Watumishi Afya wanastahili kulipwa posho muda wa ziada

17Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Watumishi Afya wanastahili kulipwa posho muda wa ziada

TUNAWEZA kusema kwamba watumishi wa afya ni askari wa mstari wa mbele waliopambana katika mazingira magumu ili kuokoa maisha ya Watanzania wenzao muda mfupi baada ya ugonjwa wa UVIKO-19 ulipoingia nchini mwaka 2020.

Ni mazingira magumu kutokana na ukweli kwamba wakati ugonjwa unaingia nchini, hawakuwa na vifaa vya kutosha vya kuwakinga wao, hivyo tunaamini kuwa walijitoa kuhakikisha UVIKO-19 hausambai kwa kasi nchini. Hakika walitekeleza wajibu wao ipasavyo licha ya kipindi hicho kuwa cha tishio, kutokana na wenzao wengi katika mataifa mengine walivyokuwa wakipoteza maisha.

Kama ambavyo wataalamu wa afya wamekuwa wakielezewa kuwa adui UVIKO-19 haonekani na wakati mwingine anasababisha vifo na kwamba kazi ya kukabiliana na janga hilo ni ngumu. Kwa kutambua ugumu wa kazi hiyo, serikali imesema inapanga kulipa madeni na stahiki zilizosalia za wazabuni na watumishi, zikiwamo posho ya saa za ziada kwa waliofanya kazi ya kuokoa maisha ya Watanzania wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), maelekezo yametolewa kwa Mamlaka za Mikoa na Halmashauri kuandaa madai yote ya posho za saa za ziada wanazodai watumishi wa afya waliofanya kazi usiku na mchana katika mapambano ya kukabiliana na janga la ugonjwa wa UVIKO-19.

Kauli hiyo ya serikali ilitolewa bungeni juzi TAMISEMI ilipokuwa ikijibu swali la mmoja wa wabunge, na kubainisha jinsi watumishi wa sekta hiyo walivyotimiza wajimu wao katika mazingira magumu na yenye tishio kubwa wakati ule.

Tunaunga mkono uamuzi huo, kutokana na ukweli kwamba watumishi hao walifanya kazi kubwa katika mazingira magumu ya kutokuwa na vifaa vya kujikinga na ugonjwa kwa lengo la kuokoa maisha ya Watanzania wenzao. Hatua ya serikali kuamua kulipa madeni yote ya posho za ziada wanazodai watumishi wa afya, tunadhani kwamba zinaweza kuwafanya wawe na ari na moyo wa kutimiza majukumu yao bila manung'uniko.

Vilevile, hatua hiyo tunaamini inaonyesha ni jinsi gani serikali inavyotambua mchango wao, kwa jinsi walivyojitoa kwa hali na mali na bila kuhifia maisha yao binafsi, hivyo kutanguliza mbele maslahi mapana ya taifa.

Wakati wa mlipuko wa ugonjwa nchini, ni wazi watumishi wa afya walifanya kazi kubwa usiku na mchana katika mapambano ya kukabiliana na janga hilo ambalo linaendelea kuumiza dunia.

Kitendo cha serikali kutambua mchango huo na kuahidi kulipa mabaki ya posho, tunaamini kinaonyesha ni jinsi gani inatambua, inajali na kuthamini mchango wa wataalamu hao wa afya kwa maisha ya Watanzania.

Madaktari, wauguzi, walezi na huduma za matibabu nchini, kama walivyo wenzao ulimwenguni walikabiliwa na mzigo mkubwa katika majukumu yao, hivyo tunaona hatua ya kukumbuka masalia yao ni jambo la muhimu.

Lakini pia tunawashauri watumishi wa afya kutokata tamaa wanapokumbana na vikwazo mbalimbali wakati wa kutekeleza majukumu yao, bali waendelee na moyo huo waliounyesha ugonjwa huo ulipoingia nchini.

Hawakuwa na vifaa vya kutosha kwa ajili ya usalama wao wanapohudumia wagonjwa wa UVIKO-19, lakini hawakata tamaa, hivyo tunadiriki kuwafananisha na wanajeshi wanavyojitoa mhanga kuhakikisha wanapoteza hata maisha yao lengo likiwa kulinda mipaka na uhuru wa nchi yao.

Ukweli ni kwamba, kufanya kazi katika mazingira hayo ambayo hayana vifaa au dawa, ni hatari, lakini wao wamemudu mazingira hayo hatarishi kwa lengo la kuokoa maisha ya Watanzania, tunadhani hawanabudi kupata haki zao.

Ni kweli kwamba stahiki hizo zimechelewa kutolewa, lakini hali hiyo inatokana na hali halisi ya uwezo mdogo wa serikali katika kugharimia mambo mengi.

Hatua ya serikali kupanga kulipa masalia ya watumishi hao inaonyesha jinsi gani ilivyo na dhamira ya dhati ya kuwalipa kwa kutambua kazi yao nzuri ya utumishi uliotukuka.

Tunaelewa kwamba katika miaka ya karibuni, serikali ilifuta posho za ziada kwa watumishi wa umma kwa kutumia sheria, lakini hailo hatuamini kama litakwamisha nia hiyo njema ya kutambua kazi yao nzruri na kuwaenzi.