Simba jipangeni, tunataka kuwaona robo fainali CAF

28Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Simba jipangeni, tunataka kuwaona robo fainali CAF

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu, Simba wanatarajia kushuka dimbani Jumapili wiki hii kwenye mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba yenye pointi saba, itakuwa nyumbani Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikaribisha US Gendarmerie ya Niger ambayo ina alama tano zinazoifanya kuburuza mkia kwenye Kundi D ambalo pia linazijumuisha Asec Mimosas ya Ivory Coast na RS Berkane ya Morocco.

Katika kundi hilo, Asec Mimosas ambayo ipo kileleni ikiwa na alama tisa Jumapili itakuwa ugenini nchini Morocco kuvaana na RS Berkane yenye alama saba kama Simba, kila timu ikihitaji ushindi ili kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ya pili kwa utajiri kwa ngazi ya klabu Afrika baada ya Ligi ya Mabingwa.

Hivyo, ushindi pekee ndiyo utakaoiwezesha Simba kutinga robo fainali bila kuangalia matokeo ya mechi dhidi ya RS Berkane na Asec Mimosas ambayo inahitaji sare tu ili kusonga mbele.

Kwa upande wa Berkane yenyewe inahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kutinga robo fainali, lakini kama ikipoteza na Simba ikapoteza, basi Asec Mimosas na Gendarmerie ndizo zitakazotinga robo fainali.

Kwa ujumla Kundi D, ndilo gumu zaidi katika michuano hii msimu huu, na hadi sasa matokeo ya mechi za mwisho Jumapili wiki hii ndiyo yatakayoamua miamba miwili itakayofuzu robo fainali kutokana na timu zote kuwa na nafasi.

Hivyo, kinachotakiwa kwa Simba ambayo inaingia kambini leo tayari kwa maandalizi ya mechi hiyo, ni makocha kuhakikisha wanafanyia kazi makosa madogo madogo ambayo wamekuwa wakiyafanya katika mechi tano zilizopita za michuano hiyo.

Katika hilo, pia kila mchezaji hana budi kujituma na kutambua kwamba kadrii timu yao inavyosonga mbele katika michuano hiyo, ndivyo ambavyo thamani zao zinaongezeka, hivyo kujiongezea soko lao kwa kutangaza vipaji vyao kwa klabu kubwa nje ya nchi na hatimaye kuweza kubahatika kusajili na kupata maslahi mazuri zaidi.

Kwa namna ambavyo tumeiona Gendarmerie katika michezo iliyopita ya Kundi D, si timu yakuibeza hata kidogo, kwani inaweza kufanya maajabu dakika yoyote kutokana na ubora wao wa safu ya ushambuliaji ikiongozwa na winga hatari anayeongoza kwa kucheka na nyavu, Victorien Adebayor.

Lakini, Gendarmerie ni timu ya kushambulia mwanzo mwisho bila kujali inacheza nyumbani ama ugenini, hivyo benchi la ufundi la Simba linapaswa kuisuka vema safu yake ya ulinzi kuelekea mchezo huo ili kuweza kushinda na hatimaye kufuzu robo fainali.

Katika hilo pia, makosa ambayo yamekuwa yakifanywa na safu ya ushambuliaji ya Simba kwa kushindwa kutumia vema nafasi wanazotengeneza, ni wakati sasa wakufanyia kazi ipasavyo kabla ya mchezo huo.

Kingine ambacho benchi la ufundi la Simba linapaswa kuwaeleza wachezaji ni kuacha kucheza na jukwaa, lakini kufuta utamaduni wao wa kusubiri hadi kipindi cha pili ndiyo waanze kufanya mashambulizi ya kasi.

Hili tumeliona mara nyingi kwa safu ya ushambuliaji ya Simba ikisubiri hadi kipindi cha pili kuanza kushambulia kwa kasi, na wakati mwingine wanakuwa tayari wameshatangulia kufungwa, hivyo mabeki wa timu pinzani kujenga ukuta imara (kupaki basi) jambo ambalo hupata shida kuwafungua.

Hivyo, hawana budi kuhakikisha wanaumaliza mchezo 'asubuhi' tu kwa kupata mabao ya haraka, kwani mechi kama hii, kusubiri hadi kipindi cha pili ndipo waanze msako mkali wa bao, inaweza kuwagharimu katika mchezo huo ambao wanachohitaji ni ushindi tu ili kusonga mbele.

Ikumbumbukwe pia katika michuano hii, timu nyingi zinapopata bao la kuongoza, zimekuwa zikitumia kipindi cha pili kupoteza muda na kucheza kwa 'kupaki basi', jambo ambalo Simba inatakiwa kuliepuka kwa kumaliza mchezo kipindi cha kwanza, hivyo kuwafanya wapinzani wao kuwa watumwa.

Tunachotaka kukiona ni bendera ya Tanzania kwa ngazi ya klabu katika soka ikiendelea kupepea na hatimaye msimu ujao kuingiza timu nne kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), na katika hilo, hakuna njia ya mkato zaidi ya kila mpenda soka nchini na Watanzania kwa ujumla kuiombea Simba isonge mbele kwenye michuano hiyo.

Simba ikishinda Tanzania imeshinda, tunaitakia maandalizi mema.