Kabla ya mechi hiyo, Simba ilipanda kileleni wakifikisha pointi 48 na kuipiku Yanga kwa pointi moja baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-0 Jumapili iliyopita kwenye Uwanja huohuo.
Kwa ushindi wa jana, mabingwa Yanga sasa wamefikisha pointo 50, mbili mbele ya Simba inayoshika nafasi ya pili na tatu dhidi ya Azam FC inayoshika nafasi ya tatu.
Hata hivyo, matokeo hayo ni mabaya kwa African Sports inayoendelea kuganda nafasi ya 15 kati ya timu 16, ikiwazidi kwa pointi moja wenzao wa Tanga, Coastal Union wenye pointi 16 wakiburuza mkia.
Kocha wa vijana hao wa Tanga, Ramadhan Aluko alisema kikosi chake kimepoteza mchezo kutokana na kushindwa kwenda sambamba na kasi ya uzoefu wa wachezaji wa Yanga kwenye mechi za Ligi Kuu.
Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, alisema dakika 30 za kwanza mchezo ulikuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kulinda lango vziuri, hata hivyo uzoefu wa wachezaji wake ulisaidia kupata ushindi huo mnono.
Yanga iliandika bao la kwanza dakika 32 tangu filimbi ya kwanza kupulizwa kupitia ka beki Kelvin Yondani aliyemtungua kipa wa African Sports kwa shuti akiunganisha krosi ya kiungo Haruna Niyonzima.
Donald Ngoma alifanya matokeo kuwa 2-0, akifunga bao lake la 12 msimu huu katika dakika ya 37 akimalizia krosi ya Juma Abdul.
Mshambuliaji Amiss Tambwe ambaye amekuwa akifunga mfululizo kwenye mechi za kikosi hicho cha Jangwani, alifunga mara mbili kwenye mchezo huo kufikisha mabao 17 msimu huu akimpiku Hamis Kiiza wa Simba mwenye mabao 16.
Alifunga bao la tatu kwa Yanga katika dakika ya 51 baada ya kumzidi maarifa kipa wa Sports, Kabali Faraji aliyetoka nje ya 18 kumkabili, kabla ya kutikisa bao la tano kwa kiki ya kushtukiza nje ya boksi la hatari dakika ya 72.
Bao la nne la Yanga lilifungwa kwa kichwa na Matheo Anthony aliyetumia dakika moja tu tangu aingine uwanjani kuchukua nafasi ya Ngoma dakika ya 57. Alitikisa nyavu baada kumalizia kazi nzuri ya Haji Mwinyi.
Bao hilo tamu la kichwa lilikuwa la kwanza kwake katika mechi za Ligi Kuu tangu asajiliwe Jangwani kutoka KMKM ya Zanzibar.
Mbali na kuibuka na ushindi huo, Yanga ingeweza kurudi Jangwani na kapu la mabao kama washambuliaji wake wangetumia vizuri nafasi nyingi za wazi kufunga.
Ushindi huo ni salamu tosha kwa APR ya Rwanda wanayokwenda kukutana nayo mwishoni mwa wiki hii katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mjini Kigali, Rwanda.
Kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kevin Yondani, Vincent Bossou (Paul Nonga dk 77), Pato Ngonyani, Deus Kaseke (Salum Telela dk64), Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Donald Ngoma (Matheo Anthony dk 57) na Haruna Niyonzima.
Kikosi cha African Sports kilikuwa; Kabali Faraji, Mwaita Gereza, Hamza Kassim/Khalfan Twenye (dk 61), Juma Shemvuni, Rahim Juma, Hussein Issa, Pera Mavuo, Rajab Isihaka, James Mendi na Omari Issa.










