Lakini mwishoni mwa mzunguko huu ndio utakaoamua timu mbili zitakazoshuka daraja moja kwa moja kwenda kucheza Ligi ya Championship na zile zitakazoshika nafasi ya 13 na 14 ambazo zitacheza mechi za mtoano 'play off' dhidi ya timu zitakazoshika nafasi ya pili kutoka Kundi A na B kwenye Championship ili kuwania nafasi mbili za kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
Kwa ujumla ni mzunguko mgumu kwani si hilo tu, bali raundi hii ya lala salama pia ndiyo ambayo itaamua dau ambalo kila timu italipata kutokana na nafasi itakayomaliza, hii ni kutokana na hadhi iliyoongezewa na wadhamini wa haki za matangazo ya televisheni, Azam Media Limited kwa kuweka bonasi itakayolipwa kwa kila timu kulingana nafasi itakayomaliza mwishoni mwa msimu.
Kwa mujibu wa mkataba ambao Azam Media Limited na Shirikisho la Soka nchini (TFF), wameingia bingwa wa Ligi Kuu atapata bonasi ya Sh. milioni 500, huku mshindi wa pili akiondoka milioni 250, wa watatu milioni 225, wanne Sh. milioni 200, nafasi ya tano milioni 65, ya sita milioni 60, ya saba milioni 55 huku dau hilo likienda likipungua hadi kwa timu itakayoburuza mkia.
Pamoja na hayo yote, huu ni mzunguko ambao kila mchezaji hata kutoka timu zinazoburuza mkia atataka kuonyesha uwezo wake ili kujitafutia soka la kubaki Ligi Kuu ama kujiuza klabu kubwa zaidi ndani na nje ya nchi.
Hivyo, tunatarajia kuona waamuzi wakichezesha kwa umakini zaidi kwa kufuata sheria zote 17 bila kuibinya timu yoyote ili mwisho wa msimu kila moja ivune ilichostahili bila kuwapo manung'uniko yoyote.
Tunatambua klabu imewekeza kiasi kikubwa cha fedha na kila moja ina malengo yake kama si kutwaa ubingwa ni kushika nafasi nne za juu ili kujihakikishia bonasi kubwa kutoka kwa wadhamini, lakini pia kuanzia sasa zipo zinazopigana kuepuka kushuka daraja.
Kosa moja ambalo linaloweza kufanywa na mwamuzi kwa kutoa maamuzi ya kutatanisha yatakayoinyima ushindi timu moja dhidi ya nyinginelinaweza kuwa kuwa chanzo cha kupoteza ubingwa, kukosa nafasi za juu ama kushuka daraja kabisa.
Hivyo, hatutaki kuona makosa ambayo yametokea mzunguko wa kwanza kutoka kwa waamuzi yakijirudia tena raundi hii ya lala salama jambo ambalo tunawakumbusha waamuzi kuongeza umakini, lakini Bodi ya Ligi (TPLB), TFF na hata Chama cha Waamuzi nchini (FRAT), kuzidi kuwamulika wale wote wanaovurunda na kuwachukulia hatua kali ili wasiwe chanzo cha kutuamulia bingwa na timu za kushuka daraja na zile za kucheza mtoano.
Pamoja na hayo yote lakini FRAT haina budi kuwakalisha kitako waamuzi mara kwa mara na kuwakumbusha wajibu wao katika maamuzi wanayoyatoa hususan ili kuzidi kutenda haki katika ligi hiyo ambayo kwa sasa ni ya 13 kwa ubora Afrika.
Nipashe tunataka kuona malalamiko dhidi ya waamuzi ambayo yalijitokeza mzunguko wa kwanza yakimalizika kabisa ili mwisho wa msimu pasiwe na timu inatoa kisingizio katika nafasi iliyomaliza.
Si hilo tu, bali pia tunatambua bila kuwa na bingwa aliyestahili, tutaishia kupata mwakilishi mbovu kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, ambaye atakwenda kulitia aibu taifa kwa kutolewa raundi ya awali.
Lakini kama Klabu ya Simba itafanikiwa kufika mbali msimu huu kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ni wazi itakuwa imetetea nafasi nne za Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano ya CAF msimu ujao, hivyo kama waamuzi hawatatenda haki ni wazi nchi itapeleka wawakilishi wabovu katika nafasi hizo nne jambo ambalo hatutaki kuliona likitokea.
Lengo letu ni kuona timu zote zitakazopata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao zikifika angalau robo fainali na kuendelea, hivyo njia pekee ni kuanzia sasa waamuzi kutoibeba timu yoyote kwenye Ligi Kuu kwa namna yoyote ile.