Mawaziri wafanye uamuzi mgumu migogoro ya ardhi

07Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mawaziri wafanye uamuzi mgumu migogoro ya ardhi

TIMU ya Mawaziri wanane imekwenda katika vijiji mbalimbali nchini kufanya tathmini kuhusu migogoro ya ardhi inayohusu wananchi na hifadhi.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa kazi hiyo ambayo walishaianza wakati wa uongozi wa awamu ya tano, ya kushughulikia migogoro sugu ya ardhi ambayo imekuwa ikisababisha uhasama kati ya wananchi na hifadhi.

Uamuzi wa timu hiyo kwenda katika vijiji zaidi ya 900 kwenye mikoa 10 kufanya tathmini ya kazi hiyo sambamba na kutoa maamuzi ni kufuatia agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan lengo likiwa kuitafutia migogoro hiyo ufumbuzi wa kudumu.

Ndani ya wiki hii baada ya mawaziri kuanza kazi hiyo, Serikali imefuta mapori 12 yenye ukubwa wa ekari 707, 659 na misitu 12 ya ukubwa wa ekari 46,755, kwa ajili ya kuwapatia wananchi, kuendesha shughuli za uzalishaji mali zikiwamo kilimo na ufugaji.

Hayo yalibinishwa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wakati wa ziara ya mawaziri wanane wa kisekta kutoa mrejesho wa utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 920.

Lukuvi alisema, tayari GN za Misitu na Mapori hayo, zimefutwa katika maeneo husika na  sasa taasisi zenye dhamana na maeneo ya hifadhi zinatakiwa kulinda na  kuweka alama za mipaka kwenye maeneo yaliyobaki kwa lengo la  kuepusha kuvamiwa na wananchi.

Uamuzi huo umepokelewa kwa furaha na baadhi ya viongozi wa kisiasa na wananchi katika Wilaya Kondoa, mkoani Dodoma na kueleza kuwa ni uamuzi uliolenga kuwaonea huruma wakulima na wafugaji.

Kwamba ongezeko la watu linafanya kuwe na uhitaji mkubwa wa ardhi na uamuzi wa kuwabakisha wananchi unatoa huruma kwa kuwa kulikuwa na vijana wa maliasili waliotoa adhabu kali kwa wananchi walioingia maeneo ya hifadhi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, katika vijiji 920 ambavyo timu ya mawaziri itapeleka mrejesho kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi, kwa Mkoa wa Dodoma pekee vijiji vyake 40 kati ya 42, vilivyoingia maeneo ya hifadhi havitaondolewa na wananchi wataendelea na shughuli zao za kilimo na ufugaji.

Tunaridhishwa jinsi timu hiyo ilivyoanza tathmini hiyo kwa kasi na kufanya maamuzi ambayo yatawekwa kisheria, hivyo kuipatia ufumbuzi migogoro mingi ya ardhi katika vijiji vingi nchini.

Njia shirikishi ya kutumia mawaziri wengi bila shaka maamuzi yake hayataacha shaka yoyote tofauti na kama maamuzi hayo yangefanywa na waziri mmoja, na itakuwa vizuri kama migogoro ya ardhi itaendelea kushughulikiwa hivyo kutokana na ardhi kuwa ni suala mtambuka.

Tunaelewa kwamba utatuzi wa migogoro ya ardhi una vikwazo vingi kutokana na kugusa maslahi ya kila mmoja, lakini tuna matumaini kuwa mawaziri hao kila eneo watatoa maamuzi yasiyopendelea wala kuonea mtu yeyote zaidi ya kutanguliza maslahi ya Taifa.

Tunashauri kwamba serikali iufanye utaratibu wa kutumia timu ya mawaziri wa wizara hizo kuwa endelevu katika suala zima la utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Moja ya sababu zinazochangia migogoro sugu ya ardhi ni wawekezaji wengi pamoja na matajiri kununua ardhi na kuihodhi bila kuiendeleza wakati wananchi wengi wana mahitaji kwa ajili ya kulima, kufuga pamoja na matumizi mengine.

Njia tunayoona kuwa inaweza kupunguza ukubwa wa tatizo hilo ni serikali kuweka muda maalum wa kuendeleza ardhi badala ya wamiliki kuihodhi na kugeuka kuwa mapori.