Jitihada zinahitajika sasa kutunza misitu endelevu

05Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Jitihada zinahitajika sasa kutunza misitu endelevu

WATAALAMU na wadau wa misitu wiki iliyopita walikutana kushirikishana uzoefu na taarifa kuhusu changamoto na fursa zilizoko kwenye utunzaji na uhifadhi endelevu wa misitu katika wakati wa mabadiliko ya tabianchi.

Kwenye mkutano huo ilielezwa kuwa hekta milioni 3.9 za misitu Afrika, hupotea kila mwaka hutokana na wadudu, magonjwa, moto na shughuli za kibinadamu, huku wakitaka jitihada za makusudi za serikali za nchi kuokoa raslimali hiyo.

Jukwaa la Misitu Afrika (AFF), ndilo liliandaa mkutano huo ambao hufanyika kila mwaka kuangalia hali halisi ya misitu, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, changamoto na kuzishauri serikali za nchi husika.

Kila nchi ina sera na sheria nzuri za misitu lakini changamoto kubwa ni kuzisimamia ili zifanye kazi hadi ngazi ya chini kabisa, ambako ndiko wanajamii wanaishi na wanahusika na misitu moja kwa moja.

Wengi hudhani misitu inaota yenyewe, haihitaji kutunzwa na kulindwa, lakini hawafahamu umuhimu wake katika kuondoa hewa ukaa na kuchangia mazingira mazuri kwa ajili ya wanadamu na viumbe vingine.

Misitu husaidia kuondoa hewa chafu na kutoa hewa safi, huboresha mwonekano mzuri wa mazingira yetu, husaidia kupatikana kwa maji, mvua na kutunza uoto wa asili, huvutia wanyama na viumbe wengine lakini kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Misitu husaidia kupatikana kwa dawa mbalimbali, huku asilimia kubwa ya dawa za hospitalini zinazotengenezwa zinatokana na misitu, pia kwenye misitu hufanyika shughuli za kimila kama matambiko ya makabila mbalimbali.

Aidha, mazao ya misitu husaidia kupata mbao ambazo hutumika kuitengeneza samani na bidhaa nyingine, pia ni biashara inayoliingizia taifa fedha ambazo hutumika kwenye miradi ya maendeleo na huwezesha wananchi kurina asali.

Kasi ya kuvuna misitu kwa ajili ya biashara na matumizi ya nyumbani ni kubwa, huku ya kupanda, ikiwa ndogo jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa maisha ya viumbe wote.

Ukikata mti leo na kupanda mwingine itachukua miaka mingi kukua na kufikia uliokatwa kwa ajili ya mkaa, ndiyo maana wananchi wanaelimishwa na serikali inawajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa nishati mbadala ili waachane na kutegemea misitu.

Wapo wananchi ambao wanategemea misitu kuendeleza maisha yao kwamba watarina asali, watavuna mbao na mikaa kisha wapata kipato, ni lazima kuwaelimisha umuhimu wa kutunza raslimali hiyo hasa wakati wa mabadiliko ya tabia nchi ili iwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, wataalamu hao wamebaini kuwa changamoto wadudu waharibifu, magonjwa ya miti ya misitu na matukio ya moto kutokana na shughuli za kibinadamu ni changamoto nyingine, ambayo inapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee.

Tanzania kuna mashamba ya miti, misitu ya mikoko, mashamba ya nyuki na misitu ya asili ambayo yote iko chini ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), ambaye dira kuu ni kwa kielelezo bora katika usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki, huku dhima ni kuwa na usimamizi endelevu wa raslimali za kitaifa za misitu na nyuki ili kuchangia mahitaji ya kijamii, kiuchumi, ki-ikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Ni muhimu wadau wote kushirikiana kuangalia kwa karibu sera na sheria zilizoko kama zinatekelezwa ipasavyo hasa kwa wakati wenye mabadiliko makubwa ya hali ya tabia nchi, kuhakikisha wananchi wanashirikishwa na kuwa sehemu ya walinzi wa raslimali hiyo.

Mathalani, kuna changamoto kubwa inayokuwa kwa kasi ya udongo wenye rutuba kuzolewa kutoka mlimani kwenda bondeni kutokana na kilimo kisicho cha kisasa, maana yake tabaka la ardhi linalobaki ni ambalo halina rutuba.

Ni lazima kuangalia kwa karibu kama sera na sheria zilizoko zinakwenda na uhalisia, lakini kuwashirikisha wananchi kutambua na kutatua changamoto za misitu na mazingira kwa ujumla kwa uhalisia ili kuhakikisha misitu inatunzwa na kuwa endelevu.