4:00 usiku, katika kuhakikisha usalama wa mashabiki na mali zao, Jeshi la Polisi limeahidi kutoa ulinzi wa kiwango cha juu ndani na maeneo ya jirani ya uwanja huo ili kila mtazamaji atakayefika kushuhudia mchezo huo kurejea nyumbani akiwa salama.
Nipashe tunapenda kuwakumbusha wachezaji wa Simba kuepuka kufanya makosa yasiyokuwa ya lazima ili kutoigharimu timu kwa kuonyesha kadi za njano au nyekundu, na kwa kufanya hivyo, mechi hiyo itakuwa nzuri na hatimaye ndoto za kutinga hatua ya robo fainali, nusu fainali na baadaye fainali itatimia msimu huu.
Simba ikifanikiwa kusonga mbele, sio tu itajizolea mamilioni ya CAF, lakini pia itampa heshima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuona wawakilishi wote wa nchi wanafanya vizuri kwenye michuano mbalimbali wanayochuana.
Katika mchezo wa soka hakuna kisichowezekana, huu ni wakati wa Simba kupambana na kushinda mechi hiyo na hatimaye kuendeleza mazuri ambayo imeyaweka katika siku za hivi karibuni, pale inapokuwa kwenye ardhi ya nyumbani.
Mungu ibariki Simba, Mungu ibariki Tanzania ambayo kesho inaingia kibaruani kusaka tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.