Lala salama Ligi Kuu Bara iwe ya kutorudia makosa

26Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Lala salama Ligi Kuu Bara iwe ya kutorudia makosa

MZUNGUKO wa pili au hatua ya lala salama ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu wa 2021/2022 ulianza rasmi jana kwa mechi moja kuchezwa kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Nyankumbu mkoani Geita kwa wenyeji Geita Gold FC kuwakaribisha Namungo kutoka mkoani Lindi.

Kuanza kwa hatua hii ni dalili kwamba Ligi Kuu Tanzania Bara inaelekea ukingoni kwa sababu imeingia kwenye duru la mwisho ambalo linatoa bingwa na timu zitakazoshuka daraja kuelekea Ligi ya Championship nazo zitajulikana.

Katika kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri, timu , waamuzi na viongozi kila mmoja anatakiwa kutimiza vyema majukumu yake kwa ajili ya kufanikisha klabu anayoitumikia iweze kufikia malengo iliyojiwekea wakati msimu huu unaanza.

Nipashe inaamini kila timu wakati inafanya mchakato wa usajili wa wachezaji pamoja na kuajiri benchi la ufundi, iliweka mipango na malengo yake ya nini inahitaji kukipata ndani ya msimu huu na utekelezaji wake ulianzia hapo na si vinginevyo.

Hatuamini kama kuna timu ilianza msimu bila ya kuweka malengo, na kama ipo, basi haistahili kuendelea kuwapo kwenye ligi hiyo ya juu ambayo hutoa mwakilishi au wawakilishi wa nchi kwenye mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo hufanyika kila mwaka.

Timu iliyojiwekea malengo yake, inatakiwa kuendelea kutembelea ndoto hizo kwa sababu bado mechi zilizobakia ni nyingi na endapo wachezaji wake watapambana na kucheza soka la kiwango cha juu basi kuzifikia itakuwa ni jambo linalowezekana na kamwe haipaswi kukata tamaa.

Tunaamini kila timu inaweza kufikia malengo yake kwa sababu mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, hivyo timu ikijipanga sawa sawa na kutumia vyema mapungufu ya klabu pinzani, tunahakika mwisho wa msimu itakuwa na kicheko na wale ambao wataendelea kuwa wasindikizaji, watavuna walichokipanda.

Weledi huu wa viongozi, wachezaji na waamuzi pia unazihusu timu zinazoshiriki Ligi ya Championship (zamani Ligi Daraja la Kwanza) na First League (zamani Ligi Daraja la Pili), ambazo zinaendelea kwenye viwanja mbalimbali nchini, tena michezo yake ikionekana kuwa na ushindani, pengine kuliko baadhi ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Juhudi na maarifa yakifanyika vyema, basi kila timu itafikia malengo yake na kwa kuamini muda wa kurekebisha makosa bado upo, wale waliofanya vizuri katika mzunguko wa kwanza wanaweza kuharibikiwa na timu zilizojifunza kupitia makosa yao, zinaweza kuibuka na kukaa kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hizo na kujiepusha na majanga ya kushuka daraja.

Kuna makosa na mapungufu mbalimbali yalifanyika katika mzunguko wa kwanza na kusababisha baadhi ya timu kuona zinaonewa huku wengine wakifaidika na madhila hayo, tunawakumbusha wote wanaohusika na kusimamia michezo hiyo kufanya kazi kwa weledi ili mwisho wa msimu, nchi ipate bingwa ambaye anastahili kubeba taji hilo.

Huu ni wakati wa waamuzi ambao wamekuwa wakibeba lawama za kupendelea baadhi ya timu kuchezesha mechi zote kwa weledi katika duru hili la lala salama kwa ajili ya faida ya soka la nchi yetu.

Lakini pia viongozi na wachezaji kila mmoja anatakiwa afanye majukumu yake vizuri kwa ajili ya kufikia malengo, na waamini kama waamuzi hawatachezesha vizuri, basi kuna kamati husika ambayo imewekwa kuwasimamia, hivyo watachukuliwa hatua zinazostahili, ingawa inauma kwa sababu matokeo ya uwanjani hayabadilishwi na kwa yule aliyeonewa anabakia na machungu.

Msimu huu umeonekana pia kuna ushindani katika Ligi ya Championship, ambayo hutoa timu zinazopanda daraja kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Kwa maana hiyo, waamuzi na maofisa wote wanaosimamia ligi hii wanatakiwa kufuata vyema kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa ili pia kupata bingwa na wawakilishi ambao ni imara watakaopanda daraja na kuhimili ushindani kwenye ngazi inayofuata katika msimu ujao.

Katika kuhakikisha makosa ya waamuzi hayajirudii, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huandaa semina kabla na katikati ya msimu ili kuwakumbusha waamuzi namna ambavyo wanatakiwa kutekeleza majukumu yao, na hili limefanyika, hivyo wadau wa soka wanatarajia kuona mabadiliko katika uchezeshaji.

Waamuzi wanapofanya majukumu yao vizuri, kamwe hakutakuwa na malalamiko ya aina yoyote kuhusiana na upangaji wa matokeo na mwisho wa msimu timu zitakazostahili kubeba taji la Ligi Kuu, Ligi ya Championship, First League na Ligi ya Wanawake Tanzania ambayo nayo msimu huu imekuwa na mvuto atapatikana na atapigiwa makofi na klabu nyingine walizokuwa wakishindana kuwania ubingwa huo.