Mawanda ya ukaguzi wa CAG hujikita kwenye serikali kuu, serikali za mitaa, taasisi na mashirika ya umma na vyama vya siasa, yaani kokote fedha ya umma ilikokwenda lengo ni kuwa na uwajibikaji na kuhakikisha kila shilingi inatumika vizuri.
Kila mwaka CAG huweka hadharani ili serikali ijue hali halisi na ichukue hatua, mara zote imekuwa kawaida kuonekana mchwa wanaendelea kujiimarisha badala ya kupungua au kwisha, licha ya kusomesha wataalamu, kuwa na sheria, kanuni na sera za kuongoza matumizi ya fedha ya umma.
Mathalani, kati ya taasisi 19 za umma 999 zilizokaguliwa mwaka 2020/21 zilizopata hati zenye mashaka ni sita na ambazo CAG alishindwa kutoa maoni ni nne.
Alimweleza Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa walikagua mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PSSSF wakabaini mafao ya pensheni yanazidi mapato yatokanayo na michango ya wanachama.
Vyama vya siasa vilivyokaguliwa vilivyopata hati yenye mashaka ni CUF, UDP, SAU huku hati mbaya ni ADC, CHAUMMA, UMD, TLP na Chama Cha Demokrasia Makini huku akishindwa kutoa maoni kwenye hesabu za AFP.
Kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, walibaini Sh. bilioni 47.07 zilizokopeshwa kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu hazikurejeshwa.
Hili ni jambo la kusikitisha kwa kuwa fedha hizi zilipaswa kurejeshwa ili wakopeshwe wengine na kuona thamani ya fedha kwa kuangalia mabadiliko kwa waliokopeshwa, lakini kwa kutorejeshwa inaonyesha kuna tatizo mahali lazima lishughulikiwe.
Mathalani, wakati wa mkutano wa sita wa Bunge, baadhi ya wabunge walisema mikopo hiyo inashindikana kurejeshwa kwa kuwa waliokopeshwa sio wanufaika bali kuna watu wameunda vikundi na kuzichukua huku wakiitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza.
Fedha hizo zinatukumbusha mabilioni ya JK (Jakaya Kikwete) ambayo yalitolewa kwa kila mkoa kukopesha makundi maalum ziliishia kupigwa kiasi cha lengo kitofikiwa.
CAG alisema halmashauri 83 hazikuchangia Sh. bilioni 6.68 ya asilimia 10 ya bajeti yao kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya kusaidia makundi hayo kubadilisha maisha yao.
Pia alibaini halmashauri zilifanya malipo ya Sh. milioni 556.84 kwa wastaafu waliofariki, kutoroka, kuacha kazi na waliokuwa likizo.
Alibaini matumizi yasiyo na manufaa yaliyofanyika kwa bidhaa ambazo hazijawahi kutolewa, huku kukiwa na matumizi ya fedha mbichi (fedha ambazo hazijapelekwa benki) zaidi ya Sh. bilioni 17 kwa halmashauri 147.
Kwa ujumla huu ni upigaji ambao kimsingi unakatisha tamaa walipa kodi wa nchi hii, ambao wanataka kuona fedha wanayotoa inasimamiwa vyema, inafanya kazi inayotakiwa na sio watu wachache kuiba wazi wazi na kunufaika wakati wengi wanaumia.
Fedha zilizoibwa zingeweza kununua vifaa tiba, dawa na kujenga majengo ya zahanati, vituo vya afya na hospitali, pia vingeongeza miundombinu ya shule na barabara, ili Watanzania wote wanufaike na keki ya taifa, lakini zinapigwa na wachache kwa manufaa ya wachache.
Ni muhimu walipa kodi wakaona uwajibikaji wa wazi wa kila shilingi yao, kwamba watu wakamatwe na kufikishwa mahakamani, lakini mali walizopata kwa njia haramu zifilisiwe kwa kuwa wametudhulumu Watanzania licha ya imani tuliyokuwa nayo kwao.
Bila hatua madhubuti kuziba mianya ya upotevu wa mapato hali itaendelea kuwa hii ambayo itakatisha tamaa, itaonekana serikali ni shamba la bibi kwamba mtu anaweza kuingia kwa ujanja wake akachota fedha akazitumia na kuendelea na maisha kama kawaida.
Tunaona umuhimu wa kuwawajibisha wote wanaotajwa katika ripoti ya CAG kwa kuwa ofisi hiyo ni chombo kilichopewa mamlaka hiyo, na kinatekeleza majukumu yake kwa weledi na utaalamu wa hali ya juu. Kwa lugha rahisi hakuna sababu ya kuwataja waliohusika kufanya ubadhirifu wa fedha za walipa kodi halafu hatua za kuwashughulikia zikachelewa.