Tahadhari muhimu udhibiti wa kirusi

23Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tahadhari muhimu udhibiti wa kirusi

WIZARA ya Afya imetangaza kuwa inafuatilia uwapo wa aina mpya ya kirusi cha UVIKO-19 kilichothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), na imeelekeza wataalamu wa afya kuangalia kama kimeshaingia nchini.

Hatua hizo zinachukuliwa kutokana na kwamba, kirusi hicho, kinajumuisha kirusi cha Delta na Omicron, ambacho kimejiunda na kuwa kirusi kipya cha Omicron BA.1, kimeshathibitishwa kuingia kwenye baadhi ya nchi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ndiye aliyetoa maelezo hayo kuwa, WHO inafanya utafiti wa kufahamu ukali wa kirusi hicho kipya, huku wizara yake nayo ikiendelea ufanya utafiti wa kuwapo kwa kirusi hicho nchini.

Pamoja na maelezo hayo, Waziri anawasihi Watanzania kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 ili kujikinga na kirusi hicho, kwa kuwa watu wengi wakipata chanjo watasaidia kupunguza madhara ya ugonjwa huo utakapothibitika kuwapo nchini.

Sisi tunaungana na serikali katika harakati za kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwamo kuchukua tahadhari zaidi ikiwamo kuhimiza watu kuchanja, kwani ni kweli kama anavyosema waziri kuwa hali ya uchanjaji bado ipo chini.

Kwani anasema, asilimia 66 ya wanaougua UVIKO-19 waliolazwa hospitalini hawajapata chanjo, hivyo tunaamini kuwa hali hiyo ni hatari kwa nchi, hivyo ingekuwa vyema kama wote tungeungana na serikali kukabili ugonjwa huo.

Tunakumbusha kuwa Tanzania siyo kisiwa ambacho hakiwezi kufikika, bali ina mwingiliano wa watu kutoka maeneo mbalimbali nchini na hata nje ya nchi, hivyo suala la kujikinga na ujio wa kirusi hicho tunaona ni muhimu. Ikumbukwe kwamba Tanzania pia inapakana na nchi zaidi ya nane.

Kwa kuwa waziri anasema baadhi ya nchi zimeshatangaza kukumbwa na kirusi hicho, ni vyema na nchi yetu tukachukua tahadhari zote zinazoelekezwa na wizara husika kudhibiti mwingiliano wa watu kutoka mataifa mbalimbali.

Lakini tukumbushe msemo wa Kiswahili kwamba; 'ukimwona mwenzio ananyolewa, na wewe tia maji', hivyo Watanzania hatuna budi kuchukua hatua zote za kutuweka salama, ikiwamo kuchanja.

Njia nyingine ambayo tunadhani ni muhimu kuchukuliwa, ni kuangalia maeneo yote ambayo yanatumiwa na watu kuingia nchini, kuanzia mipakani, viwanja vya ndege, bandarini na hata vituo vya mabasi.

Tunadhani kwamba, kuna haja ya kuhakikisha watu wote wanaoingia nchini kupitia maeneo hayo wakapimwa ili kujiridhisha ikiwa ni njia mojawapo ya kudhibiti kirusi hicho kuingia Tanzania.

Kama tulivyoeleza kuwa Tanzania siyo kisiwa ambacho hakifikiki, ni wazi suala la Mtanzania kuchukua zote zinazoelekezwa na Wizara ya Afya kwa ajili ya usalama wa afya Watanzania, tunaona ni la msingi, si la kupuuza.

Hivyo, kwa kuwa serikali imekuwa ikisisitiza suala la chanjo na kuzingatia mwongozo wa Wizara ya Afya, basi tunashauri hatua hizo zichukuliwe na ikiwezekana serikali ifuatilie kwa karibu utekelezaji wake.

Tunajua kuwa suala la chanjo ni hiari, lakini kufuata mwongozo si hiari bali kinachotakiwa ni utekelezaji tu, kuanzia kunawa maji tiririka, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na pia kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

Iwapo jamii itazingatia mwongozo huo, huku kukiwa na udhibiti maeneo yote yanayotumiwa na wageni kuingia nchini, tunaamini kirusi hicho kipya kinaweza kudhibitiwa na kisipate nafasi.

Hivyo, tunashauri udhibiti huo pia uguse 'njia za panya' zinazotumiwa na baadhi ya watu wanaoingia nchini kinyemela ili kuhakikisha wote wanajulikana wasichangie kuingiza kirusi hicho kwa njia hizo bila wao kujulikana.

Kumekuwapo na mtindo wa kusafirisha wahamiaji haramu kwa njia za panya, hivyo kwa mazingira kama hayo, tunadhani kuna uwezekano wa kirusi hicho kuingia nchini kirahisi iwapo tahadhari zote hazitachukuliwa.

Pamoja na Waziri Ummy kutangaza wiki iliyopita kuwa serikali imeondoa masharti kwa wageni kuoka nje kuhusu UVIKO-10, lakini kutokana na taarifa za kuwapo kirusi kipya, iangalie upya uamuzi wake usije ukasababisha athari.