Hatua zichukuliwe kukabili uchafuzi kwenye Mto Mara

25Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hatua zichukuliwe kukabili uchafuzi kwenye Mto Mara

MWANZONI mwa mwezi huu kuliripotiwa kuwapo uchafuzi kwenye Mto Mara mkoani Mara uliosababisha samaki kufa na kuelea kwenye mto huo.

Iliripotiwa kwamba samaki walianza kuonekana Machi 8, mwaka huu, huku maji ya mto huo yakionekana kuwa na rangi nyeusi na juu kukiwa kumetanda kilichodaiwa mafuta.

Vyombo vya habari nchini viliripoti kwamba baadhi ya wananchi walitumia fursa hiyo na kuingia mtoni na kuwaokota samaki kisha kuwauza kwa bei rahisi.

Vijiji vilivyodaiwa kukumbwa na tatizo hilo ni pamoja na Kuruya, Kwibuse na Marasibora, baadhi ya wakazi wake wakikaririwa wakisema maji hayo yalikuwa yanatoa harufu yenye ishara za kitu kilichooza na yalikuwa na utando wa kitu kama mafuta.

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria ilitoa matokeo ya utafiti wa sampuli za maji waliyopima katika maabara yao kuhusiana na uchafuzi huo, ikibainisha samaki hao walikufa kutokana na kukosa hewa ya oksijeni kutokana na kuwapo mafuta aina ya oili na grisi yaliyotanda juu ya maji eneo la Kirumi.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo maofisa wake walizuru kwenye maeneo yaliyochafuliwa, ilitangaza kuanza kwa uchunguzi kwa kuchukua sampuli za samaki hao na kuzipeleka kwenye maabara ya usalama wa chakula mjini Musoma ili kujua chanzo cha vifo hivyo.

Vilevile, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ambayo pia maofisa wake wa juu walizuru eneo la tukio, ilitangaza kuunda kamati ya kitaifa kuchunguza suala hilo.

Machi 19, mwaka huu, kamati hiyo ya kitaifa ilitangaza matokeo ya utafiti wake, ikibainisha kuwa samaki hao walikufa kutokana na uchafuzi wa maji ya Mto Mara.

Katika ripoti yake hiyo, kamati hiyo ilibainisha njia kuu mbili za uchafuzi za asili kama vile mimea kuoza na hivyo kuzalisha sumu pamoja na shughuli za kibinadamu zikijumuisha uwapo wa idadi kubwa ya mifugo iliyozalisha tani milioni 1.8 za kinyesi.

Nipashe kama mdau wa afya na mazingira, tumefuatilia kilichoripotiwa na mamlaka mbalimbali za serikali kuhusu uchafuzi huo, pia tukitembelea maeneo yaliyoripotiwa kuathirika zaidi na kuzungumza na wakazi wake.

Kwenye maeneo hayo ya waathirika wa uchafuzi huo, tulibaini kuwapo taarifa za vifo vya mifugo (ng'ombe na mbuzi) ya wakazi wa maeneo hayo vinavyodhaniwa kutokana na kunywa maji ya Bonde la Mto Mara yanayopita karibu na maeneo yao.

Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walidai kwamba walipokula samaki waliokufa kutokana na uchafuzi huo, walipata madhara kiafya, ikiwamo kuhara na kutapika.

Tukizingatia ripoti zote zilizotolewa na mamlaka za serikali kuhusu suala hilo zinabainisha kuwapo uchafuzi kwenye Mto Mara, Nipashe tunaona kuna haja serikali kuchukua hatua kukabiliana na madhara ya uchafuzi huo kwa binadamu, mifugo na mazingira.

Nipashe tunaamini kuna haja kupata mwarobaini wa kuzuia shughuli za kibinadamu zinazosababisha uchafuzi kwenye Mto Mara, ikizingatiwa kwamba kumekuwa na matukio mengi yanayohusisha uchafuzi ndani ya mto huo.

Shime, uchafuzi kwenye Mto Mara unapaswa kudhibitiwa kwa kuwa mbali na kutumiwa kama chanzo kikuu cha maji na sehemu ya kujipatia kitoweo cha samaki kwa wakazi wa maeneo unakopita, mto huo unaingia Ziwa Victoria ambalo maji yake yanatumiwa na mamilioni ya wakazi wa Kanda ya Ziwa.

Tunaona kwamba kuna sababu kwa kila mdau kujikita katika ufumbuzi wa tatizo hili badala ya kulitumia kujinufaisha kibinafsi kisiasa au kwa njia zingine za kupata fursa. Tunasema hivyo kutokana na namna makundi kadhaa ya kijamii yanavyokinzana kwa kutoa kauli zinazoonekana kutokuwa na uhalisia wake. Kwa kuwa linahusu afya za binadamu na viumbe wengine, ni vyema yakatangulizwa mbele maslahi ya taifa badala ya binafsi.