Kabla sijaendelea, naomba niwazindue watakaopitia makala yangu kuwa kuna tofauti kati ya “stahiki” na “stahili”. Hivyo ni vyema wanaodurusu kutambua tofauti za maneno hayo mawili.
“Stahiki” ni kitendo cha mtu kuwa na haki ya kupata kitu fulani kutokana na ufanisi aliopata. “Stahili” ni kitendo cha mtu kupata adhabu kulingana na jambo baya alilofanya. mfano: “Alistahili adhabu kwa kosa alilofanya.” Chondechonde! (Tamko linalomsihi mtu asiache kufanya jambo) wanaohariri safu hii.
“Upendeleo” au “upendeleaji” ni tabia ya kufanya jambo kwa kumili yaani kitendo cha kitu au mtu kuelemea upande mmoja kimawazo au kimatendo; elemea.
“Chuki” ni hisia ya kutopenda kitu au jambo na “ chukia” ni kitendo cha mtu kutopenda mtu mwingine au kitu. Poteza mapenzi; kasirika au nuna.
“Chukiza” ni kitendo cha kufanya jambo la kuudhi; kitendo cha kiumbe kufikia kiwango cha kutopendeza kwa wengine kutokana na matendo yake.
Mchezo ni jambo linalofanywa kwa nia ya kuburudisha. Jambo ambalo watu au timu hulifanya kwa kushindana ili kupata mshindi. Kwa hali hiyo, waamuzi wanapaswa kuwa makini sana wanapochezesha michezo ya aina mbali mbali bila upendeleo wowote hata kama timu wazipendazo ndizo zinazofungwa au kuelemewa na timu pinzani.
“Rushwa” ni kitu mtu anachopokea kutoka kwa mwingine au anachotoa kumpa mwingine afanyiwe jambo kwa upendeleo. Kwa majina mengine ni mlungula / mrungura, hongo, chai, chauchau, mvugulio, kilemba.
Timu mbili zinapokuwa uwanjani huwa na wanachama na mashabiki wao wanaotoa hela nyingi ili kujiburudisha na kuzishangilia zinapopambana na zingine.
Wakati naandaa makala yangu, nililazimika kuandika kwa uchache mambo niliyoyaona wakati Yanga ilipokuwa ikipambana na timu ya Geita Gold kwenye uwanja wa Mkapa wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.
Niliyoyaona kwenye mechi ile nilikumbuka moja ya makala niliyoiandika nikiwashauri T.F.F kuwa na Video Assistant Referee (V.A.R.) itakayoweza kuwasaidia waamuzi kuangalia ili kuthibitisha au kusahihisha maamuzi watowayo na kulalamikiwa si na wachezaji tu, bali na watazamaji walio uwanjani, majumbani na kule kunakoitwa vibanda hasara!
Kuna mabao mawili yaliyofungwa na Yanga dhidi ya Geita Gold lakini kwa mshangao mwamuzi aliyakataa yote! Kwanza ni bao zuri lililofungwa dakika ya 47 na Fiston Mayele kwa pasi murua ya Yacouba lakini mshika kibendera akalikataa akidai kuwa mfungaji wa bao lile aliotea kumbe sivyo!
Kama hiyo haikutosha, dakika ya 84 mchezaji Yusuf Athumani akapokea pasi kutoka kwa Heritier Makambo na kufunga bao lakini nalo lilikataliwa na mshika kibendera akidai mfungaji alikwishaotea kabla ya kufunga hivyo likakataliwa kama lile la mwanzo!
Hata kwenye marudio yaliyofanywa na televisheni iliyoonesha mchezo ule hakuna mchezaji yeyote wa Yanga aliyeonekana kuzidi hivyo kuinyima Yanga mabao mawili!
Mpaka nilipokuwa naandaa makala hii, hakukuwa na kauli yoyote iliyotolewa na T.F.F. Kwa maana hiyo, iliridhia makosa ya waamuzi!
Hii ni mara ya pili sasa naishauri T.F.F. inunue V.A.R kwani itasaidia sana kutoa uamuzi sahihi. Kama shida ya hela, nadhani shirikisho la kandanda nchini limepokea na linaendelea kupokea fedha kutoka mashirika mbalimbali nchini. Kwa hiyo linunue V.A.R yake au liombe kwa kampuni zilizo tayari kuisaidia T.F.F. ili kuondokana na kadhia hiyo yaani jambo linalojiri; tukio la kuhuzunisha.
Jambo linaloshangaza ni kuwa wakati marefarii na washika vibendera wanaposhindwa kusimamia kanuni za mchezo uwanjani, uongozi wa T.F.F. wanaokuwa uwanjani huwa wanaangalia tu kwa macho bila kuchukua hatua yoyote dhidi ya waamuzi wanaoshindwa kuchezesha, labda kwa kutokuwa makini, upendeleo au vinginevyo. Wanastahili adhabu.
Mkosa ni mtu anaetenda kinyume cha sheria au taratibu za jamii. Wasimamizi wa jambo lolote hupewa kanuni na taratibu za kusimamia kazi zao. Kama wanashindwa kutimiza wajibu, waoneshwe mlango wa kutokea badala ya kuharibu kanuni za mchezo upendwao na wengi.
0784334096










