Mechi hiyo ya raundi 24 ya Ligi Kuu Tanzania Bara, itazikutanisha timu hizo ndugu kwenye Uwanja wa Kambarage.
Kikosi cha kocha mzawa Adolf Richard kitashuka uwanjani kikiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union.
Mtibwa inayonolewa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Mexime, nayo ina rekodi nzuri ya kushinda mechi mbili zilizopita dhidi ya JKT Ruvu na Coastal Union.
Hata hivyo, vijana wa Mexime huenda wakakumbana na upinzani mkali kutoka kwa nyota wa Kagera ambao si tu kwamba wanahitaji kulipa kisasi cha kipigo cha Oktoba 28 cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa Manungu, bali wanapambana kuhakikisha timu hiyo haishuki daraja.
Kagera kwa sasa iko nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi ikiwa na mtaji wa pointi 22 baada ya mechi 23, wakati Mtibwa wanashika nafasi ya nne wakiwa na pointi 39 baada ya mechi 21.
MECHI TATU ZILIZOPITA
KAGERA
1. Kagera Sugar 3 - 0 Coastal Union
2. Tanzania Prisons 1 - 1 Kagera Sugar
3. Toto Africans 1 - 1 Kagera Sugar
MTIBWA
1. Mtibwa Sugar 2 - 1 JKT Ruvu
2. Mtibwa Sugar 3 - 0 Coastal Union
3. Majimaji 1 - 0 Mtibwa Sugar
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi mbili, vinara wa msimamo Simba wakiwa wageni wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Majimaji watawakaribisha Mbeya City mjini Songea.
Stand United ambayo imepoteza mechi nne mfululizo, itakuwa na nafasi ya kurekebisha makosa itakapowaalika Ndanda FC mjini Shinyanga.










