Tumewasikia watoa elimu sasa tuchanje

08Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tumewasikia watoa elimu sasa tuchanje

UTARATIBU wa kuwaendea wananchi kuwapa elimu na kuwahamasisha kuhusu chanjo ya corona umeonekana kuongeza chachu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo, baada ya idadi ya wanaochanja kuongezeka kwa kasi.

Hali hiyo inathibitishwa na takwimu mpya zilizotolewa na serikali juzi, zikionyesha kuwa hadi kufikia Oktoba 5 mwaka huu, jumla ya watu 681,736 wamepatiwa chanjo hiyo, sawa na asilimia 66 ya dozi zilizosambazwa nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, katika taarifa yake, alibainisha kuwa serikali kupitia kamati zake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea kuhakikisha elimu ya namna ya kujikinga na utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo inaendelea kutolewa kwa wananchi.

Alisema kuanza kwa kampeni ya jamii shirikishi na harakishi nchini kumesaidia kuongeza hamasa na mwitikio wa wananchi kupata chanjo, ambapo idadi ya wanaochanja sasa imepanda zaidi ya mara 10.

Kwamba mafanikio haya ya kampeni yanatokana na kuongezeka kasi ya uelimishaji wa wadau katika sekta mbalimbali ikiwamo Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na idara yake ya Habari (Maelezo), wasanii wa sanaa zote, makundi mbalimbali ya kijamii yakiwamo ya vijana, wanawake, wazee, wanamichezo, vyombo vya dini na madhehebu mbalimbali na wanasiasa.

Aliongeza kuwa suala la kuhamasisha wananchi kwa kwenda nyumba hadi nyumba limesaidia kuongeza kasi ya utoaji chanjo, huku vituo vya kutolea huduma hiyo vikiongezeka kutoka 550 hadi kufikia 6,784 vinavyotoa chanjo nchini.

Pia alibainisha kuwa Oktoba 4 mwaka huu, serikali ilipokea shehena ya chanjo za Sinopharm na kwamba inatarajia kupokea shehena ya pili leo na kufanya jumla ya chanjo zote zilizopokewa kuwa 1,065,000.

Alisema baada ya taratibu za uhakiki kukamilika, usambazaji utaanza na zitawafikia wananchi katika vituo vyote ambavyo kwa sasa vinatoa huduma ya chanjo huku elimu ikiendelea kutolewa na upokeaji chanjo utaendelea kuwa wa hiari kama ilivyoelekezwa na Rais Samia Suluh Hassan.

Kwa mujibu wa Dorothy, kutokana na uelimishaji na mwitikio mkubwa wa wananchi kupata chanjo, baadhi ya mikoa imemaliza mgawo wa chanjo za awali na imekuwa ikiomba mikoa ya jirani.

Kutokana na jitihada hizo za serikali, tunawahimiza wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi na kuwasikiliza wataalamu wa afya wanaotoa elimu na uhamasishaji kisha wachanje.

Taarifa za wataalamu wa wizara hiyo wanaofanya uhamasishaji na chanjo kwamba kuanzia Oktoba 4, mwaka huu kasi ya kuchanja imeongezeka na kwamba takribani watu 44,000 wanachanja kila siku nchini.

Tumaamini kuwa Watanzania wengi wanawasikiliza watoa elimu na kuwaelewa kuhusiana na athari za corona na hatua za kuchukua ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo hatari. Hatua sahihi ya kuwakinga dhidi ya maambukizi ni kuchanja kwa kuwa mtu akichanja anakuwa amepunguza makali ya ugonjwa huo hata kama atapatwa tena na virusi.

Wataalamu wanasema mtu aliyechanja hata kama ataambukizwa tena hawezi kupatwa matatizo makubwa tofauti na ambaye hakuchanja kwa kuwa kuna uwezekano wa kufa au kufikia hatua ya kulazwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kuwekewa Oksijeni.

Inaelezwa kwamba katika mataifa ya Ulaya wananchi wamechanja kwa zaidi ya asilimia 76, na ndiyo maana sasa wanajazana kwenye viwanja vya michezo.

Kuongezeka kwa wanaochanja kunamaanisha kwanza elimu inayotolewa inasaidia kuondoa taarifa za upotoshaji zinazotolewa na watu wachache wasioitakia mema nchi yetu. Hivyo tunawahimiza wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kuchanja, hivyo kujilinda na kuwalinda wengine.