Tayari Bunge limeshauri serikali kufanya tathmini ya hali ya shughuli za binadamu na uhifadhi kisha ichukue hatua.
Pia, kama itaona kuna umuhimu wa marekebisho ya sheria ipeleke bungeni Muswada wa Sheria ya Mabadiliko, jambo ambalo lilisemwa kama kauli rasli ya serikali na Waziri wa Maliasili na Utalii.
Aidha, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliagiza Ngorongoro kufanya semina kwa wabunge ambayo ilifanyika Jumamosi, lakini kwenye mjadala wabunge walionyesha kuwa na pande mbili za wanaotaka waondolewe na wanaotaka wabaki.
Baadhi ya wabunge walisema hali ni mbaya kwa maisha ya watu kutokana na wingi wa watu na hali ngumu ya maisha, huku uharibifu wa mazingira ukitishia uhifadhi, huku wakidai wataalamu hawajaonyesha faida za watu kuwepo ndani ya eneo hilo.
Wataalamu waliwaeleza wabunge kuwa hadi sasa ndani ya hifadhi kuna watu 110,000 wakati eneo lilitakiwa kuwa na watu 20,000 pekee, huku mifugo zaidi ya milioni 1, 074,000, huku madai ya wenyeji ikiwamo kupewa haki ya kulisha mifugo eneo la mazalia ya nyumbu na kreta.
Pia mwakilishi kwenye semina hiyo wa Shirika la Umoja wa Maitafa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), alisema hadi sasa mkataba wa urithi wa dunia umeshavunjwa na mapendelezo yalishatolewa kuwa shughuli za binadamu zimeongezeka sana.
Aidha, walieleza eneo hilo kuna kata 11 ambazo kwa ujumla wake zina vijiji 25, huku wastani wa kila kata ni vijiji vitatu, na kwamba kwa miaka mitano Baraza la Wafugaji la eneo hilo limepewa zaidi ya Sh. bilioni 35.3 kwa kipindi cha mwaka 2014.15 hadi 2018/19.
Baadhi ya wabunge hao walienda mbali kutaka iundwe kamati teule iende ikafanye uchunguzi kwa ajili ya kushauri bunge nini kifanyike, lakini jana Spika Dk. Tulia Ackson, alipoulizwa na waandishi wa habari alisema maamuzi ya bunge juu ya suala hilo yalishafanywa.
Suala la ongezeko la watu na miundombinu ikiwamo nyumba za kisasa kama ghorofa ambazo haziruhusiwi huku mifugo ikiwa mingi pamoja na mimea vamizi ambayo inasababisha wanyama kukosa malisho.
Aidha, watu 47 wameuawa na wanyama huku wengine 168 wakijeruhiwa, jambo ambalo ni hatari, huku kiwango cha umaskini kufikia asilimia 50 huku watoto wasiojua kusoma na kuandika ni asilimia 64.
Kwa ujumla kila upande unaona kuna tatizo, lakini shida ni namna ya kulitatua hasa kwa kuwa linahusu maisha ya watu, huku kukiwa na jitihada za kulinda hifadhi kwa manufaa ya Watanzania.
Hakuna ubishi hadi sasa mbinu tatu zimependekezwa ambazo ni kuwaondoa watu kwa nguvu, kuwalipa fidia na kuwahamasisha wahame kwa hiari, kinachosubiriwa ni utayari wa serikali.
Nasi tunaishauri serikali kuhakikisha busara inatumika kwanza kufanya uchunguzi wa madai kuwa kuna matajiri wachache wanamiliki makundi ya mifugo, pia watu ambao hawakustahili kuwapo humo kuingia bila utaratibu lakini watu kuliwa na kujeruhiwa na wanyama.
Ni muhimu kuwafikia wananchi kuwaelimisha umuhimu wa kupungua ndani ya hifadhi na kuridhia kwenda maeneo mengine, ili kuokoa urithi wa nchi ambao ni tegemeo katika kuliingizia taifa fedha za kigeni.
Ngorongoro ni kiini cha uhai wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA), Hifadhi ya Masai Mara Kenya na eneo la mazalia ya nyumba Loliondo na hifadhi nyingine kama Ziwa Manyara na nyinginezo.
Pia Hifadhi ya Serengeti inategemeana sana na Ngorongoro ambayo ukiua mmoja lazima wote wafe, na hata watalii wanaofurika kuona nyumbu waamao kwenda Masai Mara kwenda kubeba mimba na kuja kuzalisha nchini hawatakuwapo tena.
Maisha mseto ndani ya hifadhi ni kivutio kizuri kwa watalii lakini lazima kuhakikisha watu wanakuwapo kulingana na uwezo wa eneo kuwahifadhi kwa wale wanaotaka kuendelea kuwapo, lakini uhamaji wa nyumbu ni kivitio kingine.
Tunaamini mgogoro huu utamalizika kwa amani kwa kupunguza watu ndani ya hifadhi kwa kuzingatia haki za binadamu, na kulinda hifadhi kwa maendeleo endelevu.
Busara itumike kupunguza watu Hifadhi ya Ngorongoro
15Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Busara itumike kupunguza watu Hifadhi ya Ngorongoro
MVUTANO mkali unaoendelea kwa sasa juu ya hatua za kuchukua kunusuru Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), dhidi ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu huku haki za kila mmoja zikilindwa.










