Simba au Wekundu wa Msimbazi kama inavyoitwa na mashabiki wake iko katika Kundi D pamoja na US Gendamarie, RS Berkane ya Morocco na Asec Mimosas kutoka Ivory Coast.
Mechi hiyo ya kesho itakuwa ni ya pili katika hatua ya makundi baada ya Jumapili iliyopita kuanza kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Asec Mimosas, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
RS Berkane ndio vinara wa Kundi D baada ya wao kupata ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya US Gendamarie na hivyo kesho atakayepata matokeo bora ndiye atakaa kileleni kwenye kundi hilo.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanatakiwa kuingia katika mchezo huo kwa nidhamu ili wajiweke kwenye mazingira mazuri ya kusonga hatua inayofuata ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwenye ngazi ya klabu.
Kama wachezaji wa Simba wataendelea kujituma na kucheza katika kiwango bora kama walivyofanya kwenye mechi iliyopita dhidi ya Asec Mimosas, watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata ushindi na hatimaye kuendelea kufukuzana na vinara wa kundi hilo, RS Berkane.
Tunawakumbusha wachezaji wa Simba kushuka dimbani wakifahamu wanapeperusha bendera ya Tanzania, hivyo wanatakiwa kuonyesha ubora wa juu.
Wakati wa kauli ya Kocha Mkuu wa Simba, Mhispania Pablo Franco kwamba kila mechi kwao ni sawa na fainali sasa inatakiwa ionekane kwa vitendo kwa sababu mechi za hatua ya makundi ni chache na kamwe isiwadharau wapinzani wao kwa kuangalia matokeo ya mchezo wao uliopita.
Ni wazi mashabiki, wanachama na wadau wa soka nchini bado hawajasahau matokeo ya kufungwa na kutolewa na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa kuamini timu hiyo ni ndogo au wamemaliza kazi, wachezaji wanatakiwa kuwa makini katika dakika zote 90 za mchezo.
Simba inatakiwa ifahamu si Watanzania tu wanawaangalia, lakini pia wanawawakilisha wananchi wote wa Afrika Mashariki kwa kuwa ni klabu pekee kwenye ukanda huu iliyobakia kwenye michuano hiyo.
Watanzania wanatakiwa kusahau tofauti na itikadi zao za ndani kwa kuiombea Simba ipate ushindi katika mechi ya kesho na itakapopata nafasi ya kusonga mbele, itakuwa imetoa nafasi kwa nchi kuwa na wawakilishi wanne katika mashindano yanayoandaliwa na CAF katika msimu ujao.
Kimsingi ni jambo gumu kwa wapinzani wao hasa Yanga kuwaombea dua njema, lakini moyoni wanafahamu matunda ambayo Tanzania itayapata endapo Simba itasonga mbele.
Tunafahamu gharama za maisha zimepanda, lakini kama kuna mashabiki wenye uwezo, huu ni wakati wa kusafiri pamoja na timu hiyo kwenda katika mechi zake za ugenini ili kuwaongezea hamasa wachezaji.
Kama ambavyo hufanya kwa timu zote zinazoshiriki mashindano ya kimataifa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lisichoke kukaa pamoja na viongozi wa Simba kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri kwa sababu hata wao wanajua Simba ikipata matokeo chanya, sifa huwafikia wao kama wasimamizi wa mchezo huo hapa nchini.
Nipashe hatutaacha kutumia nafasi hii kuwakumbusha pia wachezaji wa Simba kucheza kwa nidhamu kwa sababu hata kama mchezaji ana uwezo lakini akikosa nidhamu, anaweza kuiweka timu yake kwenye hatari ya kupoteza pointi au yeye mwenyewe kujiondoa sokoni kwa wale mawakala wanaotafuta wachezaji.
Kila la kheri Simba, kila la kheri Tanzania katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika.










