Uporaji mali ajalini ni uhalifu, udhibitiwe

06Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Uporaji mali ajalini ni uhalifu, udhibitiwe

KUNA matukio ambayo yanaendelea kwa kasi katika maeneo yote ya Tanzania, ambayo wananchi wanapora mali za abiria zinapotokea ajali barabarani.

Kadhalika, wananchi hao wanavamia magari ya mizigo na kupora mali baada ya kutokea ajali. Tumekuwa tukishuhudia uporaji huo malori yanapoanguka na kodondosha bia, soda, saruji na wakati mwingine kuchota mafuta kwa kutumia madumu, ndoo na vifaa vingine.

Kibaya zaidi ni kwamba wananchi hao wanawapekua majeruhi na hata maiti kwenye mifuko na kuwanyang’anya fedha badala ya kuwapa msaada ikiwamo kuwapeleka hospitali au kuwahifadhia mali zao,

Vitendo hivyo hivi sasa vinaonekana kama vya kawaida, lakini ukweli ni kwamba ni uhalifu kama mwingine, ambao vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinapaswa kuuchukuliwa hatua.

Yametokea matukio mengi ya aina hi na la karibuni ni la juzi Mbagala Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo wananchi walivamia lori la saruji na kuanza kuiba saruji baada ya kupata ajali katika eneo la Misheni, Mtaa wa Kizinga.

Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwa eneo hilo, baada ya lori hilo kufika eneo la Misheni lilifeli breki na kuanza kuteremka chini kwenye makazi ya watu na kugusa daladala mbili kwa upande wa nyuma pamoja na nyumba.

Kwamba ndipo wananchi hao walivamia na kuanza kuchukua mali za watu waliokuwamo katika lori hilo pamoja na kuanza kuiba saruji.

Kutokana na jinsi ambavyo wananchi walikuwa wakitumia nguvu nyingi kupora saruji na mali nyingine, waliokuwamo kwenye lori iliwabidi wakimbie kwa ajili ya kuokoa maisha yao.

Miaka iliyopita yalitokea matukio mengi ya aina hiyo, ambayo yalisababisha vifo vya baadhi ya wananchi waliokuwa wakijaribu kupora mali baada ya ajali. Kwa mfano, mkoani Mbeya watu kadhaa walikufa walipokuwa wakichota mafuta baada ya lori kuanguka.

Mwaka juzi takribani 100 walikufa katika Manispaa ya Morogoro kwa kuungua walipokuwa wanachota mafuta, huku baadhi wakiwa ni wapiti njia baada ya lori la mafuta kuanguka.

Mwendelezo wa vitendo hivi vya kikatili sio tu kwamba vinasababishwa na umaskini miongoni mwa Watanzania, bali ni tamaa ya kutaka mali bila kufanyakazi pamoja na kutokuwa na hofu kwa Mungu.

Kutokana na hali hiyo, tunashauri kwamba sasa ni wakati mwafaka kwa jamii kuvichukia vitendo hivyo, ambavyo kama havitadhibitiwa, upo uwezekano wa kushuhudia majeruhi na abiria wengine wakidhuriwa na watu hao ambao hawathamini uhai wa binadamu.

Inawezekana wananchi wengine wanajiingiza kwenye uporaji huo kwa mkumbo bila kujua kuwa huo ni uhalifu, hivyo tunashauri kwamba zichukuliwe hatua, na kwa kuanzia utoaji wa elimu kwa umma hususan kwa wakazi wanaoishi katika maeneo ya barabara.

Nyingine ni kwa mamlaka zinazohusika na utekelezaji wa sheria hususan vyombo vya dola kuzitumia sheria zilizoko kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wote watakaobainika wakipora mali kwenye ajali.

Tunaamini kwamba kwa kufanya hivyo, ukubwa wa tatizo hili utapungua, hivyo abiria na bidhaa zinazosafirishwa kufika salama. Udhibiti huo pia utawaepusha wananchi kuepukana na majanga ambayo yamekuwa yakitokea, ikiwamo kuteketea wanapovamia magari ya mafuta.