Idadi hiyo ya mabao ambayo ni wastani wa mabao mawili kila mechi, tayari imeshaipiku rekodi ya raundi 23 za awali msimu uliopita wa ligi hiyo zilizokuwa na mabao 335 yaliyofungwa katika mechi 181.
Magoli hayo yamefungwa na wachezaji 151 wakiongozwa na straika wa kimataifa kutoka Uganda anayekipiga Simba, Hamisi Kiiza aliyeona nyavu za wapinzani mara 18.
Takwimu za Nipashe zinaonyesha kuwa kati ya mabao yote, 23 yametokana na mapigo ya penalti. Jumla ya penalti 35 zimetolewa (12 zilibuma) -- Raphael Alpha wa Mbeya City anaongoza akifunga penalti nne (hajakosa hata moja) akifuatwa na Salum Kanoni wa Kagera Sugar (3) na Ally Ramadhani wa African Sports (2).
Mabingwa mara 25 wa Tanzania Bara (Yanga) wamefunga mabao 51 (14% ya magoli yote) katika mechi 21 walizokusanya pointi 50, wakipewa penalti sita -- walikosa tatu -- Simba na Mwadui FC zimekosa penalti mbili kila moja.
Vinara wa msimamo kwa sasa Simba wanakamata nafasi ya pili katika utupiaji magoli wakiwa wamefunga mara 41 katika mechi 23 walizokusanya pointi 54.
Takwimu za gazeti hili pia zinaonyesha mzunguko wa kwanza wa VPL msimu huu ulikuwa na mabao 250. Tayari kuna 'hat-trick' tano zilizopigwa na nyota wanne -- Kiiza (Simba 3-1 Kagera), Ibrahim Ajibu (Simba 6-1 Majimaji), Amissi Tambwe (Yanga 4-0 Stand Utd, Yanga 5-0 Majimaji) na Mbarouk Yusuph (Kagera 3-0 Coastal).
Raundi ya 10 ndiyo inashikilia rekodi ya kuwa na mabao mengi zaidi msimu huu (28), wakati raundi ya sita ndiyo yenye mabao machache zaidi hadi sasa (6).
Imeandikwa na Sanula Athanas na Adam Fungamwango










