Katika ajali za mwezi huu, imo iliotokea mkoani Morogoro iliyosababisha vifo vya watu 22 na nyingine ikiwamo iliyokatisha uhai wa aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Mzumbe, kampasi ya Dar es Salaam, Profesa Honest Ngowi.
Jana asubuhi matukio hayo ya kukatisha uhai wa Watanzania wenzetu yaliendelea baada ya watu sita kufa na wengine kujeruhiwa kufuatia gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kutumbukia korongoni majira ya asubuhi kwenye eneo la Nyasa (Soni) - Mombo wilayani Lushoto, mkoani Tanga likihusisha gari aina ya Fuso lililokuwa limebeba bidhaa za sokoni kutokea Lushoto kwenda wilayani Handeni.
Hakika, matukio ya kasi ya ajali za barabarani yanasikitisha na kuleta simanzi kutokana na kuondoa nguvu kazi ambayo ni tegemeo la nchi yetu katika mandeleo yake licha ya kwamba siku za nyuma zilionekana kupungua kwa kiwango kikubwa.
Kwa kuwa ajali hizo zinaendelea kupoteza maisha ya watu, tunadhani ni vyema sasa zikachukuliwa hatua madhubuti za kuhakikisha viashiria vyote vinavyoweza kusababisha ajali vinadhibitiwa.
Ni kweli kwamba, ajali haina kinga, lakini tunaamini kuwa viashiria vinaweza kudhibitiwa hasa uzembe wa madereva na mwendo usioruhusiwa unaoweza kumfanya dereva ashindwe kumudu gari na kujikuta akisababisha ajali.
Kwa kiasi fulani, ajali za barabarani zilianza kupungua, lakini ghafla tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2022, matukio ya ajali hizo yanazidi kuripotiwa kutoka maeneo mbalimbali nchini kila uchao, hivyo kuzua shaka kwamba kuna wenye dhamana wasiotekeleza majukumu yao inavyotakiwa.
Ajali hizo zinatusukuma kushauri Jeshi la Polisi hasa Kikosi cha Usalama Barabarani kukaa na kutafakari na kujitathmini ni kwa nini zimeibuka kwa kasi mwaka huu na kisha hatua zichukuliwe haraka ili kuzikomesha au kuzipunguza.
Kwa maana hiyo, tunadhani ni vyema watakafakari, je, zile tochi ambazo zilikuwa zinatumika kuwamulika madereva wasiozingatia sheria za usalama barabarani zinaendelea kufanya kazi au hapana? Kwa nini ajali zimeibuka ghafla na kwa kasi? Haya ni maswali ya msingi kujiuliza kwa lengo la kujua chanzo cha tatizo hili ni nini.
Iwapo wakatafakari na kisha kuchukua hatua, tunaamini wahusika watakuwa makini wawapo barabarani ili kuhakikisha abiria wanasafiri na kufika kule wanakokwenda bila kukatishwa uhai wao njiani na wengine kupata vilema vya milele.
Tunatambua kazi nzuri inayofanywa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, ya kukabiliana na madereva wasiozingatia sheria kwa kuwatoza faini ili waogope na kufanya kazi yao kwa umakini.
Hivyo, tunashauri kasi hiyo iendelee, kwani inawezekana ikawa imepungua na kusababisha ajali kujirudia, lakini abiria nao kwa upande wao ni vyema wasiwe wazito kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya ajali.
Hapa tunaaminisha kuwa, ili kuwa salama safarini, kila upande ufanye sehemu yake. Madereva wazingatie sheria za usalama barabara, lakini abiria nao kwa upande wao wakemee au kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapowaona madereva wakikaidi kufuata sheria, kanuni na taratibu za barabarani.
Kama kila upande utatimiza jukumu lake katika kukabiliana na ajali hizo, tunaamini kasi ya ajali inaweza kupungua kuliko kuendelea kujitokeza mfululizo kama ambavyo imetokea tangu kuanza kwa mwaka huu.
Tunalisisitiza hili kwa umuhimu mkubwa, kutokana na ajali kuchangia katika umaskini wa familia na taifa kwa ujumla.
Ajali nyingi huwa zinaelezwa kuwa chanzo chake ni uzembe wa madereva, tunawashauri wafanye kazi kwa mujibu sheria zinazowaongoza, kwani kwa njia hiyo kuna uwezekano wa kuwafikisha salama abiria kokote waendako.