Lakini mchezo huo dhidi ya USGN ukiwa wa kwanza kwa Simba ugenini baada ya kushinda mechi yake ya kwanza nyumbani kwa mabao 3-1 dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast iliyopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili ya Februari 13, mwaka huu.
Matokeo hayo yaliifanya Simba na RS Berkane ambayo ilishinda nyumbani kwa mabao 5-3 dhidi ya USGN, kukaa kileleni kila moja ikifikisha ponti tatu katika Kundi lao la D ambalo linatabiriwa kuwa gumu zaidi.
Ikumbukwe kuwa kwenye michuano hiyo kuna makundi manne kila moja likijumuisha timu nne na zitakazoshika nafasi ya kwanza na ya pili kutoka katika kila kundi, zitafuzu moja kwa moja hatua ya robo fainali.
Hivyo, ili kuwa na uhakika wa kufuzu kwanza ni timu kuhakikisha inashinda michezo yake ya nyumbani na angalau kuvuna pointi nne ugenini, kwa kushinda mechi moja na sare moja.
Kwa uzoefu tulionao katika kufuatilia michuano hiyo ambayo hufanyika kila msimu, ili timu kukamilisha mapema hesabu zake za kufuzu robo fainali ni kutofanya makosa katika mechi hizi tatu za mzunguko wa kwanza.
Tayari Simba imeanza vema mechi yake ya kwanza nyumbani kwa ushindi na ratiba imeangukia vizuri upande wao ambapo itacheza mechi mbili mfululizo ugenini kuanzia ya jana kabla ya kukamilishia ratiba hiyo nyumbani.
Baada ya mchezo wa jana usiku, Simba imesema itaweka kambi nchini Niger kabla ya kuifuata RS Berkane nchini Morocco kwa mechi yao ya tatu kukamilisha mzunguko wa kwanza wa hatua hiyo ya makundi.
Hivyo, kinachotakiwa kwa Simba ni kuhakikisha inapata matokeo chanya katika mechi hiyo ambayo tunatarajia ndio utakuwa mchezo mgumu zaidi kwao kuliko mingine yote ya kundi hilo.
Hata hivyo, tunaamini kwa uzoefu mkubwa Simba ilionao kwenye michuano ya kimataifa, haitaliangusha taifa na tukiwa wadau wakubwa wa michezo nchini, tunatarajia kuiona hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ya pili kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa.
Tunachotarajia kukiona ni Simba ikibeba vema jukumu hilo la kuipeperusha bendera ya Tanzania katika medani ya soka kimataifa na kuzipigania nafasi za kuingiza timu nne kwenye michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF); mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho kwa msimu ujao.
Lengo letu ni kuona kila mwaka Tanzania inakuwa miongoni mwa mataifa 12 Afrika yanayoingiza timu nne katika michuano hiyo ya CAF na katika hilo hakuna njia ya mkato zaidi ya kila mpenda soka nchini kusimama kidete kuiombea Simba kufanya vizuri kwenye michuano hiyo kwa sasa.
Ikumbukwe tayari kuna nchi 11 zenye pointi nyingi za kuziwezesha kuingiza timu 12, ambazo kwa msimu huu pekee Tanzania haiwezi kuzipiku, na nafasi iliyobaki ni moja ambayo inawania pia na Libya yenye timu mbili katika michuano hiyo ya CAF, hivyo Simba ikishindwa kufuzu robo fainali na kuendelea ni wazi tutaipoteza nafasi hiyo.
Kikubwa kwa sasa ni kila mmoja kuiombea Simba kufanya vizuri na kusonga mbele hata ikiwezekana kufika hata nusu fainali ama fainali huku tukiziombea timu hizo za Libya kuaga mapema michuano hiyo, jambo ambalo tunaamini kilichobaki ni dua zetu tu kwani kwa suala la uwezo na uzoefu hatuna shaka na wawakilishi wetu hao, katika hilo hatuna budi kuitakia kila kheri kwa majukumu hayo mazito.










