Mikakati ya kilimo itekelezwe na ufuatiliaji

06Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mikakati ya kilimo itekelezwe na ufuatiliaji

JUZI Rais Samia Suluhu Hassan, alizindua mpango wa kugawa vitendea kazi kwa maofisa ugani nchini, ambao unalengo la kuboresha kilimo chini ya kaulimbiu ya kilimo na biashara, lengo ni kuwapa hamasa wakulima kuondoa zana ya unyonge, kwa kuwa zipo fursa nyingi za kuondokana na umaskini kupitia kilimo.

Katika hafla hiyo Rais Samia aligawa pikipiki 6,700 zitakazotumiwa na maofisa hao baada ya zingine 300 kutangulia, huku akisema Tanzania inakwenda kufanya kilimo cha kisasa kitakachomkomboa mkulima na kwamba imani yake ni kuwa sekta hiyo inaweza kuikomboa nchi na kuongeza mapato.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema mkakati uliopo ni kupeleka utafiti kwa wakulima badala ya kubaki kwenye makabati.

Alieleza mkakati wa kukabili upungufu wa sukari kwa kuongeza nguvu katika uzalishaji kwenye mashamba ya miwa na viwanda vilivyoingia ubia na sekta binafsi ili kuhakikisha hadi 2025 kusiwe na upungufu.

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Tanzania inazalisha tani 367,000 za sukari huku mahitaji ni 420,000.

Kwenye mafuta ya kula, Bashe alisema mkakati ulishaanza tangu msimu uliopita kwa wizara kuingilia kati bei ya mbegu za alizeti na kuziuza kwa Sh. 3,500 kilo moja badala ya bei ya wafanyabiashara ambayo ilikuwa Sh. 35,000 kwa kilo.

Hizi ni habari njema hasa ya kugawa vitendea kazi kwa maofisa ugani ambao wanahudumia wakulima wa chini kabisa yaani vijijini ambako ndiko kilimo kipo, tunaamini kwa kuwaahidi umiliki wa vifaa hivyo baada ya miaka miwili kutaongeza morali ya kazi na kuvitunza tofauti na awali ilionekana ni mali ya serikali.

Tunatambua jitihada za sasa za kuinua kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa Tanzania, huku watu zaidi ya asilimia 70 wakiwa vijijini wakikitegemea, pia walioko mjini wanategemea chakula kutoka kwa wakulima, ambao kimsingi mipango ya juu haikuwafikia ipasavyo.

Tuna Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), ambacho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1984, na vyuo vingine vya elimu ya kati na vituo vya utafiti wa kilimo, vimekuwa vikitoa wataalamu wa kilimo, vimefanya utafiti wa kuboresha kilimo, lakini bado kilio cha nchi kujitosheleza kwa chakula au kilimo kumkomboa mkulima kiko pale pale.

Tunatambua mabadiliko mengi ikiwamo ya utashi wa kisiasa na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababishwa na uharibifu wa mazingira duniani, kwa kukosekana, kuchelewa au kubadilika kwa vipindi vya mvua, lakini kuondolewa kwa tabaka la juu la ardhi kutokana na kilimo kisicho cha kitaalamu.

Mara nyingi zimezinduliwa programu na mikakati ya kuboresha kilimo zimebuniwa kama tulivyokuwa na kilimo kwanza kwa kutoa matrekta na power tiller kwa wakulima, lakini kutoa mikopo ambayo bado haikusaidia kuboresha na kufikia lengo tarajiwa.

Tunachoona bado elimu waliyopata wasomi wetu hawajajishusha na kuifanya nyepesi ya kueleweka kwa wananchi wa kawaida ambao ndiyo wanafanya kilimo, ilipaswa kuwafundisha kilimo cha wakati wa mabadiliko ya tabia nchi, badala ya kuendelea kuwa na machapisho na kufundisha wataalamu ambao wanashindwa kuhamisha elimu waliyoipata kwenye vitendo.

Zamani tuliona mabwana na mabibi shamba walivyotembelea wakulima kuwapa utaalamu wa kisasa tena hawakuwa na vitendea kazi, sasa tuna teknolojia ambayo unaweza kuzungumza na mkulima kwa simu au kumtumia ujumbe au kutumia vipeperushi na ukamfikia kirahisi bado kilimo kimeshindwa kuwa na tija tarajiwa.

Kama alivyoahidi waziri kuwa watahakikisha utafiti unafika kwa wananchi wa chini kabisa, tunapenda kuona tathmini na ufuatiliaji wa kina unafanyika kila baada ya miezi mitatu au kabla na baada ya msimu wa kilimo ili tuone mabadiliko.

Mara kadhaa, kila mwaka kunapokuwa na maonyesho ya Nanenane utaona mashamba darasa mazuri yaliyoandaliwa kitaalamu yakionyesha tija ya kilimo kwa mavuno mengi kwenye eneo dogo, lakini bado hatujaona matokeo ya maonyesho hayo kubadili maisha ya mkulima zaidi ya kutumia mabilioni ya fedha kwa watendakazi.

Tunatambua kuwa vitendea kazi hivi vimetumia fedha nyingi, kinachotakiwa ni kuona mabadiliko ili Watanzania waone thamani ya fedha yao na kama kilimo kitakuwa na mafanikio basi vijana wataondoka mjini kwenda shambani kutafuta fedha.

Leo hii tunazungumzia uhaba wa mafuta kwenye nchi yenye ardhi ya rutuba inayoweza kuzalisha mafuta yakatosheleza mahitaji, bado tunaagiza nje, lakini tunazungumzia ukuaji wa viwanda ambao unahitaji malighafi kutoka shambani.
Ni lazima kuunganisha mashamba, viwanda na miundombinu muhimu.