Serikali sasa ifuatilie kwa karibu upandaji holela bei za bidhaa

07Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali sasa ifuatilie kwa karibu upandaji holela bei za bidhaa

JUZI Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilitangaza bei mpya za mafuta ikiwa na ongezeko la Sh. 321 kwa lita ya petroli , Sh. 289 kwa dizeli na Sh. 474 ya taa yanayopokelewa Bandari ya Dar es Salaam.

Aidha, kwa Bandari ya Tanga ongezeko ni Sh. 85 kwa petroli na Sh. 295 kwa dizeli, huku wanaochukulia Bandari ya Mtwara ni ongezeko la Sh. 281 kwa dizeli huku petroli ikibaki kwa bei ya zamani.

Kupanda kwa mafuta moja kwa moja kunakwenda kuongeza bei ya bidhaa mbalimbali na kuongeza ugumu wa maisha.

Jana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwasilisha makadirio na mapato ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2022/23, aliagiza wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu kushusha bei walizopandisha pasipo kuendana na uhalisia wa soko.
 
Alisema hivi karibuni kumekuwapo taarifa za uhaba na upandaji wa bei usioendana na uhalisia wa soko katika bidhaa za ujenzi, vyakula, nishati na pembejeo za kilimo.

Kimsingi, tangu Rais Samia Suluhu Hassan, alipoeleza umma kuwa kupanda kwa bei ya vitu hakutaepukika kutokana na athari ya vita ya Russia na Ukraine, baadhi ya wafanyabiashara walipandisha bidhaa zao.
 
Aidha, wengine walipandisha kwa kisingizio cha UVIKO-19, licha ya serikali kutoa onyo mara kadhaa ikiwamo kufanya tathmini ya bei za bidhaa hizo, lakini bado zilizidi kupanda.
 
Mathalani, vifaa vya ujenzi vilizidi kupanda bei kabla ya vita, mfano nondo ya milimita 12 ilitoka Sh. 19,500 hadi 26,000, misumari kutoka Sh. 3,000 hadi 3,500, huku sababu kubwa ikiwa ni kupanda kwa bei ya chuma.
 
Pia, mafuta ya kula ya alizeti yalianza kuadimika na baadaye kupanda bei kutoka Sh. 4,500 lita moja hadi sasa ni Sh. 10,000, huku sabuni ya mche ikipanda kutoka Sh. 2,500 hadi 3,500.
 
Bidhaa nyingine ni gesi ambayo ilipanda toka Sh. 45,000 mtungi wa kg 30 hadi Sh. 55,000, hali iliyowalazimu wananchi wengi kurudi kwenye kutumia mkaa, au kupandisha bei ya vitafunwa na chips.

Kwa sasa rasmi EWURA imetangaza bei mpya ambazo zimepanda kwa kiasi kikubwa katika historia ya Tanzania, maana yake hakuna namna ya kuzuia kupaa kwa bidhaa hizo.

Kwa ujumla kauli za serikali kuwataka wafanyabiashara kushusha bei za bidhaa mara kadhaa, lakini imekuwa ngumu kutekelezwa kutokana na ukweli kuwa ni soko huria na kwamba wauzaji watashindana kwa kadri ya hali ya soko.

Februari mwaka huu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, ilifanya tathmini ya hali bei ya bidhaa na kuelekeza wafanyabiashara kutopandisha bei huku ikiahadi kuchukua hatua kali.
 
Tunatambua wizarani kuna kitengo cha Biashara, ambacho hufuatilia bei za bidhaa kila siku kwenye mikoa mbalimbali na kutoa taarifa, lakini bado haijasaidia kupunguza bei.

Tanzania kuna wasomi wengi wa uchumi wanaoweza kushauri nini kifanyike kuwapunguzia wananchi makali ya maisha, bila kulazimisha wafanyabiashara ambao wanawajibu wa kulipa kodi kupunguza makali.

Kwa nchi zilizoendelea serikali huweka ruzuku kwenye bidhaa, ili kuwasaidia wananchi wasiumie na wauzaji wasipate hasara, lakini kwa nchi zetu ni ngumu zaidi ya kufuatilia kwa karibu hali ya soko ili kuona kama bei siyo ya maumivu.

Ni lazima serikali ifuatilie kwa karibu hali kwenye masoko na maduka, ili kuona bei zinaendana na uhalisia, kwa kuwa wakiachwa kuna uwezekano wa wafanyabishara kujipanga kuwa na msimamo wa bei ambao unawatengenezea faida kubwa, huku ikiamsha umuhimu wa kuwa na umoja wa walaji ili kutetea maslahi ya wengi.

Tunashauri hivyo kwa kuwa uzoefu unaonyesha kuwa katika nchi zinazoendelea hakujawa na uelewa kuhusu mfumo wa soko huru, hivyo tusishangae hata muuza mhogo shambani kwake akipandisha bei kwa kisingizio cha mafuta na makali ya UVIKO-19.