Mo aipa Simba siku 3 kuinunua

31Dec 2015
Nipashe
Mo aipa Simba siku 3 kuinunua

BILIONEA aliyetenga Sh. bilioni 20 kuinunua Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, ameupa uongozi wa klabu hiyo siku tatu uwe umeamua kuhusu kukubaliana ama kutokukubaliana na mpango wake huo.

Mohamed Dewji ‘Mo’

Mo, bilionea kijana zaidi Tanania, ametenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuiendesha kibiashara klabu hiyo kongwe nchini.
Wakati uongozi wa Simba umemtaka Mo kuwasilisha maombi rasmi juu ya mpango huo, mfanyabiashara huyo ameupa siku tatu kuanzia juzi hadi leo Desemba 31 uwe umeweka wazi msimamo kuhusu suala hilo.
Mo alikaririwa na moja ya vituo vya redio vya jijini Dar es Salaam jana akieleza kuwa anataka viongozi wa Simba chini ya Rais Evans Aveva, waamue moja kama wako tayari ama la. Wasipompa jibu ndani ya muda huo, hataendelea tena na mpango huo.
Mo alidai kuwa aliwahi kukutana na uongozi wa Simba (Aveva aliyekuwa na Kassim Dewji na Musley Ruhwehi ofisini kwake na kuwaeleza dhamira yake hiyo), lakini bado hawajampa jibu.
Mfanyabiashara huyo amepanga kuwekezaji katika klabu hiyo kwa kusajili wachezaji mahiri na kujenga uwanja wao wa Bunju ili wapate kituo maalum cha kulea vipaji vya vijana.