Wanawake endeleeni na ajenda ya 50 kwa 50

18Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wanawake endeleeni na ajenda ya 50 kwa 50

MOJA ya mikakati ambayo wanawake wamekuwa nayo kwa muda mrefu hususani baada ya kufanyika kwa mkutano wa nne wa kimataifa wa Beijing nchini China mwaka 1995 ni kutaka nafasi za uongozi au kwenye ngazi za maamuzi kuwa asilimia 50 kwa 50 kati ya wanawake na wanaume.

Ajenda hiyo ilipata msukumo mkubwa duniani kote kutokana na mkutano huo uliofanyika chini ya Mtanzania, Getrude Mongella, akiwa katibu kutokana na suala hilo kuwa moja ya maazimio yake.

Hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba, uongozi si misuli bali ni akili, hivyo na wao wana akili na wamekamilika kwa kila kitu kama wanaume na wana uwezo wa kuongoza, hivyo wasitengwe kwa kuangalia jinsi.

Ajenda hiyo ya wanawake tunaona ina ukweli ndani yake, sio siri kwamba uongozi ni akili, uzoefu uwezo wa kuongoza na si kutumia nguvu, na hilo sasa limeanza kudhihirika baada ya serikali nyingi duniani kuona mantiki na umuhimu wake, hivyo kuanzisha michakato ya kuwapa fursa nyingi za uongozi.

Kwa Tanzania suala hilo sasa linatekelezwa kwa kiwango kikubwa kwa mfano Rais Samia Suluhu Hassan anatokana na jinsi hiyo huku Spika wa sasa ni mwanamke pamoja na Baraza la Mawaziri kuwa na idadi kubwa ya wanawake zikiwamo wizara nyeti kama Ulinzi, Mambo ya Nje, Afya, Utumishi kwa kutaja baadhi. Wengine wakiongoza mikoa, wilaya pamoja na wakurugenzi wa wilaya.

Tumeshuhudia jinsi ambavyo wameonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza, hivyo tunadhani ni vyema wengine wakaiga mfano huo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kupata uteuzi.

Rais Samia ameshasema kuwa atateua wanawake kulingana na vigezo bila kujali chama anachotoka, hivyo nasi tunaunga mkono maelekezo wanayopewa ya kuwataka kukuza vipaji vyao vya uongozi.

Wanaharakati wa kutetea usawa wa kijinsia, huwa wanasema kwamba kaulimbiu ya mwanamke akiwezeshwa anaweza, haipaswi kupewa nafasi kwa sasa, kwa madai kwamba wanaweza kujiwezesha wenyewe.

Tunadhani hiyo inatokana na kwamba wanajiamini, hivyo kwa kujiamini huko, tunashauri waendelee kuimarishana na kuhimizana kuchukua hatua mbalimbali za kunyanyuana ili kushika nafasi za uongozi.

Kwa njia hiyo, tunaamini kwamba wanaweza kutafutiana nafasi hata kwenye vyama vya siasa ili waongeze, kwani kama wanavyosema wao, uongozi si misuli bali ni akili na kweli wamedhihirisha hilo.

Rais amewateua kwa wingi, hivyo wito wetu ni kwamba wasimwangushe, bali iwe ni fursa ya kuonyesha kwamba wanaweza kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa maana ya tija na ufanisi kama wafanyavyo wanaume au hata kuwazidi.

Iwapo watatimiza majukumu yao kama inavyotakiwa, tunadhani kuwa watamfanya Rais azidi kuwaamini zaidi na kuendelea kuwateua kadri inavyowezekana na hatimaye ile asilimia 50 kwa 50 inaweza kufikiwa.

Kimsingi, uongozi wa nchi si wa jinsi moja bali wa wote ili mradi wahusika wawe na na sifa zinazotakiwa ikiwamo elimu, weledi, uadilifu, kujiamini , uzalendo na utu ambazo tunaona ni za msingi kwa ajili ya kutumikia umma wa Watanzania.

Tumeshuhudia kuanzia awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi hii, wanawake wamekuwa wakiteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi, lakini awamu ya sita wamekuwa wengi zaidi.

Wingi huo unaonyesha ni jinsi gani ambavyo wameweza kuibeba ajenda hiyo vizuri, kuendelea kuaminiwa. Kutokana na hali hiyo, tunadhani ingekuwa vyema iwapo watahamasishana na kupigiana chapuo kwa wale wenye sifa na vigezo vya kuongoza ili wapewe nafasi.

Waswahili wanasema kwamba, 'umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu', hivyo tunaona ni vyema wangeendelea kushikamana na kuwezeshana wanapotafuta asilimia 50 kwa 50 na inawezakana wakafanikiwa kwani dalili zimeanza kuonyesha hilo.

Hata hivyo, pamoja na Rais Samia kudhihirisha kwa vitendo utashi katika kutekeleza ajenda hiyo kivitendo kwa kuteua wanawake katika ngazi mbalimbali, wanawake wasiridhike kwa nafasi za kuteuliwa pekee, bali waende pia kugombea udiwani kwenye kata na ubunge wa majimboni wachuane na wanaume ili idadi yao iongezeke katika vyombo vya kutoa uamuzi.