Wakulima wapewe elimu kukabili viwavijeshi, nzige

24Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wakulima wapewe elimu kukabili viwavijeshi, nzige

HIVI karibuni timu ya watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), ilitembelea Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro kujionea uharibifu katika hekari 4,976 za mpunga na 228 za mahindi zilizoharibiwa na wadudu aina ya viwavijeshi.

Wataalamu hao walikwenda pia kuwafundisha wakulima namna ya kukabiliana na wadudu hao hasa kwenye matumizi sahihi ya viuatilifu.

Pia wanatakiwa kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo kwa kuwa kuna viuatilifu vinavyoua viwavijeshi, ndiyo maana wanashauri kufuata utaalamu ili kufanikiwa.

Baadhi ya wakulima walisema kuna wenzao wameenda kununua dawa bila kufuata ushauri, walipopulizia waliendelea kuwapo, jambo ambalo ni hasara kwao.

Wakulima hao walieleza kuwa kwa zaidi ya miaka 70 ni mara ya kwanza wanaona viwavijeshi vikishambulia mpunga kwa kasi ya ajabu, jambo ambalo linahitaji msaada wa kipekee.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, alieleza viwavijeshi wako kwenye kata 12 kati yake saba zimeathirika zaidi, na kwamba serikali imepeleka lita 90 za viuatilifu vya kuwagawia wakulima.
 
 Aidha, alisema wanawasiliana na Wizara ya Kilimo ili kupata lita 1,500 za kupeleka maeneo mengi zaidi kuwasaidia wakulima kukabiliana na wadudu hao waharibifu.

Kuwapo kwa wadudu hawa ni dalili mbaya kwa usalama wa chakula kwa ujumla, ikiwa bado wakulima wa mikoa ya kaskazini hawajasahau maumivu yaliyoachwa na nzige ambao walianzia Ethiopia na kusambaa Kenya hadi Tanzania.

Ni muhimu serikali kwa kutumia wataalamu wake kupeleka elimu sahihi kwa wakulima, ili wanapoona dalili wajue ni dawa gani sahihi kwa wadudu hao, katika kuepuka uharibifu.
 
Tunatambua uwapo wa maofisa ugani kwenye ngazi za kata ambao moja ya jukumu lao ni kusaidia wakulima, wanatakiwa kuhakikisha katika mpango kazi wao kuwa wamewafikia na kuwapa elimu stahiki.

Kilimo ni uti wa mgongo ni muhimu kukipa uzito unaostahili kwa kuhakikisha wazalishaji wana taarifa sahihi ili wafanye maamuzi sahihi, tunaamini wakulima hawa wasingepoteza fedha kwa kununua dawa ambazo hazijaua wadudu kama wangekuwa wamepata taarifa sahihi.
 
Tuna vyuo vya kilimo ambavyo vinafundisha wataalamu ambao wanaajiriwa serikalini na kwenye sekta mbalimbali nchini, ipo haja kuwatumia kwa manufaa ya wazalishaji nchini.

Pia, ipo haja serikali kufuatilia kwa kina madai ya kuwapo kwa viuatilifu visivyo na ubora ambavyo wakulima wameingia hasara wakanunua, kuacha hivyo ni hasara kwao na nchi kwa ujumla kwa kuwa hawatazalisha na kiasi cha chakula tarajiwa kitapungua.

Baadhi ya wabunge mara kadhaa wakati wa Mkutano wa Sita wa Bunge walipaza sauti wakitaka kauli ya serikali juu ya kuwapo kwa viuatilifu hivyo ambavyo ni hatari.

Lazima mamlaka zifanye kazi kwa kushirikiana kukabili uingizwaji sokoni wa bidhaa hizo ambazo ni hatari kwa maisha ya watu na hasara kubwa.

Pia serikali iharakishe kufikisha viauatilifu sahihi kwa wakulima ili kuepusha madhara zaidi, hasa kusambaa kwa wadudu hao kuepusha njaa inayoweza kutokea na kuleta athari.