Kufungia mwandishi liangaliwe kwa makini

23Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kufungia mwandishi liangaliwe kwa makini

JUZI Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekonolojia ya Habari, Nape Nnauye, alisema moja ya maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari, 2016, ni kutofungia chombo cha habari bali mwandishi aliyeandika habari yenye utata.

Alisema kinapofungiwa chombo cha habari ni hasara kwa nchi, pia inaathiri wengi ambao hawahusiki kama wafanya usafi na wauzaji wa magazeti na ndiyo maana wanaona sasa ni muhimu kushughulika na mwandishi.

Tunampongeza waziri kwa kuona hilo kwa kuwa kufungia vyombo vya habari kumesababisha hasara hata kwa serikali yenyewe ambayo ingekusanya mapato kutoka kwa kampuni za wafanyakazi walioajiriwa, lakini pia wategemezi au maskini waliongezeka.

Kilio cha wadau wa habari na taasisi zake kimekuwa kikubwa muda mwingi, na wengi wamepinga uamuzi wa kufungia chombo kizima cha habari, lakini sasa linakuja jambo jingine la kumwadhibu mwandishi aliyeandika kilichosababisha matatizo.

Taasisi za wanahabari zimepaza sauti ikiwamo kuchambua sheria hiyo na nyingine zinazosimamia tasnia ya habari nchini, kwa kuainisha faida na hasara za baadhi ya vifungu, kwa namna gani vinaminya uhuru wa vyombo vya habari na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike.

Tunatambua kuwa Nape alikuwa waziri kwenye wizara hiyo hiyo wakati sheria hiyo inatungwa, alikaa kando kwa muda tunaamini alipata nafasi ya kutathmini, kujitathimini na kuona namna sheria inavyofanya kazi.

Lakini tunaamini alisikia kilio cha wadau wengi kuhusu sheria hiyo, na tunaamini hata sasa atatoa nafasi kwa wadau wote wa habari (taasisi za habari zaidi ya 12 na wanahabari wenyewe) kuzungumza naye, kuhusu mambo mbalimbali ambayo kimsingi yanakwaza utendaji kazi wao.

Tunakubalinana kuwa kufungia chombo cha habari ni kuumiza wengi, lakini lazima sasa tunapofikia uamuzi wa kumfungia mwandishi tuufahamu utendaji kazi wa vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa utendaji wa vyombo vya habari kwenye gazeti, mwandishi hana mamlaka ya kuamua kichwa maudhui ya habari yake wala kichwa cha habari zaidi atapendekeza tu, lakini siyo lazima kitumike hicho.

Aidha, mwandishi wa habari hana mamlaka ya habari yake itoke ukurasa gani, kwa uzito gani na eneo gani, hawezi kuamua ipi ikae mbele au wapi, yote jukumu la wahariri.

Wajibu wa mwandishi wa habari unaanzia kwenye kupewa kazi ya kufanya au kuwa na wazo la kutekeleza ambalo atajadiliana na mhariri, ndipo ataendelea kukusanya taarifa na zitakapokamilika atatakiwa kurudi tena kwa mhariri aliyempa kazi kwa mrejesho ndipo watakubaliana cha kuandika.

Habari inapotoka mikononi mwa mwandishi ni mali ya chombo cha habari na ndiyo maana walioajiriwa hawaruhusiwi kupeleka kwenye chombo zaidi ya kile alichoingia nacho mkataba, lakini kwa ambaye hajaajiriwa baadhi ya vyombo hawataki wasambaze kwingine kwa kuwa kuna mashindano ya kibiashara.

Mwandishi anapokabidhi habari kwenye chombo cha habari kupitia mhariri ambaye kitaalam anatambulika kama (gate keeper) kazi yake ni kuisoma kuangalia matakwa ya sheria, kanuni, sera ya chombo cha habari na weledi wa taaluma kabla ya kuruhusu itoke kwenye chombo cha habari.

Ndani ya chombo cha habari kuna kikao cha uhariri ambacho hukutana asubuhi kwa ajili ya kupanga mipango ya siku hiyo kwamba gazeti litoke na habari gani, kisha kikao cha jioni hujadili zote zilizopatikana na kuamua kitu gani kiongezwe au kipunguzwe ili kuhakikisha inakidhi vigezo muhimu.

Kwa mtiririko huo haitoshi kumwadhibu mwandishi mwenyewe kwa kuwa mhariri wake anabeba dhamana anapaswa kujiridhisha na maudhui yote anayoletewa kama yanakidhi matakwa ya kisheria, kitaaluma na sera ya chombo husika.