Kupanda bei ya gesi tishio kwa mazingira

25Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kupanda bei ya gesi tishio kwa mazingira

BEI ya gesi mtungi mdogo imepanda kutoka Sh. 20,000 hadi 25,000 huku mtungi wa kati ukitoka Sh. 53,000 hadi 58,000, ambayo hutumiwa sana na watumiaji wa nyumbani.

Baadhi ya wananchi tayari wameacha kutumia nishati hiyo badala yake wamerudi kwenye matumizi ya mkaa, ikiwa ni namna ya kukabiliana na ongezeko la gharama ambazo wanashindwa kuzimudu.
 
Kipindi cha nyuma bidhaa hiyo ilipatikana kwa bei iliyomwezesha mtu kununua na kutumia, lakini kadiri siku zinavyosonga inazidi kupanda hali inayotishia usalama wa mazingira nchini.
 
Mara kadhaa serikali imesema kasi ya uharibifu wa mazingira nchini inatisha, huku ikihamasisha upandaji miti na utunzaji mazingira kwa ujumla wake.
 
Kuna wakati taasisi kama magereza, shule na vyuo vilitakiwa kutumia gesi au nishati mbadala, ili kuachana na matumizi ya kuni kwa kuwa ndiyo ziliongoza kwa uharibifu kutokana na ukweli kuwa huhitaji kuni nyingi.
 
Licha ya maelekezo hayo utekelezaji ulikuwa mgumu kwa kuwa bei ya nishati hiyo haishikiki, hadi sasa taasisi hizo zinaendelea kutumia kuni, maana yake tani za miti zinazidi kuteketea.
 
Wazalishaji wa gesi wanasema hawajapandisha bei bali wamebaki kwenye bei elekezi, lakini uhalisia kwenye soko inauzwa bei ya juu, kiasi cha kujiuliza maswali mengi.
 
Kwa sasa dunia inapaza sauti dhidi ya uharibifu mkubwa wa mazingira unaochochea mabadiliko ya tabianchi, zipo jitihada za ndani na nje kutunza mazingira ambayo ni muhimu kwa viumbe wote.
 
Unaposafiri barabara kuu majira ya kuanzia saa 12 jioni utaona mifuko ya mkaa ikitoka porini kuja barabarani, muda huo ndiyo wanunuzi na wauzaji hujitokeza kwa kuwa inajulikana hairuhusiwi kuuza mkaa bila kibali.
 
Kama nishati hii inazidi kupanda hivi kuna hatari kubwa ya jitihada zinazofanywa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, zisiwe za mafanikio kwa kuwa mti unaokatwa leo kwa ajili ya kuzalisha mkaa itachukua miaka kadhaa kufikia umri wa kuvunwa tena.

Mara kadhaa viongozi wa serikali kwa nyakati tofauti wameeleza mpango wa kupunguza idadi ya wanaotumia mkaa, waelekee kwenye nishati mbadala, sasa nayo inazidi kupanda kiasi cha wengi kushindwa, lakini uhalisia ni tofauti.
 
Pia, viongozi hao waliwahi kueleza kuwa ujio wa gesi asilia utasaidia wananchi kusambaziwa nyumbani na kutumia kwa bei rahisi, lakini hadi sasa uhalisia wake ni finyu matokeo yake kasi ya kutumia mkaa inaongezeka.
 
Ni lazima nchi iwe na mikakati ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira, lazima wizara na taasisi zake zizungumze lugha moja, kwamba tuone Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Ofisi ya Kamishna wa Nishati Jadidifu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TAMISEMI na Wizara ya Maliasili na Utalii zizungumze lugha moja.
 
Dunia inazungumzia nishati jadidifu au nishati mbadala ambayo haiharibu mazingira, hamasa kubwa ni kuachana na uharibifu wa mazingira ambao ni tishio kubwa duniani hasa ukataji miti na matumizi makubwa ya mkaa ambayo hutoa hewa ukaa na kuharibu tabaka la juu.
 
Tayari baadhi ya visiwa Zanzibar, Rufiji, Pangani vimemezwa na maji, huku kina cha bahari na Ziwa Tanganyika kikiongezeka kwa kasi kiasi cha wananchi kushindwa kuendelea na uzalishaji.
 
Kuhamasisha wananchi waache matumizi ya mkaa bila kuwapa njia mbadala haina maana yoyote, bali ni kutwanga maji kwenye kinu jambo ambalo ni hatari kwa uhai wa kila mwanadamu.
 
Ni muhimu kuyatunza mazingira kwa jitihada kubwa, kuheshimu sheria, kanuni, sera na taratibu zilizopo, isiwe ni nyaraka za kukaa makabatini au kuacha kushughulika na tatizo.
 
Mathalani, utaona muuza mkaa anashughulikiwa na idara za maliasili kwa kukamata mkaa wake, ilipaswa kuhakikisha gesi inashuka bei kuhamasisha matumizi kwa kuwa hakuna ubishi, hakuna asiyetaka urahisi wa kufanya shughuli zake.
 
Kwa sasa hata wauza ‘chips’ na mama lishe taratibu wanaanza kurudi kwenye matumizi ya kuni, huku bei ya vyakula hivyo ikipanda kwa ambaye ataendelea kutumia gesi, hii siyo sawa.
 
Ni muhimu serikali ikaingilia kati kuhakikisha bei ya gesi inaendana na uhalisia wa maisha, kuliko kufanya kazi kwa muundo wa zima moto.