Serikali yakiri mlundiko wodi kinamama

14Apr 2018
Augusta Njoji
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali yakiri mlundiko wodi kinamama

SERIKALI imekiri kuwapo kwa changamoto ya wajawazito na waliojifungua kulala kitanda kimoja hali inayochangiwa na ufinyu wa nafasi kwenye jengo la wazazi katika hospitali ya Rufan ya Mkoa wa Rukwa.

Aidha, serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetenga Sh. bilioni 100.5 katika mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za halmashauri 67, ikiwamo za mkoa huo na kila mmoja imetengewa Sh. bilioni 1.5.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Faustine Ndugulile, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Aida Khenani.

Alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo hilo katika hospitali hiyo.

Dk. Ndugulile alijibu ongezeko la idadi ya watumiaji wa huduma imetokana na hospitali hiyo kuanza kama kituo cha afya mwaka 1974.

“Vile vile tatizo hili linachangiwa na ukosefu wa hospitali za wilaya katika halmashauri za Kalambo na Sumbawanga, hali inayochangia hospitali ya rufani ya mkoa kuhudumia wateja wote wanaotoka kwenye halmashauri zote mbili,” alisema Ndugulile.

Hata hivyo, alisema wizara imeweka mikakati mbalimbali ya ufumbuzi wa changamoto hizo.

Alitaja moja ya mikakati ni kupitia mpango kabambe wa hospitali ya mwaka 2017/18 wa CHOP, wizara imekamilisha ukarabati wa wodi mbili hivyo kuongeza nafasi ya vitanda vya ziada 20, ambavyo tayari vinatumika na hivyo kupunguza msongamano.

Aidha, alisema serikali inafanya ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya vituo vya afya sita ambavyo ni Mazwi, Nkomolo, Kirando, Mwimbi, Legeza mwendo na Milepa, ndani ya mkoa ili kupanua wigo wa huduma za kujifungua kwa njia ya upasuaji.

“Hatua hii itapunguza tatizo la wajawazito wengi kupewa rufani kujifungua katika hospitali ya rufani ya mkoa,” alisema.