WMA zielimishwe kuhusu uhifadhi kipindi cha UVIKO -19

29Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
WMA zielimishwe kuhusu uhifadhi kipindi cha UVIKO -19

HIFADHI ya Jamii ya Burunge, Wildlife Management Area (WMA), iliyoko Tarafa ya Mbugwe, Wilaya ya Babati Vijijini mkoani Manyara, yenye kilomita za mraba 283 inayomilikiwa na vijiji 10, ni moja ya eneo la utalii lililoathiriwa na uwepo wa ugonjwa wa UVIKO-19 kwa mapato yake kupungua kutokana na ...

uchache wa watalii.

Hifadhi hiyo mali ya vijiji vya Mwada, Sangaiwe, Ngolley, Vilima Vitatu, Kakoi, Minjingu, Olasiti, Maweni, Magara na Manyara ambavyo kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi vilitoa maeneo yao na kuunda hifadhi ili kulinda maliasili ya wanyamapori na uoto wa asili.

Eneo hilo limelazimika kuwa WMA kwa sababu kuna mapito ya wanyama maarufu kama Shoroba ya Kwakuchinja ambayo inaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara na Hifadhi ya Taifa Tarangire, kuwezesha wanyama kuwa salama wanapovuka kutoka eneo moja kwenda jingine.

Ili maliasili hiyo iwe salama ni lazima wananchi wahusike kuitunza kikamilifu, lakini ni lazima wajue faida za kutunza kama ilivyojitokeza kwa Burunge ambako kuna uwekezaji wa hoteli za kitalii, uwindaji na upigaji picha kitalii, shughuli ambazo huingiza mapato.

Kabla ya kuanzishwa kwa WMA hiyo wananchi walielimishwa umuhimu wa uhifadhi kutokana na ukweli wapo kwenye eneo muhimu kwa hifadhi za Taifa za Ziwa Manyara na Tarangire, walikubali kwa hiari wakamega ardhi ya vijiji.

Katika eneo hilo wawekezaji mbalimbali wamewekeza hoteli za kitalii ikiwamo inayotazama Ziwa Manyara na Ziwa Burunge ambako wanyamapori wa aina mbalimbali husambaa eneo hilo na kuwa kivutuo kwa watalii, huku mapato yakiingia kwa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Halmashauri ya Babati.

Burunge WMA ni kati ya Jumuiya 38 zinazotambulika nchini na kati ya 16 zilizosajiliwa na miongoni mwa nne zinazofanya vizuri kimapato, walianza na makusanyo ya Sh.milioni 300 ambayo yaliongezeka hadi kufikia zaidi ya Sh. bilioni 2.2 mwaka 2018/19.

Makusanyo hayo hugawanywa kwa WMA asilimia 65, TAWA asilimia 25 na halmashauri asilimia 10, kwa mwaka waliopata Sh. bilioni 2.2 kila kijiji kilipata Sh. milioni 104 kwa ajili ya shughuli za kipaumbele kwenye eneo lao kwa kadri ya mkubaliano ya wananchi.

Aidha, uwapo wa rasilimali wanyama kumewezesha kijiji cha Sangaiwe kilichopakana na Hifadhi ya Taifa Tarangire na jumuiya kujenga hoteli mbili za kitalii ambazo wamekodisha kwa mwekezaji, ambazo zimewawezesha kukusanya zaidi ya Sh. milioni 500.

Kijiji hicho kwa fedha za utalii wamejenga zahanati ya kisasa na kuweka vifaa tiba, shule ya msingi, ofisi ya kijiji ya kisasa, wametengeneza barabara kwa kiwango cha changarawe na kusomesha wanafunzi wanaofaulu kwenda vyuo vikuu.

Kutokana na UVIKO-19 wageni kutoka nje ya nchi wamepungua na sasa mapato yameporomoka hadi Sh. milioni 400, huku mgawa kwa kila kijiji ukipungua na miradi ya kijamii kusuasua, huku baadhi ya maeneo wakianza kuchangishana.

Miaka ya nyuma kutokana na michango ya kuchangia huduma za kijamii baadhi walikimbia makazi yao kukwepa michango, na sasa baadhi wameanza kujihami.

Hadi sasa WMA imeanza kuongea na wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwa kuwa UVIKO-19 itakwisha na mapato yataendelea kupatikana, lakini kubuni miradi rahisi isiyo ya gharama kubwa ambayo wananchi wataimudu.

WMA hizi zinazotunzwa na wananchi zinahitaji kuelimishwa ili wananchi wasifike mahali wasione faida ya maliasili hiyo, kwa kuwa changamoto ni nyingi ikiwamo mazao kuharibiwa na wanyamapori, watu kujeruhiwa au kuuawa, uharibifu wa mali na ujangili ambao wanafutwa machozi kwa kupata fedha za miradi ya maendeleo.

Mathalani, kwa msimu huu wananchi wa kijiji cha Sangaiwe hawatarajii kupata mavuno kwa kwua yameharibiwa na wanyamapori, lakini wanafutwa machozi na fedha za uhifadhi wanazozipata, lakini wanahitaji kusaidiwa kupata chakula ili waweze kuendelea na maisha yao ya kila siku.

UVIKO-19 tutaendelea kuishi nayo ni lazima kuzifundisha WMA namna ya kutumia raslimali zilizoko kupata fedha, kuendelea kuvutia watalii kuamini kuwa wanaweza kuendelea kutembelea vivutio hivyo na kubaki salama.

Wanyamapori ni rasilimali muhimu ambayo huliingizia taifa fedha za kigeni, inahitaji kutunzwa na jamii ndiyo inahusika moja kwa moja, ili hifadhi hizo ziendelee kuwepo ni lazima wanyama wanapopita kwenye shoroba wawe salama, na kwa wakati huu maeneo haya yanahitaji elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa uhifadhi kwa faida yao na vizazi vijavyo.

Tunaamini kwa kuwa wameshaonja faida ya uhifadhi kwenye miradi ya huduma za kijamii na kwa mtu mmoja mmoja mwanaye kusomeshwa hadi chuo kikuu, wanatambua umuhimu wa maliasili hiyo, wanawajibika moja kwa moja kuhakikisha inakuwa endelevu.