Serikali imeanzisha mradi huo ambao ni wa kimkakati kwa ajili ya kusaidia kuinua nchi kiuchumi, lakini cha kushangaza kuwapo kwa vitendo vya hujuma ikiwamo wizi wa mafuta unaofanywa na baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu.
Mafuta hayo ni ya magari na mitambo mingine huku wanaotuhumiwa kufanya vitendo hivyo wakidai kwamba mshahara wanaolipwa ni mdogo.
Lakini sisi tunaamini sababu za kufanya vitendo hivyo si sahihi. Ni vyema kama wanaona mshahara ni mdogo, basi wangeacha kazi kuliko kujiingizwa kwenye vitendo vinavyokwamisha miradi inayojengwa kwa fedha nyingi zinazotokana na kodi za wananchi.
Kwa mtazamo wetu, serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kufanikisha mradi huo, hivyo wanapojitokeza watu wanaouhujumu, ni wazi kwamba wanakwamisha maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla wake.
Serikali inatafuta mikopo, inatumia fedha za walipa kodi kufanya shughuli za maendeleo ukiwamo mradi huo wa treni ya umeme, hivyo kwa vitendo vya wizi, tanaamini kuwa vinatishia na kurudisha nyuma juhudi za serikali kukamilisha mradi huo wa kimkakati kwa wakati.
Watuhumiwa wa wizi huo ni vyema pia wakatambua kuwa sababu wanazotumia kuhalalisha vitendo vya wizi, hazina mashiko, kwani hata kutojua sheria haiwezi kuwa sababu ya kuhalalisha makosa.
Siku za nyuma, vitendo vya kuhujumu mradi huo viliripotiwa maeneo ya Morogoro na sasa vinazidi kushamiri na maeneo ya mkoa wa Shinyanga na Simiyu hasa kwa wizi wa mafuta yakiwamo ya magari na mitambo. Vitendo hivi ni uhujumu uchumi.
Tunadhani kwamba hujuma kama hizo si za kuvumilia, na haziwezi kuhalalishwa kwa kisingizio cha aina yoyote ikiwamo mshahara mdogo, badala yake kama mtu anaona mshahara ni mdogo, aache kazi ili nafasi yake ichukuliwe na wengine kwa kuzingatia kuwa ajira kwa sasa ni vigumu kupatikana.
Miradi yote ya kimkakati ni kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote, wanapojitokeza watu wanaoihujumu kwa kisingizio kama hicho, ni wazi kwamba wanashindwa kuwa wazalendo kwa nchi yao, hivyo sheria zilizoko ikiwamo ya uhujumu uchumi zitumike kudhibiti wahusika.
Kimsingi, tushauri kila Mtanzania kujali miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini ili imnufaishe yeye pamoja na vizazi vijavyo badala ya kuwa na ubinafsi hadi kuamua kufanya hujuma na kukwamisha maendeleo ya nchi.
Sote tunashuhudia juhudi zinazofanywa na serikali kwa ajili ya maendeleo ya nchi na watu wake kwa kuanzisha miradi mbalimbali ukiwamo huo ambao umeanza kuhujumiwa, hivyo ingekuwa ni vyema kama kila Mtanzania atatambua kuwa kinachofanywa ni kwa manufaa yake na nchi.
Hatuamiani kama mtu anayejitambua, akili timamu, mwenye uchu wa maendeleo kwa nchi yake anaweza kuthubutu kufanya vitendo hivyo vya wizi wa mafuta na vifaa vingine vinavyotumika kufanikisha mradi huo.
Tunashauri watu wa aina hiyo wasifumbiwe macho, bali ikipendekeza, msako ufanyike kila eneo lote ambalo mradi huo unapita ili kubaini vitendo hivyo na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika.
Iwapo vitendo hivyo visipodhibitiwa, inawezekana mradi usikamilike kwa wakati huku watu wachache wakineema kwa wizi na kuwaacha Watanzania walio wengi wakibaki bila kujua la kufanya.
Tunaamini kuwa serikali itachukua hatua hukakilisha miradi yote ya kimkakati kama SGR, barabara, miundombinu ya reli, viwanja vya ndege na madaraja inalindwa kwa gharama yoyote dhidi ya uhujumu, kwa kuwa ndiyo msingi na kichocheo kikubwa cha kukua kwa uchumi na nchi kupata maendeleo.










