Mkakati uwepo upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini

22Mar 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mkakati uwepo upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini

MAJI ni hitaji muhimu sana katika maisha ya binadamu. Kutokana na umuhimu huo, kuna usemi kuwa ‘bila maji hakuna uhai’.

Maji yanahitajika kwa ajili ya kupikia, kunywa, kufulia, kumwagilia, viwandani pamoja na shughuli nyingine nyingi. Kukosekana kwa maji, kunasababisha shughuli nyingi kusimama, zikiwamo za nyumbani na uzalishaji mali.

Licha ya umuhimu wa maji, mahitaji ya maji katika maeneo mengi ya nchi yetu ni makubwa kuliko maji yanayozalishwa. Maeneo mengi ya vijijini yanaathirika zaidi kutokana na kutopata huduma ya majisafi na salama kulinganisha na mijini.

Hatua kadhaa zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kuhakikisha kwamba huduma ya majisafi na salama inapatikana kwa Watanzania wengi mijini na vijijini pamoja na mambo mengine, kuwawezesha wananchi kuwa na afya njema.

Kadhalika, mikakati mbalimbali imekuwa ikianzishwa na kutekelezwa kwa ajili ya kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za majisafi na salama katika maeneo ya vijijini, ambayo yamekuwa yakitoa kilio cha uhaba wa huduma hiyo kwa serikali.

Katika kuhakikisha kwamba wananchi wa vijijini wanapunguziwa kero hiyo, serikali inasema ina dhamira ya dhati kuhakikisha kwamba maji ya uhakika yanapatikana katika maeneo ya vijijini.

Aliyebainisha dhamira hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Clement Kivegalo, na kuweka wazi malengo matatu yanayolenga kurahisisha upatikanaji wa maji vijijini ikiwamo kuanzisha mfumo mpya wa kusanifu miradi kwa kutumia vyanzo vikubwa vya maji.

Aliyasema hayo mkoani Dar es Salaam katika mjadala maalumu wa kuonyesha mafanikio ya mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, na kubainisha kuwa watatumia vyanzo vikubwa kama maziwa kuhudumia vijiji vingi kwa wakati mmoja.

Mkakati wa pili alisema ni kupunguza gharama za maji vijijini ili yawe yapatikane kwa urahisi na watatu ni kuanzisha mfumo wa malipo kabla ya huduma na wanatarajia mwezi ujao kuingia makubaliano ya kimkataba na Chuo cha ufundi cha Arusha, Dar es Salaam na Mbeya ambao wameshawahakikishia kwamba wana uwezo wa kuandaa mifumo husika ambayo itatumika kirahisi na watu wa kijijini.

Alisema wanataka waunganishe na mifumo ya simu za mikononi ili mtu akiwa mjini anaweza kumnunulia maji mama yake kijijini akalipa akaenda kuchota maji kwa kutumia kadi.

Kwamba ndiyo maeneo ambayo wanataka kuyapa kipaumbele ili kupunguza gharama pamoja na kurahisisha upatikanaji wa maji vijijini.

Pia alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia wamepata mafanikio mbalimbali ikiwamo kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini pamoja na kutekeleza miradi 522 na kupeleka maji kwenye vijiji vipya 1,560 ambavyo vimewezesha zaidi ya watu milioni mbili kupata huduma hiyo.

Tunaridhishwa na hatua za serikali kuongeza miradi ya maji na mikakati hii ya kupanua wigo wa upatikanaji maji maeneo ya vijijini, lakini tunashauri kwamba mipango na mikakati tunayoelezwa itekelezwe kwa vitendo, ili wananchi wetu waondolewe vikwazo katika suala zina la upatikanaji wa huduma ya maji.

Haitakuwa vizuri kubainisha mikakati mizuri, lakini mwishowe isitekelezwe kwa visingizio mbalimbali. Tunaamini kuwa mikakati aliyoieleza Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA itatekelezwa kwa kuwa fedha zitaliwa zimepatikana au zinakaribia kuiva.

Tunatarajia kusikia mikakati na mipango mingine mingi kutoka kwa watendaji wa mamlaka za maji nchi nzima na wa Wizara ya Maji wakati huu wa maadhimisho ya Wiki ya Maji kuhusiana na walivyojipanga kubuni na kuendeleza miradi iliyoko, kwa lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa maji hususan katika maeneo ya vijijini.

Matumaini yetu yanatokana na serikali kuipatia RUWASA Sh. bilioni 79.5 ambapo wanatarajia kutekeleza miradi mingine kwenye vijiji 331 na kupitia vijiji hivyo wananchi zaidi ya milioni 1.36 watapata huduma ya maji, kupitia fedha
za UVIKO-19.